Na Oswald Ngonyani.
Huu ni mwendelezo wa makala yangu kuhusu
Mashujaa wa soka waliowahi kuikonga dunia na hata kujenga historia isiyofutika katika
viriba vya ubongo wa mashabiki wengi wa mchezo wa soka duniani kote.
Hapa nilikuwa nawazungumzia akina Edison
Pele wa Brazili na Diego Maradona wa Argentina. Tayari nilikwisha maliza
kumuelezea Pele na ukulu wake katika usakataji wa ‘Gozi la ngo’mbe’, leo hii ni
zamu ya Maradona, Muargentina ambaye Waingereza wamegoma kabisa kumsamehe.
Unadhani kwanini wamegoma kumsamehe?
Ungana nami mstari kwa mstari uweze kujua ukweli kuhusu kisa hiki lakini pia
ukweli kuhusu umaridadi wake katika historia ya mchezo wa soka.
Mwanamume huyu aliwahi kuitingisha dunia katika
miaka ya 1976 mpaka 1997. Alizaliwa miaka 54 iliyopita (30/10/1960) nchini
Argentina katika mji wa Lanus, Buenos-Aires.
Ana urefu wa Mita 1.65 ambaye katika enzi zake za
kusakata kabumbu alikuwa akicheza katika nafasi ya ushambuliaji wa kati.
Katika nyakati fofauti yaani kati ya mwaka 1976
mpaka 1997 aliwahi kuvichezea vilabu vya Argentina Juniors, Boca Juniors,
Barcelona, Napoli, Sevilla, na Newell’s Old Boys, huku akiwa tegemezi katika timu
yake ya Taifa katika miaka ya 1977-1994.
Mchezo wa soka kama unavyojidhihirisha kwa kuwa
na ubora wa hali ya juu na hata kujikusanyia mashabiki wengi kuliko michezo
mingineyo umekuwa ni zaidi ya mchezo wa kawaida.
Hauna tofauti
na sanaa. Kwa baadhi ya watu mchezo wa soka ni imani kama ilivyo imani
nyingine za dini. Kuna watu akili na mawazo yao siku zote yameathirika na soka.
Ndivyo ilivyo kwa wakazi wa Taifa la Argentina,
Taifa ambalo kwayo mchezo wa soka hauna tofauti
na dini au imani. Kwa wenyewe mwanaume huyu ‘Diego Maradona’ ni kama Mungu.
Mambo yote aliyowahi kuyafanya enzi zake za usakataji wa kabumbu na hata sasa
baada ya kustaafu kwao ni mambo yaliyowekwa katika vitabu vya kumbukumbu na
kamwe hawatakuja kuyasahau.
Ni kama kusema kuna wafuasi wengi sana wa dhehebu la Maradona ndani na
nje ya Argentina hususan Amerika. Diego Armando Maradona hana tofauti na nabii
aliyetokea kupendwa sana lakini pia kuchukiwa sana na jamii ya wapenda soka
ulimwenguni kote. Hapa ndipo
anapotofautiana na nguli mwingine wa kandanda, Pele wa Brazil.
Kwa jinsi ilivyo ni wazi kuwa hakuna shabiki wa
soka atakayeweza kunipinga iwapo nitaandika sentensi hii ‘Ni wanasoka wachache
sana katika ulimwengu huu wa kandanda waliotokea kuibua hisia za wapenzi wa
mchezo huo kwa namna ya pekee kama ilivyo kwa Maradona’. Huo ndio ukweli.
Japo sikuzaliwa lakini takwimu za soka
zinanifanya niweke bayana kuwa uwezo wa Maradona na umahiri wake katika
kulisakata ‘Gozi la ng’ombe’ ulionekana wazi zaidi katika mwaka wa 1986 katika
michuano ya Kombe la Dunia na hususan katika pambano la Argentina dhidi ya
Uingereza.
Mpaka leo hii waingereza wamegoma kabisa
kumsamehe Maradona. Pengine wana sababu
nyingi zinazowafanya wamjengee ‘bifu’ la milele
lakini sababu kubwa ni hii Maradona alifunga goli la mkono, lakini
baadaye kidogo Maradona alifunga goli la kiufundi na la utalaamu wa hali ya juu
zaidi pale alipoambaa kwa kasi na mpira akitokea nusu ya uwanja.Unadhani kwanini wamegoma kumsamehe?
Ungana nami mstari kwa mstari uweze kujua ukweli kuhusu kisa hiki lakini pia
ukweli kuhusu umaridadi wake katika historia ya mchezo wa soka.
Jemedari huyu aliwapiga chenga za maudhi karibu
wachezaji wote wa Uingereza waliomkabili. Kisha aliukwamisha mpira kimiani.
