Ligi daraja la kwanza hatua ya lala salama imeendea kushika kasi katika viwanja mbalimbali huku ikishuhudiwa vilabu kadhaa vikionesha nia thabiti ya kutaka kupanda daraja na kucheza katika ligi kuu msimu ujao kwa kujikusanyia alama muhimu katika kila mchezo.
Kwenye kundi A ambalo klabu ya Majimaji ya Songea imo limeonekana kuwa na upinzani mkubwa sana na matokeo ya kushangaza sana katika kuwania nafasi mbili muhimu za kupanda kwaajili ya kushiriki ligi kuu nchini Tanzania, kwani ukiutazama msimamo ulivyo katika kundi hilo unaweza kuona namna ambavyo mpambano umekuwa mkali.
Mpaka sasa klabu ya Majimaji inaongoza msimamo wa kundi hilo ikiwa tayari imekwishajikusanyia alama 35 mara baada ya kujitupa dimbani takribani mara 16, ikifuatiwa na klabu ya African Sports ya Jijini Tanga yenye alama 32 ilizojikusanyia baada ya kushuka dimbani takribani mara 16 ikiwa ni michezo sawa na vinara wa kundi klabu ya Majimaji huku Lipuli ya Mjini Iringa aka Wanapaluhengo iko katikaa nafasi ya 3 ikiwa na alama zake 28 mara baada ya kushuka dimbani takribani mara 16.
Tangu kuanza kwa ligi hiyo kumekuwa na tuhuma zisizo na msingi na ukweli wowote dhidi ya klabu ya Majimaji kuwa imekuwa ikipendelewa sana kwenye michezo yake ya nyumbani ili kuhakikisha kuwa timu hyo inapanda daraja msimu huu.
Mmoja kati ya watu ambaye bila ya aibu na kukosa uungwana aliamua kuinyooshea kidole klabu ya Majimaji kuwa imekuwa ikipendelewa na kuingilia michezo yao ili wao wafungwe na kutoka kwenye mbio za kupanda daraja ni kiongozi mwandamizi wa klabu ya Friends Rangers, Herry Mzozo ambaye alizungumza na kituo cha redio cha Clouds Fm cha jijini Dar es salaam {Sports Extra ya tarehe 15/01/2015} na kudai kuwa kupoteza kwao kwa michezo yao ya nyumbani na ugenini kwa siku za hivi karibuni kunatokana na klabu ya Majimaji kuwarubuni waamuzi wanaochezesha michezo yao ili wao wapoteze michezo hiyo na hatimaye watoke kwenye mbio za kupanda daraja msimu huu.
Kinachonishangaza mimi kwenye kauli yake hiyo ni kuwa wakati Mzozo akitoa tuhuma hizo, ni kuwa siku hiyo hiyo ambayo klabu yake ya Friends Rangersilipoteza mchezo dhidi ya wanadaresalama wenzao klabu ya Ashanti United kutoka mitaa ya Ilala pia klabu ya Majimaji ilikua imejitupa ugani kucheza dhidi ya timu ya Polisi Dar kwenye dimba la Majimaji.
Uongozi wote wa klabu ya Majimaji ulikuwepo kwenye dimba la Majimaji ukiwatazama manduna wao wakipambana kuzisaka alama tatu muhimu tena ikiwa ni siku moja tu tangu wampokee mkurugenzi wao wa ufundi Muingereza Stewart John Hall aliye wahi kuwa kocha wa klabu ya Azam na timu ya taifa ya Zanzibar almaarufu kama Zanzibar Heroes.
Kinachonifanya nibakie kinywa wazi kwa kujiuliza maswali yanayokosa majibu ni jinsi gani uongozi wa klabu ya Majimaji unavyoweza kuwahonga waamuzi wa mchezo wa Dar es salaam huku wakiwa mjini Songea na kama hayo yanawezekana kwanini pia asiwahonge waamuzi wa mchezo uliokuwa unachezwa Tanga kati ya African Sports na KMC {Tessema} ambapo Sports ameonekana kuwa na madhara makubwa kwa upande wa Majimaji kuliko Friends Rangers kwa sasa?
Hali kadharika kituo cha redio cha Clouds Fm kupitia kipindi chake cha Sports Extra mara kadhaa kimekuwa kikitoa ripoti ambazo hazina ukweli juu ya masuala ya UZALENDO kwenye dimba la Majimaji kwa mmoja wa watangazaji wake kwenye kipindi cha tarehe tunayoihifadhi kutamka kuwa 'UKITAKA KUONA UZALENDO UWANJANI NENDA SONGEA UKAONE' jambo ambalo si tu kuwa limekuwa likiniacha mdomo wazi bali limekua likiwapoteza wadau na wasikilizaji wa kipindi chao kwenye mkoa huu wa Ruvuma walioanza kusikika hivi karibuni lakini pia ni uzushi uliopitiliza kutokana na ukweli wa mambo ulivyo kwenye dimba hilo.
