0
Kocha wa Kilimanjaro Stars, Abdallah Kibadeni, anaamini kikosi chake kitafanya vizuri kwenye Kombe la Chalenji bila ya Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Kilimanjaro Stars itacheza mechi yake ya kwanza ya Cecafa Chalenji leo Jumapili kwenye Uwanja wa Addis Ababa dhidi ya Somalia.

Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaoichezea klabu ya TP Mazembe ya Jumhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kiungo Mrisho Ngassa wa Free State Stars ya Afrika Kusini, hawapo katika kikosi cha Kilimanjaro Stars na wamerejea katika klabu zao baada ya mchezo wa pili kufuzu Kombe la Dunia 2018 wa Taifa Stars dhidi ya Algeria.

Nyota wengi wa Taifa Stars, ndiyo wanaounda Kilimanjaro Stars na timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes.

“Ni pengo kuwakosa Samatta, Ulimwengu na Ngassa, lakini nitajitahidi kuwatumia waliopo kuhakikisha tunapambana kupata ubingwa.” Alisema  Kibadeni.

Katika moja ya mechi za leo kwenye Uwanja wa Addis Ababa, Kilimanjaro Stars ambayo ipo kundi A itashuka dimbani kumenyana na Somalia huku Kenya ikigonganisha pembe na Uganda "The Cranes".

Hali kadhalika Zanzibar Heroes ilifungwa goli 1-0 na Burundi katika mechi iliyopigwa jana Jumamosi na Wenyeji wa michuano hiyo Ethiopia wakiangukia kipigo cha 1-0 kutoka kwa Rwanda.

Post a Comment

 
Top