Tarehe 26 Juni mwaka huu 2016, familia ya soka duniani kote ilifanya kumbukizi ya pekee ya kukumbuka miaka 13 ya kifo cha mpambanaji Marc Vivian Foe, Kijana aliyefariki ghafla uwanjani akiwa analitumikia Taifa lake la Cameroon nchini Ufaransa.
Jasiri huyu aliyekuwa na umri wa miaka 28 kwa wakati huo alianguka katika zulia la uwanja wa Stade Gerland mjini Lyon nchini Ufaransa na kuzua hali ya sintofahamu miongoni mwa mashabiki wengi wa soka.
Baada ya majaribio ya kumfufua kufeli, aliondolewa uwanjani kwa machela huku matabibu kadha wa kadha wakitumia dakika 45 kujaribu kuyanusuru maisha yake kabla ya kuieleza dunia kuwa jasiri huyo wa soka alikuwa amefariki dunia.
Kijana huyu aliyetokea katika familia masikini kwenye kijiji kimoja cha Nkolo nje ya mji wa Younde, alijikuta akilala usingizi wa milele huku wachezaji wenzake wakiongozwa na nahodha wa kikosi hicho nyakati hizo Rigobert Song wakiandamwa na simanzi.
Ilikuwa ni hali iliyozua ukimya wa muda mrefu katika nafsi za wapenzi wengi wa kandanda ulimwenguni kote. Wakameruni walikuwa wamempoteza mchezaji wao, kipenzi chao Marc Vivien Foe. Alizaliwa tarehe Mosi Mwezi Mei mwaka 1975 huko Younde nchini Cameroon. Alianza soka akiwa na klabu ya daraja la pili ya Union Garoua kabla hajahamia kwenye klabu ya Canon Yaoundé, moja ya timu kubwa nchini Cameroon. Alianza kung`ara tangu alipoitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon mwaka 1993 na kuwafanya mawakala na makocha wa vilabu kadhaa barani Ulaya kuanza kuitafuta saini yake mwaka 1994 kwenye fainali za kombe la dunia nchini Marekani.
Kifo chake kiliishitusha dunia ya wapenda kandanda wengi, kwani ilikuwa ni ghafla mno.
Ilikuwa kwenye michuano ya kombe la mabara mwaka 2003 tena katika hatua ya nusu fainali wakati Cameroon ikicheza na Colombia ambapo kunako dakika ya 72, Foe alidondoka katikati ya dimba na juhudi za kuokoa maisha yake ziligonga mwamba.
Nakumbuka kunako mwendelezo wa mashindano hayo, mshambuliaji Thiery Henry wa Ufaransa alishangilia goli lake kwenye mechi ya pili ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuonyesha vidole juu kama ishara ya kumkumbuka Foe, ambapo kabla ya mchezo huo wachezaji wengi walitokwa na machozi kwa kumpoteza mwenzao.
Hata katika mchezo wa fainali, Baada ya Thiery Henry kufunga, manahodha Marcel Desailly na Rigobert Song waliinua kombe pamoja huku baadhi ya mashabiki wakiinua mabango yaliyosomeka hivi: “Simba huwa hafi, huwa analala tu chini kupumzika.”
Foe alifariki dunia kwa kile kilichodaiwa kuwa ni mshituko wa moyo. Nchini Cameroon Foe alipewa mazishi ya kitaifa na heshima zote, ambapo Serikali ilisimamia gharama zote za mazishi.
Thiery Henry alijikuta akishindwa kujizuia kumwaga chozi kwenye mchezo wa fainali. |
Ni miaka kumi na mitatu sasa tangu Foe aanze safari ambayo kila aendaye huwa harudi. Imeendelea kuwa simanzi isiyofutika katika nyoyo za wapenda soka wengi asilani.
Marc Vivien Foe shujaa aliyewahi kupewa tuzo ya kamanda wa taifa la Cameroon, alifia vitani, alifariki dunia akiwa anaipigania nchi yake huku mashuhuda wa kifo chake hicho wakibaki midomo wazi.
Alilifia Taifa lake akiwa anapambana uwanjani. Alikata kauli akiwa anaitumikia Timu yake ya Taifa kwa dhati ya moyo wake lakini wala hakufikia hatma aliyokuwa anaitegemea, Mwenyezi Mungu aliamua kumchukua.
Ingawa ni kipindi kirefu kidogo tangu nchi ya Cameroon na Afrika ikumbwe na gadhabiko hili la nafsi, Taifa hilo bado halijakuwa katika kiwango kile ambacho kilikuwepo katika enzi na nyakati za Foe.
Fainali za mwaka juzi (2014) zilizofanyika nchini Brazili ni ushahidi tosha wa namna ambavyo Taifa hili limekuwa la kawaida mno katika mawanda ya usakataji wa Gozi la ng’ombe tofauti na miaka ile ya 2000’s.
Leo hii dunia ya wapenda soka inapomkumbuka mpambanaji huyu ni lazima itataka kujua mustakabali wa mchezo wa soka nchini humo kwa sasa, kitu ambacho ni wazi kuwa kitawafanya wasimanzike nyoyo zao kutokana na ubora wa Taifa hilo katika soka kuzidi kuwa chini.
“A Lion Never Die, He Just Lays There Sleeping” Ama kwa hakika Simba huwa hafi, analala tu chini kupumzika. Pumzika kwa amani Marc Vivien Foe, wewe mbele yetu sisi nyuma yako! Tutazidi kukuenzi sasa na hata siku zijazo….! Amina.
Maoni/Ushauri tuma kwenda (0767 57 32 87) au ngonyanioswald@gmail.com
Post a Comment