0

Kelvin Haule (mwenye jezi namba sita) akiwa na kikosi cha Tukuyu Stars.

Na Oswald Ngonyani

Fumbua macho Kaka, fumbua macho rafiki, fumbua macho Kelvin. Kwanini mapema hivi?

Majira ya Saa Moja za asubuhi leo hii, nikiwa ndio kwanza najiandaa kwenda Ofisini, mara simu yangu ya mkononi inaita. Pasipo kuangalia jina la mpigaji naipokea na kuanza kuzungumza.

“Oswald, Kuna Taarifa kuhusu Kifo cha Kelvin Haule kilichotokea asubuhi hii katika Hospitali ya Mkoa (Ruvuma), ikiwezekana andika kitu kuhusu marehemu kiende mtandaoni leo leo”

Ndivyo sauti ya mpigaji wa simu ilivyozungumza, sauti ya Mchambuzi wa Michezo wa Kituo pendwa cha Redio Mjini Songea cha Jogoo fm (93.0) Rafiki yangu na Kaka yangu Hossam Ulaya ambaye pia ni Mkurugenzi wa Hossamulaya.blogspot.com.
Kelvin Haule akiwa na Idrisa Juma Shaabani mtoto wa mlinzi wa zamani wa klabu ya Yanga kwenye bonanza la maveterani jijini Mbeya-2012 wote wakiwa wachezaji wa Songea Veterans.

Ni Taarifa iliyotia ukakasi ndani ya moyo wangu. Ni Taarifa iliyonifanya nihoji mara mbili mbili kuhusu tatizo lililomuondoa Kelvin Haule juu ya uso huu wa dunia tunayoishi. “Maralia” ndilo jibu nililopewa.


Akizungumza kwa njia ya simu Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya TFF Bw.James Mhagama ambaye pia ni rafiki wa karibu wa marehemu alieleza kuwa Marehemu Kelvin Haule alikwishawahi kulazwa kabla Hospitalini hapo lakini aliruhusiwa.

Bwana Mhagama ambaye aliwahi pia kucheza mpira na marehemu alizidi kueleza kuwa Alfajiri ya leo (Alhamisi) hali ya Marehemu (Kelvin) ilibadilika ghafla na hivyo kukimbizwa haraka Hospitali ambapo juhudi za Matabibu wa Hospitalini hapo ziligonga mwamba kwani muda mchache baadaye alifariki dunia.
Kelvin Haule akiwa na mmoja ya mdau wa mpira wa jijini Mbeya aliyeomba kupata naye picha ya kumbukumbu wakati bonazna likiendelea.

Hivi ndivyo nafsi ya Shujaa wa soka katika ardhi ya Mkoa wa Ruvuma ilivyoachana na dunia. Mzalendo wa kweli aliyeipigania Majimaji FC kwa jasho na damu.

Ni taarifa ya majonzi iliyonifanya niikumbuke ile Taarifa ya Januari 31, mwaka 2013 iliyomhusu shujaa mwingine mkongwe zaidi wa Majimaji marehemu Ahmed Dizumba. Pengine Dizumba alitangulia ili akawaandalie wengine makao, na safari hii imekuwa zamu ya Kelvin. Inasikitisha sana.

Ni rasmi sasa, Kelvin ameianza safari ya milele, safari ambayo kila aendaye huwa harudi. Kelvin ameondoka akiwa bado anahitajika sana katika maendeleo ya mchezo wa soka mkoani Ruvuma na Tanzania kwa ujumla.

Ameondoka na busara zake, ameondoka na weledi wake, ameondoka na kila kitu kilichokuwa dira katika ustahimilivu wa kandanda ya ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma.
Kelvin Haule akiwa kwenye benchi na Patrick Betwel (Masai), Lenzian Mpangwa, Goddy Mvula,Johackim Komba,Ramadhani Ronaldo na Hossam Ulaya anayeongea na simu wakifuatilia mchezo kwenye bonanza la maveterani jijini Mbeya.
Waungwana wana msemo wao wa Kiswahili unaosema, ulipo moyo wako, yalipo matendo yako, Ishi na moyo wako, hakuna jema kwenye nafsi lishindalo upendo wa moyoni.

Kwa jinsi ninavyomfahamu Kelvin, daima aliishi katika wema, wema ambao ulimfanya ahusudiwe kwa mazuri zaidi kwa jamii ya ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma, ulipokuwepo moyo wake ndipo yalipokuwepo matendo yake.

Ilipokuwepo nafsi yake, ndipo ilipotawala kweli ya mwenendo wake, kweli ambayo ilikuwa inamaanishwa zaidi na yale yaliyotoka kinywani mwake. Pengine wana Ruvuma tulishindwa kuipa fasili mapema Kauli hii ya Kiswahili ‘Kizuri hakidumu”

Amekata kauli katika wakati ambao alikuwa anahitajika zaidi. Ubobevu wake katika tasnia ya Michezo, hususan mchezo wa kandanda ni kitu ambacho kimetuweka wengi katika babaiko. Nenda kapumzike Kelvin, sisi tupo nyuma tunakufuata.
Kelvin Haule akiwa na Ramadhani Boimanda aka Mjomba Boi.
Mbona mapema hivi, kulikoni? Pengine swali hili linaweza likatia makazi katika fikra za wengi, lakini siku zote kila kinachoamriwa na Mwenyezi Mungu, hakuna Binaadamu mwenye uwezo wa kukizuia.

