Na Oswald Ngonyani.
Pengine
linaweza likawa ni swali ambalo mashabiki wengi wa mchezo wa soka
wamekwishawahi kujiuliza lakini kwa bahati mbaya wakajikuta wakikosa majibu
stahiki kuhusu ubora wa watu hawa ‘Cristian
Ronald’ na ‘Lionel Messi’.
Majina
haya ‘Cristian Ronaldo na Lionel Messi’ kamwe hayawezi yakawa mageni katika
fikra za mashabiki wengi wa mchezo wa soka duniani hususan katika zama za sasa,
zama ambazo dunia imekuwa kama kijiji.
Kama
ilivyo kwa wakongwe wa mchezo wa soka akina Pele na Maradona, ndivyo ilivyo
sasa kwa vijana hawa wawili kutoka katika nchi na mabara tofauti ambao uwezo
wao katika kuucheza mchezo wa soka upo juu tena juu kuliko
Ni
kama kusema mashabiki wengi wa kandanda wapo njia panda kwa sasa, wameshikwa na
kigugumizi kutokana na kukosa majibu stahiki ya nani ni nani miongoni mwa
wanandinga hawa wawili wanaoonekana kuigawa dunia kama ilivyokuwa enzi zile za
akina Pele na Maradona.
Wapenzi
na wasomaji wengi wa Makala zangu wamekuwa wakiniuliza mara kwa mara swali hili
‘Messi na Ronaldo, nani zaidi?” Katika hili, ni lazima nikiri kuwa kamwe
sikuwahi kuwapa majibu waliyotegemea.
Kwanini
sikuwapa majibu waliyotegemea? Kwa sababu nilijua wazi kuwa kipimo cha uwezo wa
kila mchezaji huendana na takwimu halisia zinazompambanua mchezaji huyo katika
mawanda ya soka ya kimataifa.
Ndiyo
maana ilinipasa kupitia tena na tena katika baadhi ya takwimu zinazowahusu ’majemedari’
hawa ili kuweza kuja na jibu stahiki, ndivyo nilivyoamua kufanya kwa siku ya
leo.
Lionel Messi ni nani?
Jina
halisi la Mwanamume huyu ni Lionel
Andre’s Messi Cuccittini. Alizaliwa miaka 27 iliyopita huko Rosario,Sante Fe –
Argentina. Ni mchezaji tegemeo katika kikosi cha Barcelona ya nchini Hispania, akiwa
ameifanyia makubwa klabu hiyo.
Ndiye
mshindi mara nne wa tuzo ya Mchezaji bora wa FIFA wa Dunia, akitwaa tuzo hiyo
katika miaka ya 2009,2010,2011 na 2012. Ni mchezaji wa kwanza kushinda tuzo
zote hizo katika historia ya mchezo wa soka ulimwenguni kote.
Tazama,
jina lake limeingia katika orodha ya mchezaji aliyefunga magoli mengi ndani ya
mwaka mmoja akiwa amefunga magoli 91 mwaka juzi (2012) ambapo hakuna mchezaji mwingine yeyote aliyewahi
kufikia rekodi hiyo.
Ndiye
mchezaji aliyefunga katika mechi 21
mfululizo akiwa amefunga magoli 33 katika michezo 21 na hivyo kuzidi kuitikisa
dunia katika historia ya mchezo huo unaoongozwa kwa kuwa na idadi kubwa ya
mashabiki.
Muargentina
huyu ndiye mchezaji wa kwanza kuzifunga timu zote katika ligi kubwa akifanya
hivyo katika Ligi kuu nchini Hispania.
Amewahi
kushinda tuzo ya Mfungaji bora wa Ligi kuu ya nchini Hispania maarufu kama La
liga mara 3 yaani katika miaka tofauti tofauti ya 2010, 2012, na baadaye mwaka 2013.
Ndiye
mchezaji wa Kwanza kuwahi kufunga magoli 200 katika Ligi kuu nchini Hispania
akiwa na umri mdogo (Miaka 25), alifanya hivyo mwaka 2012.
Kama
hiyo haitoshi, Lionel Messi amefunga Hat Tricks (Magoli matatu) nyingi zaidi
katika mechi kubwa ya El Clasico (Barcelona vs Real Madrid) ambapo amewahi kufunga
mara mbili.
Vipi
kuhusu Cristian Ronaldo?
Mreno
huyu alizaliwa miaka 29 iliyopita huko Tunchal, Madeira. Kabla ya mwaka 2013
huyu ndiye alikuwa mchezaji ghali kabisa kuwahi kutokea katika Historia ya mchezo
wa kandanda.
Ndiye
Mchezaji wa kwanza kufikisha magoli 40 kwa msimu katika misimu miwili mfululizo.
Ameshinda
mara mbili wa tuzo ya mchezaji bora wa Dunia wa FIFA akiitwaa mwaka 2008 na
mwaka 2013.
Ronaldo
ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi kuu ya Hispania ‘La liga’ mara mbili yaani
katika msimu wa mwaka 2010/2011 na msimu wa 2013/2014, lakini pia amewahi kushinda
tuzo ya Mchezaji bora wa msimu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) mwaka 2013/2014
Ndiye
mchezaji pekee aliyefunga magoli mengi katika msimu mmoja wa ligi ya Mabingwa
Ulaya akifunga magoli 17 katika msimu wa 2013/2014, rekodi hii kamwe hii haijawahi kutokea asilani.
Mshambuliaji
huyu wa klabu tajiri ya Real Madrid ndiye mchezaji pekee katika ligi ya
mabingwa Ulaya aliyefunga magoli katika mechi 8 mfululizo katika msimu wa
2013/2014.
Ndiye
Mchezaji aliyefunga magoli mengi katika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa
barani Ulaya akifunga magoli 9 katika msimu mmoja.
Tazama,
‘fundi’ huyu wa kandanda ndiye mchezaji wa kwanza katika La Liga kufunga magoli
150 katika ligi ikiwa ni kipindi kifupi kabisa kuwahi kutokea kwa mchezaji
binafsi.
Ni kama kusema Cristian
Ronaldo na Lionel Messi ni aina ya watu ambao wamejaliwa uwezo wa kufunga goli
zaidi ya 20 katika kila msimu.
Ni wachezaji ambao wanacheza
katika wakati huu ambao umetawaliwa na mabeki wenye roho mbaya wenye uwezo wa
hali ya juu, lakini bado wangali wakifunga, tena idadi kubwa ya magoli.
Bila shaka katika dunia ya
leo hususan katika hulka ya kuushabikia mchezo wa soka ni wazi kuwa mashabiki
wengi wa soka wamejigawa katika pande mbili zinazokinzana, pande za wachezaji
hawa ambapo kila mmoja anaonekana kuwa bora zaidi kuliko mwingine.
Si nia yangu kuwa hakimu
wa mjadala huu, pengine kwa haya machache niliyoyaandika huenda mchezaji fulani
akaonekana kuwa juu kuliko mwingine.
Pengine kuna rekodi
nyingine nzuri zaidi sijaziandika kuhusu ‘wataalamu’ hawa lakini angalau hiki
kidogo nilichokiandika kinaweza kikawa kimetoa jawabu stahiki.
Hapana shaka wanastahili kuenziwa kutokana na uwezo wao
ndani ya dimba, lakini Je! Nani ni zaidi ya mwingine?
Tamati rasilimali……….
(Maoni ushauri tuma kwenda namba 0767 57 32 87, au kwa
barua pepe kwenda ngonyanioswald@gmail.com).
Post a Comment