0
MAMBO siyo mabaya kwa mshambuliaji Mbwana Samatta, baada ya kuiwezesha klabu yake ya TP Mazembe kubeba ubingwa wa tano wa Klabu Bingwa Afrika.

Ubingwa huo ni wazi umezidi kuweka hai matumaini ya Mtanzania huyo kuachana na timu hiyo msimu ujao na kutimkia Ulaya ambako, ndipo ndoto zake zimeonyesha kuhamia huko kutokana na uzoefu mkubwa alioupata katika misimu minne aliyodumu kwenye klabu hiyo kubwa Afrika.

Samatta anahusika kwa karibu katika ubingwa wa Mazembe kwasababu katika ushindi wa mabao manne waliyoifunga USM Alger yeye peke yake amefunga mabao mawili na kutoa pasi ya bao moja kitu kinacho mfanya kuwa mtu muhimu wa kukumbukwa kwa mashabiki wa TP Mazembe.

Niwazi mpambano wa fainali ulikuwa anaangaliwa na watu mbalimbali wakiwemo makocha wa klabu kubwa barani Ulaya na kwa kipaji alichokionyesha Samatta, bila shaka kitakuwa kimewavutia wataalamu hao na watakuwa tayari kuipata saini ya Mtanzania huyo.

Hilo lilikuwa taji lake la kwanza kubwa tangu alipoanza kucheza soka la ushindani akitokea Mbagala Market baadaye Simba na sasa TP Mazembe kote alipopita alionyesha kuwa atakuwa mchezaji hatari kutokana na kipaji alichokuwa nacho.

Baada ya kushangilia ubingwa huo wa kwanza Samatta amesema medali yake ya ubingwa wa klabu bingwa Afrika anamzawadia Babayake mzazi Mzee Ally Samatta, ambaye ni mtu muhimu kwenye maisha yake huku akihuzunishwa na kifo cha mama yake na kudai anatamani kama angekuwepo ili kushuhudia mafanikio yake.

Licha ya kuibuka mfungaji bora, Samatta amesema alikuwa anatamani zaidi kuchukua ubingwa wa mashindano hayo kuliko kutwaa kiatu cha mfungaji bora.

“Nimemaliza nikiwa mfungaji bora lakini kitu nilichokuwa nakitamani sana ni kutwaa ubingwa, nilikuwa nahamu nao zaidi na hii imekuwa historia kwangu”, amesema Samatta.

“Nai-dedicate medali hii kwa babayangu kwa jinsi ninavyompenda na kumuheshimu kwasababu amenilea mpaka nimefika hapa, nampa huu ushindi, nadhani ingekua vizuri kama mamayangu angekuwepo leo na kushuhudia mafanikio yangu, lakini bahati mbaya ameshafariki siku nyingi kwahiyo nimebakiwa na mzee pekeyake”.

Samatta amechukua tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya vilabu bingwa Afrika baada ya kufunga jumla ya magoli nane na kumpiku mpinzani wake Bakry ‘Al Medina’ Babiker wa Al Merreikh.

Post a Comment

 
Top