Na Oswald Ngonyani.
Pengine siwezi kuongopa kama
nitaeleza kuhusu maisha ya Ronaldinho katika enzi zile akiwa na ubora wa hali
ya juu zaidi na kuzikonga nyoyo za wapenda soka wengi duniani kote, ni kama
kusema kilikuwa kipindi cha Ufalme wake, Kipindi cha Mfalme Ronaldinho.
Uwezo wake wa kuufanyia chochote
mpira uliwakuna wengi na hata kuzidi kukumbukwa mpaka leo hii katika nyakati za
akina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, ama kwa hakika miaka ile ya 2000 na
ushee ilipendezeshwa sana na Mbrazili huyu.
Ronaldinho ni nani?
RONALDINHO Gaucho ni mwanasoka nyota wa Kibrazil
ambaye amekuwa akicheza soka kama kiungo mshambuliaji na ni mtundu sana wa
kuchezea mpira na anawavutia mashabiki wengi awapo uwanjani.
Jina lake halisi ni Ronaldo de Assis Moreira
aliamua kuitwa Ronaldinho kwa kufuata matamshi ya lugha ya Kireno na
kujitofautisha na akina Ronaldo wengine ambao ni wengi huko Brazil, kama
walivyo akina Mapunda, Tembo, Komba huko
Songea ama akina Mwandosya, Mwambulukutu, Mwakasege wa Mbeya.
Gaucho ni jina lake la kimichezo ambalo
linamtofautisha zaidi na wanasoka wengineo kama akina Rivaldo, Ronaldo, na wengineo wengi. Ni miongoni mwa wanasoka
wachache waliowahi kuiteka dunia nyakati hizo ambao wanaendelea kuhusudiwa
mpaka sasa.
Kutokana na umahiri wake wa hali ya juu wa kuuchezea
mpira katika sehemu ya kiungo na kushambulia amefunga magoli mengi katika klabu
alizochezea lakini pia katika timu yake ya taifa, Brazili.
Aliwahi kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia
mara mbili mfululizo yaani katika miaka ya 2004 na 2005. Alipata mafanikio
makubwa zaidi katika uchezaji soka alipokuwa katika timu ya FC Barcelona ya
Uhispania lakini hata baada ya kuhamia katika kikosi cha AC Milan cha nchini
Italia bado aliendelea kuwa moto wa kuotea mbali.
Aliwahi kuvichezea vilabu gani?
Achana na klabu ya Flamengo ya nchini Brazili,
Ronaldinho amewahi kuvichezea pia vilabu kama FC Barcelona ya Hispania lakini
pia AC Milan ya Italia na kuweza kuzifanyia mambo makubwa timu hizo.
Lakini katika miaka ya hivi hakuna atakayenipinga
kama nitatamka wazi kuwa mtalamu huyu wa chenga amepungua kiwango, pengine hali
hii imesababishwa na kuongezeka uzito, lakini pia kutokana na starehe nyingi
anazozifanya baada ya kuwa na fedha za kutosha.
Je, ni
kweli ana fedha za kutosha?
Ronaldinho ni mmoja kati ya wanasoka matajiri
duniani ambaye amepata utajiri huo kupitia uwezo wake wa usakataji wa kandanda
kwenye klabu kubwa duniani na hata kuingia katika mikataba minono na makampuni
makubwa yaliyokuwa yakimlipa kwa matangazo.
Amekuwa akipata kiasi cha dola milioni 24 kwa
mwaka. Anaelezwa kuwa alikuwa akipata kiasi cha Euro milioni 25 kwa mkataba
wake wa miaka mitatu katika timu ya AC Milan ya Italia. Lakini pia inasemekana
kuwa alikuwa akilipwa kiasi cha dola milioni 10 kwa mwaka kutokana na mshahara
wake wakati alipokuwa Barcelona.
Ametengeza fedha nyingi zaidi hasa kwa kuonekana
katika matangazo mbalimbali ya kampuni za Pepsi na Nike na hata kuweza kuwazidi
baadhi ya nyota wengine wa dunia. Anaaminika kuwa na utajiri wa zaidi ya dola
milioni 90.
Vipi
kuhusu mipangilio yake ya kifedha?
