RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewapongeza
wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kwa kuisaidia klabu yao ya
TP Mazembe ya DR Congo kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi zote mbili mshambuliaji Mbwana Samatta ameweza kufunga
mabao mawili kati ya manne yaliyofungwa na timu hiyo na kumfanya awe
mfungaji bora wa michuano hiyo.
Malinzi amesema kuwa hayo ni mafanikio makubwa kwa wachezaji
hao na faida kwa Tanzania kwasababu mchango wao umetumika kulitambulisha
soka la Tanzania.
“Nawapongeza sana vijana hawa wawili kwa jitihada zao kubwa na kupata
mafanikio hayo ambayo kwa Tanzania wao ndiyo wakwanza kuyafikia na hii iwe
changamoto kwa wachezaji wengine waweze kucheza kwa malengo ili waweze
kupata mafanikio kama ya Samatta na Ulimwengu,”amesema Malinzi.
Katika salamu zake Malinzi amewataka wachezaji hao kutobweteka kwa
mafanikio hayo badala yake waongeze bidii na kuisaidia timu yao ya taifa
inayokabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Algeria wiki ijayo.
Post a Comment