Binafsi ninawaheshimu na kuwaamini sana timu nzima ya Sports Extra ya 88.4 Clouds Fm ambayo wao wanadai kuwa ni zaidi ya sports Tanzania, na nina imani kuwa ina watu wenye weledi mkubwa wa kufanya kazi na binafsi huwa nawafananisha na katapila ambalo linafanya kazi ya kuchinga njia kwani ni ukweli usiopingika kuwa wao ni kituo cha kwanza kabisa kuanza kufanya michezo ya dunia ya sasa {modern sports}
Wakati mwingine huwa najiuliza swali dogo sana kuhusiana na kauli zinazotolewa na watu mabali mbali na redio mbali mbali kuhusiana na suala la uzalendo mjini Songea kuwa hivi ni kweli watu hao na kituo cha Clouds wameshindwa kabisa kuja mjini songea kimya kimaya {Kinyemela} na kuutazama angalau mchezo mmoja wa klabu ya majimaji na hatimaye kuupata ukweli wa tuhuma zinazotolewa za uwanja huu kuwa na uzalendo uliopitiliza?
Wakati fulani nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania na klabu ya Yanga, Shadrack Nsajigwa 'Fusso' aliwahi kuja Songea kwa lengo la kuja kufanya kazi ya ung'amuaji wa vipaji aliyotumwa na klabiu yake ya Yanga na kushuhudia mchezo wa mwisho wa raundi ya kwanza na kujionea hali ya mambo ilivyokuwa kwenye mchezo huo uliokuwa umejawa na ufundi mwingi huku akishuhudia klabu ya Majimaji ikiibuka na ushindi wa jumla ya magoli 3:1 dhidi ya Kimondo Fc kutoka kule Mbozi Mbeya.
Mara baada ya mchezo huo mimi binafsi na mkurugenzi wangu wa Jamvi la habari communications tulifanya mahojiano na Nsajigwa kuhusiana na kile alichokishuhudia na haya hapa chini ni maoni yake kuhusiana na suala la klabu ya Majimaji kupendelewa.
Kinachonishangaza mimi ni kuwa iwapo Nsajigwa na Yanga waliamua kuingia kimya kimaya mjini Songea kwa minajiri ya kuja kufanya kazi hiyo inakuwaje kwa redio yenye zaidi ya muongo mmoja kushindwa kufanya hivyo? Labda kuna mambo makubwa mawili yaliyomo hapa mjini Songea na ndani ya klabu ya Majimaji ambayo pengine watu mliopo nje ya Songea hamuyafahamu kuhusiana na timu hii kwa sasa.
Jambo la kwanza ni juhudi za dhati za za Mbunge wa Songea mjini mheshimiwa Dr. Emmanuel John Nchimbi katika kuhakikisha kuwa badala ya timu kuendeeshwa kwa kutumia pesa zake au pesa za mifukoni basi timu ipate udhamini wa uhakika kutoka kwa makampuni mablimbali.
Dr Nchimbi hakuanza leo wala jana harakati zake hizo za kuisaidia klabu ya Majimaji na kuhakikisha kuwa timu inafanya vizuri kwani kabla hata Majimaji haijashuka daraja aliwahi kuitafutia timu hiyo udhamini mnono kutoka kwa kapuni ya CASPIAN ambao uliifanya Majimaji ambayo ilikua na akina Said Mohammed, Partick Betwel 'Masai' Six Mwasekaga, Lucio Almasi, Evaristi Maganga na wengineo wengi kumaliza ikiwa katika nafasi ya sita ya msimamo wa ligi kuu kabla ya kushuka daraja kwenye msimu uliofuata kwa sababu za kiutawala.
Msimu wa mwaka jana wa 2013-2014 klabu ilianza kwa kusua sua sana na mpaka mzunguko wa kwanza unakamilika ilikua inashika nafasi za chini kabisa ikiwa na alama 5 tu lakini mara baada ya Dr Nchimbi kuitafutia udhamini wa nguvu kotoka kwa kampuni ya SIMBION Majimaji ilifanikiwa kuwatwaa kwa mkopo Marcel Boniventure na Frank Sekule kutoka klabu ya Simba ya jijini Dar es salaam na kufanikiwa kumsajili Fred Mbuna aliyekuwa huru kwa wakati huo na kuifanya ti u imalize katika nafasi tatu za juu.
Kwa sasa klabu ya Majimaji haina shida za kupitiliza kwani inafanikiwa kufika kituoni kwa wakati lakini wachezaji wake wanalipwa posho ya safari siku moja kabla ya safari jamboa ambalo kwa vilabu vingi limeibuka kuwa tatizosugu. Wachezaji wa klabu ya majimaji wancheza wakiwa hawana madai yoyote yale na hivyo kuwa katika hali nzuri ya kupambana kuutafuta ushindi mahala popote wanapocheza.
Jambo la pili ni kuzikwa kwa tofauti zilizokua zikiendelea baina ya mashabiki wa vilabu viwili vya mjini hapa vya Majimaji Fc na Mlale Jkt na kuja na kaulimbiu ya RUVUMA KWANZA ambayo imewafanya wana Ruvuma kuzipa sapoti ya nguvu timu timu zao na hivyo kuamsha morali zaidi kwa wachezaji na viongozi.