Kilikuwa ni kitendo cha aibu kubwa sana kwa
wachezaji wa Uingereza kwao ni kama aliwafedhehesha na hata kuonekana si kitu
mbele ya halaiki ya mashabiki wao waliojitokeza kuangalia mchezo huo nchini
Mexico.
Maradona alidhihirisha umahiri wake katika sanaa
ya kandanda, sanaa inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wafuasi. Itakumbukwa,
kuwa Argentina ilishinda Kombe la Dunia mwaka ule., ni wazi kuwa goli la mkono
lilichagiza kuivusha Argentina katika hatua iliyofuata, mpaka leo waingereza
bado wana kinyongo na nabii huyu wa soka.
Miaka minne baadaye, juhudi binafsi za Maradona
ziliiwezesha nchi yake kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la
Dunia. Huu ni ukulu mwingine wa Maradona, ukulu ambao unamfanya azidi kuheshimika
zaidi katika mawanda ya soka.
Katika
fainali zile mechi kati ya Brazil na Argentina ndiyo iliyokuwa na kivutio cha
pekee. Brazil waliwazidi Argentina katika idara zote, hivyo basi, Argentina na
Maradona hawakupumua kwa muda mrefu. Lakini ajabu iliyoje, kama radi, Diego
Maradona alizinduka na kuishangaza dunia ya wapenda soka wengi duniani
waliokuwa wakifuatilia mchezo ule.
Akiwa
amebanwa katika kila upande huku akikabwa na walinzi wa Brazil, Maradona
alifanikiwa kutoa pasi muhimu katika maisha yake ya yote ya kisoka.Ilikuwa pasi
murua kwa mchezaji mwenzake, Claudio Caniggia ambaye alifunga goli pekee katika
mchezo huo.
Argentina waliingia fainali na kushindwa mbele ya wababe wengine wa soka ‘Ujerumani’. Lakini kwa bahati mbaya Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1994 zilimshuhudia Maradona akiwa katika hatua za kuporomoka kisoka. Nabii huyu wa soka sasa likuwa ameanza kupoteza mvuto.
Alijitahidi kidogo katika mechi za awali, kisha likalipuka bomu lililomharibia kabisa sifa yake ya kuwa juu kisoka na hata kumpa mwanya mpinzani wake, Edson Pele kuonekana bora zaidi kuliko yeye.
Maradona alibainika kutumia vidonge vya kuongeza nguvu aina ya efedrin. Argentina nayo ikapoteza mvuto mbele ya washika dau wengi wa kandanda lakini pia haikufanya cha maana katika hatua za awali za fainali hizo.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Nabii Maradona, nabii wa soka anayezungumzwa zaidi mpaka sasa. Soka kama dini ina wafuasi wengi sana ambao si rahisi kuwahesabu. Siku zote bila mpira uwanjani hakuna soka.
Kama ulivyo mpira wenyewe, una umbo la mviringo, wenye sura nyingi zisizoelezeka na wenye kudunda, basi hata pambano lenyewe la soka laweza kuwa na sura nyingi. Ndiyo maana watu husema Mpira unadunda, hii maana yake ni kwamba katika soka lolote laweza kutokea.
Soka, kandanda, kabumbu, kipute au ndinga. Yote hayo na mengineyo ni majina yenye kuzungumzia aina moja ya mchezo ambao si mchezo mwingine bali ni mpira wa miguu.
Kwangu mchezo huu ni kama mchezo wa maajabu, Tazama, katika mchezo huu mchezaji anaruhusiwa kutumia sehemu nyingine zote za mwili, kichwa, kifua, tumbo, mgongo, kisigino, makalio na hata kidevu, lakini kamwe haruhusiwi kutumia mkono.
Tofauti na michezo mingine kama Wavu, Kikapu, Mpira wa meza na mingineyo mingi ambapo mikono hupewa kipaumbele zaidi katika kila mchezo. Ajabu iliyoje, Ni dhambi kubwa sana katika soka kwa mchezaji wa soka kuucheza mchezo huo kwa kutumia mkono na kibaya zaidi akifanya hivyo kwa kudhamiria, kwa makusudi. Dhambi hiyo haisameheki katika soka, adhabu yake ni kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Mkono ni Ibilisi wa soka.
Ndio maana mpaka leo hii, Waingereza ambao kihistoria ndio waliovumbua mchezo wa soka enzi hizo, kamwe hawatakoma kumlaani Maradona kwa kufunga goli lile la mkono nililolielezea katika aya za mwanzoni.
Kwa Waingereza, Maradona alifunga goli kwa kumtumia Ibilisi wa soka, wana haki ya kumlaumu kwani safari yao nchini Mexico katika mwaka huo (1986) iliishia hapo. Maradona mwenyewe alitoa kauli ambayo ilizidi kuwanyong’onyesha Waingereza alipodai kuwa lilikuwa goli la mkono wa Mungu!
Ninafunga mjadala.
(0767 57 32 87)
Post a Comment