Na Oswald Ngonyani.
Baada ya mechi za wikiendi
iliyopita, Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), imesimama kwa wiki moja sasa
kwa lengo la kupisha mechi ya kimataifa, iliyo katika Kalenda ya Shirikisho la
Kimataifa la soka (FIFA) ambapo timu
yetu ya Taifa (Taifa Stars) itapambana na Benin katika dimba Taifa Jumapili
hii.
Tofauti na Ligi zilizopita, Ligi ya msimu huu imeonekana kuwa na upinzani mkubwa
zaidi na hata kutoa changamoto ya kiushindani kwa vilabu Kurwa na Doto (Yanga na Simba) ambapo katika misimu iliyopita zilijijengea mazoea ya kupokezana
ubingwa.
Katika Ligi ya sasa vilabu vyote
14 vimeonekana kujidhatiti kuhakikisha kuwa vinafanya vema katika mbio hizo za
ubingwa ndio maana hata katika Ligi ya mwaka jana ubingwa ulikwenda Azam na
siyo kwa Simba au Yanga.
Ligi hiyo imesimama ikiwa kila
timu imecheza mechi tatu huku klabu ya Mtibwa Sugar kutoka katika mashamba ya
miwa ya Manungu mkoani Morogoro ikiwa inashikilia usukani wa Ligi baada ya
kushinda michezo yake yote na kujipatia pointi tisa muhimu.
Tangu kuanza kwa Ligi hiyo,
Septemba 20 mwaka huu tayari kumejitokeza matukio kadhaa ya utovu wa nidhamu ambayo kwa kila hali
yanatakiwa kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo ili kulinda ubora wa ligi yetu
kwa sasa.
Nakumbuka Septemba 20 wakati wa
mchezo uliozihusisha timu za Mtibwa Sugar ya Morogoro iliyokuwa mwenyeji wa Dar
Young African ya Dar es Salaam, mashabiki wa Yanga walionesha vitendo vya utovu
wa nidhamu baada ya kumrushia chupa mshambuliaji hatari wa Mtibwa Sugar
Mzanzibar Ame Ally katika mchezo ambao mabingwa hao wa kihistoria wa VPL
walilala kwa goli 2-0.
Kama hiyo haitoshi, jijini Mbeya
klabu ya Coastal Union ilionekana kutokuwa tayari kutumia vyumba vya
kubadilishia nguo vya Uwanja wa Sokoine wakidai kuwa vyumba hivyo vilikuwa na
harufu nzito, katika mchezo wao dhidi ya Mbeya City, Wagosi hao wa kaya
walifungwa goli 1-0.
Hata katika mchezo wa Jumamosi
iliyopita wa Simba na Stand United, Viongozi wa Stand United waligoma kuingia
katika vyumba vya kubadilishia nguo vya uwanja huo wakidai kuwa kulikuwa na
harufu nzito ya dawa kwenye vyumba hivyo.
Hiyo tisa, kumi ni kuhusu matukio
ya vitendo vya ushirikina ambavyo vimeonekana kupewa nafasi kubwa zaidi katika
VPL 2014/2015 huku vilabu vikubwa katika soka la bongo vikionekana kuwa vinara
zaidi ukilinganisha na vilabu vinginevyo.
Ndio maana mpaka sasa tayari
vilabu vya Simba na Coastal Union ya Tanga vimekwishalimwa adhabu ya kulipa
faini ya Shilingi 500,000 kila moja baada ya kinachosemekana “Kumwaga Maji ya
Uchawi” kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji katika uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi wa Septemba 21 ambapo timu
hizo zilitoka sare ya 2-2.
Si mara ya kwanza kwa klabu kubwa
ya Simba kuhusishwa na vitendo hivyo uwanjani kwani hata katika Ligi ya msimu
uliopita 2013/2014, klabu hiyo ilihusishwa pia na matukio ya imani za
kishirikina jijini Arusha.
Hata kwa upande wa Yanga hali ni
hiyo hiyo. Nakumbuka katika mchezo wa Yanga dhidi ya Mtibwa sugar Mjini
Morogoro, mchezaji tegemeo wa klabu hiyo na timu ya Taifa ya Tanzania, Simon
Msuva alijikuta akizivamia ‘gloves’ za mlinda mlango wa Mtibwa sugar Said
Mohamed zilizokuwa pembezoni mwa nyavu za milingoti mitatu ya goli lake.
Sijajua sababu ya Msuva kufanya
vile, lakini kwa tafsiri ya haraka haraka ni wazi kuwa imani yake ilimtuma
kuamini kuwa ‘gloves’ zile zilikuwa zinawazuia wao kufunga, ndio maana alifikia
hatua ya kuzichukua na kuzipeleka kwa mmoja wa Viongozi wa juu wa klabu yake .
Tukio hili lilinifanya niikumbuke
mechi ya marudiano ya VPL ya msimu uliopita 2013/2014 baina ya watani wa jadi Simba na Yanga ambapo
taulo la kujifutia mikono la golikipa wa Simba, Ivo Mapunda lilizua kizaa zaa
pale Taifa baada ya wachezaji fulani wa Yanga kuamini kuwa walikuwa hawafungi
kwa sababu ya uwepo wa taulo hilo langoni.
Ni vitu vinavyoweza kuonekana
vidogo sana lakini kwa kiasi kikubwa vinaweza vikachagiza kudhorotesha ligi
yetu na hata kudharauliwa na mataifa mengine ambayo mchezo wa soka unaonekana
kupewa nafasi kubwa zaidi kwao na hata kuyafanya mataifa hayo yasifike katika
mawanda ya soka ya kimataifa.
Pengine makosa tajwa hapo juu
yanaweza yakawa ya kawaida sana, lakini kama mamlaka husika hazitachukua hatua
kwa watendaji wa makosa hayo, hapana shaka hulka hii itaendelea kujengeka tena
na tena kwa wahusika hao na hata kuwa sehemu ya utamaduni wao katika maisha yao
ya kila siku.
Wito wangu kwa mamlaka husika
kuhakikisha kuwa kadhia hii inafanyiwa kazi na hata kutoa adhabu kubwa zaidi
kwa wahusika ili kuwa fundisho kwa Viongozi na wachezaji wa timu husika
wanaoendekeza ‘madudu’ haya.
Ni upuuzi mkubwa kuamini katika
‘nguvu za giza’ ili kupata ushindi, badala yake Viongozi wa timu husika hawana
budi kufanya maandalizi yenye tija kwani ndiyo haswa uchawi wenyewe unaoweza kuiwezesha
timu fulani kupata mafanikio katika michezo yake na si vinginevyo. Kinyume
na hapo tutaendelea kuwa wasindikizaji milele.
(Mwandishi wa makala
haya ni Mwandishi/Mchambuzi wa Makala za Michezo ya Kimataifa katika Gazeti la Michezo la
Dimba, anapatikana kwa simu namba 0767 57 32 87 au kwa barua pepe
ngonyanioswald@gmail.com)
Post a Comment