Usajili wa Paul Pogba umevunja rekodi za sajili tano
zilizowahi kuwa ghali zaidi duniani baada ya kutua United kwa paundi
milioni 89.
Manchester United imethibitisha kukamilisha uhamisho wa kiungo wa
Juventus Paul Pogba ambaye amejiunga na mashetani wekundu kwa ada
iliyoweka rekodi ya dunia, kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Manchester
United.
Baada ya uvumi na tetesi za muda mrefu, miamba hiyo ya EPL hatimaye
siku ya Jumapili waliujulisha ulimwengu kwamba, dili la Mfaransa huyo
kurejea Old Trafford linakaribia kukamilika baada ya kuanza kwa
mchakato wa kumfanyia vipimo vya afya.
Alfajiri ya Jumanne, United walitupia chapisho kwenye mtandao wa
twitter kwamba, mchezaji huyo wa zamani wa klabu hiyo amesaini mkataba
wa miaka mitano kuitumikia klabu hiyo wenye kipengele cha kuongeza mwaka
mmoja zaidi.
Uhamisho huo unatajwa kugharimu £89m, ukivunja rekodi ya usajili
ghali zaidi duniani wa £85m uliomshuhudia Gareth Bale akihama kutoka
Tottenham Hotspur na kujiunga na Real Madrid mwaka 2013.
Usajili wa Paul Pogba umevunja rekodi ya sajili tano ghali zaidi
duniani katika miaka ya hivi karibuni ambapo wachezaji wote walihamia
klabu za La Liga, (Hispania), hususani Real Madrid.
Ikumbukwe wachezaji wote hao watano walikuwa wakitoka klabu nyingine
kuhamia Real Madrid, Kwa hiyo tangu mwaka 2000-2013, Real Madrid pekee
ndiyo klabu iliyosajili wachezaji kwa dau kubwa zaidi duniani rekodi
ambayo imevunjwa na Manchester United mwaka 2016.
Mwaka 2000 – Luis Figo £37m (Barcelona kwenda Real Madrid),
mwaka 2001 – Zinedine Zidane £46m (Juventus kwenda Real Madrid), mwaka
2009 – Kaka £56m (AC Milan kwenda Real Madrid), 2009 – Cristiano
Ronaldo £80m (Manchester United kwenda Real Madrid), 2013 – Gareth
Bale £86m (Tottenham Hotspur kwenda Real Madrid)
Chanzo: Goal.com
Post a Comment