Inawezekana wanaRuvuma walimpenda na kumhitaji sana Kelvin hasa katika nyakati hizi za mwanzo mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL 2016/2017) lakini huwezi jua hesabu za Karima zimelenga nini mbinguni.

Ushauri wake, Busara zake, Hekima yake lakini pia uadilifu wake wa Kiuongozi tutavienzi daima.

Kelvin Haule ni nani katika Soka?

Kwa mujibu wa maelezo niliyopewa na James Mhagama, Kelvin Haule ni miongoni mwa wachezaji wa soka majalali nchini Tanzania. Wachezaji wa kiwango cha juu ambapo Tanzania itaendelea kuwakumbuka daima dumu.


Pamoja na kuwa na jina kubwa katika ardhi ya ndani ya Mkoa wa Ruvuma hususan katika klabu ya Majimaji, lakini safari ya Kelvin katika soka ilianzia mbali sana.

Unazikumbuka timu za Meko FC na Tukuyu Stars za Jijini Mbeya? Kwa misimu tofauti, Marehemu aliwahi kuzitumikia timu hizo kwa mafanikio makubwa.

Utumishi wake uliotukuka katika timu hizo ndio uliopelekea  jina lake kuwa kubwa na hata kuota mizizi ya umaarufu na baadaye kujikuta akijumuishwa katika orodha ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania miaka ile ya 80.

Unaikumbuka Tukuyu Stars ya mwaka 1986? Wanyakyusa hawa walipanda  daraja mwaka 1986 na kwenda moja kwa moja kuchukua ubingwa wa Tanzania bara wakiziacha Simba na Yanga zikitahayari.

Majina kama ya akina Mbwana Makatta, Ally Kimwaga, Michael Kidulu, Godwin Aswile, Selemani Mathew, Aston Pardon, Justine Mtekele, Karabi Mrisho, Richard Lumumba, na Peter Mwakibibi ni miongoni mwa majina ya wachezaji ambao marehemu Kelvin Haule alishirikiana nao vema uwanjani mwaka 1986 na hata kufanikiwa kuipa ubingwa Tukuyu Stars.

Mbali na kuzitumikia timu za Tukuyu Stars na Meko FC za Mbeya, aliwahi kuwika pia na klabu ya Mazao FC ya Mjini Iringa.

Umaridadi wake ndani ya Majimaji FC-Songea.

Huwezi kuizungumzia Historia ya Vilabu vya soka nchini Tanzania pasipo kuzingumzia klabu ya Majimaji maarufu kwa jina la “Wanalizombe” ya Mkoani Ruvuma.


Kuanzia mwaka 1980 mpaka mwaka 2000 mwenendo wa Klabu ya Majimaji ulikuwa hauelezeki. Kiwango cha wachezaji wake kiliwakosha watanzania wengi na hata kujikuta wakihamasika kuwa wafuasi wa kudumu wa Majimaji.

Maji Maji ambayo ilizaliwa rasmi mwaka 1977 kwa muunganiko wa timu mbali mbali mjini Songea chini ya Mwasisi wa timu hiyo Dk Lawrence Mtazama Gama ilianza kupata umaarufu mkubwa mwaka 1980 mwaka ambao timu hiyo ilipata nafasi ya kushiriki kwa mara ya kwanza ligi Daraja la kwanza hapa nchini.

Uwezo wa Maji Maji ulipanda ghafla ambapo mwaka 1996 ikachukua nafasi ya 4 katika Ligi, mwaka1997 nafasi ya 3 na mwaka 1998 Majimaji ilichukua ubingwa wa Muungano kwa mara ya  tatu chini ya wachezaji Bora kabisa hapa nchini.


Shaib Kambanga, David Mjanja, Omari Kapilima,Godfrey Kikumbizi,James Mhagama,Steven Mapunda, John Alex, Doyi Moke, Dello Ntumba,Omari Hussein,Wille Martin,Said Msham,Samson Poul, Hamis Ngwena, Amri Said pasipo kumsahau marehemu Kelvin Haule, ninayemzungumzia hapa.
    
Kilikuwa ni kikosi bora na cha mwisho cha ushindi kwa Timu ya Majimaji, kikosi kilichokuwa kimesheheni wachezaji waliotengeneza ‘kombinesheni’ adhimu kabisa katika soka la bongo, Kelvin akiwepo.

Mpaka leo hii imeendelea kubaki historia. Kilikuwa ni kikosi cha Mauaji kilichowapa jeuri wanaRuvuma wengi ambao Vilabu vya Simba na Yanga vilisubiri sana.

“A Lion Never Die, He Just Lays There Sleeping”   Ama kwa hakika Simba huwa hafi, analala tu chini kupumzika. Fumbua macho Kelvin Haule, angalau uinuke uwape neno la mwisho wana Ruvuma….!

 (0767 57 32 87)

Post a Comment

 
Top