Kama walivyo watu wengine wengi walio na fedha, Ronaldinho
naye hayupo nyuma katika hili, ni mahiri katika matumizi ya pesa hususan katika
kuishi maisha ya kifahari kutokana na faida aliyoipata baada ya kukitendea haki
kipaji chake ndani ya dimba.
Anamiliki nyumba kadhaa nchini kwao Brazil lakini
pia barani Ulaya katika nchi ya Hispania. Anamiliki na kuendesha magari ya bei
mbaya ya kifahari miongoni mwake ni Mercedes-Benz Eclass na Mercedes-Benz CLS.
Pia anamiliki gari la bei ya juu zaidi aina ya
Bugatti Veyron ambalo linasifika kwa kuwa na kasi. Gari hilo la mashindano
limekuwa likiteka nyoyo za watu wengi akiwemo Ronaldinho mwenyewe.Lina mvumo
kama wa nyuki likiwa na uwezo wa kusafiri kwa kasi ya kilometa 253 kwa saa na
injini ya W16, alilinunua gari hilo kwa dola milioni 1.8.
Anapokuwa nyumbani hupenda sana kuliendesha gari
hilo ambalo nalo lina kazi kubwa ambalo hulitumia wakati wa kwenda mazoezini.
Ana Hummer H2, ambayo ni imara na yenye
nguvu. Ni gari ya ajabu wakati inapoendeshwa ambayo humvutia kila mtu. Unaweza
kusema kuwa haliendani na hadhi yake lakini ndiyo hivyo amelipenda. Ni moja
kati ya magari yanayopendwa na mastaa wa majuu mmoja wapo akiwa ni mcheza
sinema za kibabe Arnold Alois Schwarzenegger.
Si mtu anayependa kujinyima kama wafanyavyo
wengine amekuwa mfuasi mzuri wa anasa kama walivyo akina Ronaldo wa Brazili
lakini pia akina Ronaldo wa Ureno. Mara zote anaposafiri safari ya mbali lakini
pia hata safari ya karibu amekuwa akisafiri kwa kutumia ndege ya kukodi na hata
kulipa kiasi kikubwa cha pesa.
Ameifanyia
nini Jamii?
Achana na habari za Desemba 8 mwaka
jana (2013) zilizowahi kutikisa anga la Tanzania kuhusu Mwanasoka huyo mahiri
kutoa msaada wa fedha zitakazo tumika kwa
ajili ya ujenzi wa hospitali katika
mkoa wa Singida.
Kutokana
na kufahamika zaidi kwa watu wengi na hata kulifanya jina lake kuwa kubwa,
Ronaldinho amekuwa mwenye ushawishi mkubwa katika jamii na hata kuweza kumiliki
mfuko wa hisani kwa ajili ya kusaidia watu wengine. Wakati fulani aliwahi kugombana
na kaka yake kwa kutumia fedha vibaya.
Ametokea
katika familia ya namna gani?
Ronaldinho alizaliwa kutoka katika familia ya
tabaka la kati nchini Brazil. Baba yake alikuwa akifanya kazi getini na
alipatwa na mkosi wa kufiwa na baba yake wakati akiwa mdogo wa umri wa miaka
nane.
Katika familia yao amezaliwa pamoja na kaka yake
na dada yake. Amekuwa na mahusiano na wanawake wengi na anajulikana zaidi kwa
kuwa na mahusiano na mwanamke wa Kifaransa wakati alipokuwa Barcelona.
Ana mtoto wa kiume aliyepata kutokana na kuwa na
mahusiano ya kimapenzi na dansa mmoja wa Kibrazil, Janaina Mendes. Ili kujenga
kumbukumbu isiyofutika, aliamua kumpatia mwanaye jina la marehemu baba yake.
Kwa sasa anadaiwa kuoa, awali aliwahi kuoana na Milene Domingues lakini baada
ya muda mfupi walipeana talaka.
Kuna mengi sana ya kuandika kuhusu mtalamu huyu
wa mchezo wa soka, lakini kwa leo acha tu niishie hapa. Ni imani yangu
mmeburudika vya kutosha kupitia aya za makala haya.
(Mwandishi
ni Mchambuzi wa Makala za Kimataifa katika gazeti la Michezo la Dimba, kwa
wenye Maoni au Ushauri wanaweza wakatuma kwenda namba 0767 57 32 87)
Post a Comment