Mutasim Jaffer kutoka nchini Sudan amechaguliwa rais
mpya wa Shirikisho la soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati
CECAFA.
Jaffer ataliongoza Shirikisho hilo kwa muda wa miaka minne ijayo na
anachukua nafasi ya Leodegar Tenga kutoka Tanzania ambaye amekuwa katika
wadhifa huo kwa miaka minane iliyopita.
Rais huyo mpya wa CECAFA alipata kura 6 kati ya 10 zilizopigwa huku
mpinzani wake wa karibu Lawrence Mulindwa kutoka Uganda akipata kura
tatu na Vincent Nzamwita akipata kura moja.
Rais wa zamani Tenga amesema ana imani na matumaini makubwa kuwa rais huyo mpya atasaidia kuinua soka katika Ukanda huo.
“Nina furaha kubwa ya kukabidhi madaraka kwa mtu ambaye najua ana
mapenzi makubwa na ya dhati katika mchezo wa soka.Tungependa kuiona
CECAFA ikikua hatua kwa hatua,”.
“ Nina furaha kuwa nimefanya bidii nilivyoweza kwa kipindi chote cha
miaka minane niliyokuwa rais wa CECAFA na nitafanya majukumu yoyote
nitakayopewa katika siku zijazo,” alisema Tenga.
Rais huyo mpya wa CECAFA amesema atatumia uzoefu wake aliopata Sudan kujaribu kuinua soka Afrika Mashariki na Kati.
Aidha, ameonesha kutoridhishwa na mataifa kutoka ukanda wa CECAFA
kutofanya vizuri katika mashindano ya kufuzu kushiriki fainali za kombe
la dunia mwaka 2018 zitakazofanyika Urusi.
Uchaguzi huu umefanyika siku moja kabla ya kuanza kwa mashindano ya soka ya CECAFA mwaka 2015 jijini Addis Ababa.




Post a Comment