Lakini pia uwepo wa mkurugenzi wa ufundi Stewart Hall ndani ya timu ya Majimaji kumesaidia timu kuimarika zaidi kwani hakuna mwanakandanda wa nchi hii asiyemjua Hall na uwezo wake wa kufundisha soka tangu alipokua kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar na wana lambalamba Azam Fc.
Wanaoituhumu Majimaji na Uzalendo wanatakiwa kujiuliza maswli kadhaa kabla ya kuzitoa au kuzikubali tuhuma hizo kwani endapo tuhuma hizo ni kweli basi je klabu ya Majimaji inapata matokeo gani inapokua njea ya Songea?
Majimaji ni moja kati ya timu iliyoambulia sare pale uwanja wa Samora mjini Iringa ikicheza dhidi ya Lipuli kabla ya kusafiri kwenda jijini Dar ambako ilipata ushindi wa jumal ya magoli 2:0 dhidi ya Polisi Dar na kurejea mjini Mafinga na kulazimishwa sare na wenyeji timu ya Kurugenzi ya Mafinga kwenye mchezo ambao takribani mabomu 15 ya machozi yalipigwa kuzuia ghasia zilizokuwa zikiendelea kwenye uwanja wa Wambi-Mafinga.
Kwenye mchezo huo wa Mafinga kadhalika mlindamlango wa klabu klabu ya Majimaji Oddo Nombo akijeruhiwa kwa kurushiwa mawe na mashabiki wa klabu ya Kurugenzi hali ambayo ilitaji nguvu ya ziada ya Polisi kuhakikisha kuwa usalama kwa viongozi, wachezaji na washabiki wa klabu ya Majimaji ambao walikua wameambatana na Meya wa mji wa Songea bwana Charles Mhagama na mwenyekiti wa chama cha soka cha mkoa wa Ruvuma bwana Golden Sanga maarufu kama Sanga One.
Kimsingi mafanikio ya klabu ya Majimaji yanatokana na mshikamano uliopo baina ya wananchi wote wa Ruvuma kwani kabla ya kuanza kwa ligi inayoendelea wapenzi, wanachama na mashabiki wa vilabu vya Majimaji na Mlale Jkt waliketi kwa pamoja na kuamua kwa umoja wana wanatakiwa kuweka dhamira ya kweli kupambana kwa hali na mali kuhakikisha kuwa wanaileta ligi kuu mkoani RUVUMA na hakuna njia mbadala ya kuileta ligi kuu isipokuwa kuhakikisha kuwa moja kati ya timu itakayoonesha muelekeo inasapotiwa ili ipande daraja na hivyo kuzisapoti nje na ndani ya mkoa.
Jambojingine ni mshikamano na umakini wa viongozi katika kufanya usajili kwani wao ndio waliowaleta wachezaji wa kiwango cha juu kama Samir aliyekuwa Ashanti United, Kudra Omary, Marcel Boniventure, Frank Sekule, Ditram Nchimbi, George Mketo, Sadick Gawaza, Alex Zegega 'kondo' Fred Mbuna na wengineo ambao ukiangalia karibu wote wanatokea Dar es salaam ambako waliona kuwa ganda la muwa la jana na Majimaji akajifanya Chungu ha kuamua kuwavuna na hatimaye kugeuka kuwa mwiba mchungu kwa wapinzani wao katika ligi.
Uwepo wa benchi la Ufundi zuri na lenye utulivu linaloongozwa na mkufunzi HASSAN BANYAHI akiwa samabamba na mchezaji wa zamani wa Ushirika ya Moshi na klabu ya Majimaji John Kabisama aka Mnyasa na Godfrey Ambrosse Mvura almaarufu Papaa Mvura.
Juu ya yote ni juhudi binafsi za Mbunge wa jimbo la Songea mjini mheshimiwa EMANUEL JOHN NCHIMBI za kuhakikisaha kuwa timu inapata udhamini wa uhakika maana bila ya udhamini huo sidhani kama klabu ya Majiimaji ingeweza kumlipa Mkurugenzi wake wa Ufundi Muingereza Stewart John Hall posho hata ya siku moja tu.
Kwakuwakumbusha tu labda niwakumbushe jambo moja ndugu wangu kuwa bila ya utafiti unakosa haki ya kuzungumza hivyo niwasihi ndugu zangu wa Sports Extra ya Clouds Fm kuja Songea kufanya utafiti ili mjiridhishe na tuhuma mnazozipokea na wakati mwingine kuzitangaza kadhalika ninyi binafsi sasa mpate haki ya kuyazungumzia masuala haya kwa ujumla wake.
"Ngosi sikelela Majimaji, Ngosi sikelela Ruvuma".
ADIOS AMIGO.
hossamulaua@gmail.com.
0713281932/0755231571
Post a Comment