0
OliverKahn (1) 
Na Oswald Ngonyani.

UPEKEE WA MCHEZO WA SOKA
Mpira wa miguu maarufu zaidi kwa jina la soka au kandanda ni mchezo unaochezwa na jumla ya wachezaji ishirini na wawili katika timu mbili husika, kila timu ikiwa na wachezaji kumi na mmoja.
Lengo hasa la mchezo huu ni wachezaji kuumiliki mpira kwa kutumia miguu na kuuingiza mpira katika wavu wa wapinzani kadiri inavyowezekana, ni mchezo wenye idadi kubwa ya mashabiki kuliko michezo mingine yote inayochezwa katika pande zote za dunia.
Tofauti na michezo mingine yote, katika mchezo huu matumizi ya mikono ni marufuku isipokuwa kwa mlinda mlango tena katika eneo maalumu la ndani ya kiboksi chenye vipimo vya mita 18 lakini pia wakati wa kurudisha mpira baada ya kutoka nje ya uwanja.

NAFASI YA WALINDA MLANGO KATIKA UCHAMBUZI WA MCHEZO WA SOKA
Mara kwa mara wachambuzi wengi wa mchezo wa soka tumekuwa tukiwasahau sana walinda mlango katika makala zetu za uchambuzi tunazoziandika katika magazeti yetu ama mitandao mbalimbali ya kijamii.
Tumekuwa tukiwapa sana kisogo wachezaji hawa ambao pengine ndio wachezaji muhimu zaidi kutokana na majukumu yao makubwa ya kuzuia magoli tangu dakika ya kwanza mpaka kutimilika kwa mchezo husika.

UMARIDADI WA OLIVER KHAN
Kunako nafasi hii ya ulinzi wa goli, kuna mtu anaitwa Oliver Khan. Jina hili si geni hata kidogo kwa mtu aliye mfuasi mzuri wa mchezo wa soka. Mjerumani huyu ana sifa iliyotukuka katika mawanda ya soka la kimataifa na hata kujikuta akiweka alama isiyofutika katika vichwa vya wapenzi wengi wa soka duniani kote.
Mwanamume huyu kwa sasa ni mtu wa kukaa jukwaani na kuuangalia mchezo wa soka na siyo mtu wa kucheza tena kandanda kama ilivyokuwa awali. Hapana shaka nyakati na enzi zake zimekwishataradadi, lakini angali akikumbukwa kwa kile alichokionyesha wakati ule akicheza kama mlinda mlango.

UBABE WAKE LANGONI
Kahn alikuwa ni aina ya wachezaji wasiotaka masihara anapokuwa uwanjani. Nakumbuka aliwahi kuwakoromea wachezaji wenzake na kutaka kuwapiga kwenye michuano ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006 zilizochezwa kwenye ardhi ya kwao Ujerumani na Italia kuibuka bingwa. 

Kitendo cha wachezaji wenzake kucheza ‘show game’ kwa lengo la kutia nakshi ufundi wao wa kuuchezea mpira kilionekana kumuudhi sana golikipa huyu aliyewapasha ‘live’ kuwa wachezaji hao hawakujitoa kwa ajili ya timu ya ya Taifa, walionekana kukosa moyo wa uzalendo.

Sifa yake kubwa ilikuwa ni uwezo wake mkubwa wa kupanga safu yake ya ulinzi wakati timu yake ilipokuwa kwenye hali ya kushambuliwa na timu pinzani. Hakuwa mwoga wa kuwaonya wenzake pale walipokosea alikuwa tayari akosane nao kwa lengo la kuipigania timu yake.

Alikuwa hodari sana kwenye suala la uokoaji wa mipira ya penalti, alikuwa mahiri katika matumizi ya viungo vyake vya mwilini kama vile kichwa, miguu katika namna ambayo haikuweza kuelezeka.

Ilifikia wakati familia ya wapenda soka wengi ulimwenguni ilimbatiza jina la ‘Mikono elfu moja’ kutokana na umaridadi wake  wa kuzuia michomo langoni katika kila upande wa lango alilokuwa analilinda.

Haikuwa rahisi kumfunga magoli ya kizembe. Ilikuwa ni lazima mfungaji atumie mbinu ya ziada zaidi kuliko ilivyo kwa magolikipa wetu wa kizazi cha sasa. Kwa sasa hayo yote yamebaki kuwa historia, ni wazi kuwa ataendelea kukumbukwa na kuheshimika duniani kwa yale aliyoyafanya katika enzi na nyakati zake.

ALIANZAJE KUCHEZA MPIRA?
Alianza kuitumikia timu  ya taifa, Ujerumani mwaka 1994, kwenye ngazi zote za vijana, hadi kustaafu soka mwaka 2006. Moja kati ya mechi ambayo mashabiki wa soka hawawezi kumsahau Khan, ni kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2002.

Mchezo huo ulizikutanisha Brazil na Ujerumani, lakini uliisha kwa Brazil kutwaa kombe kwa kuwafunga Ujerumani mabao 2-0. Mabao hayo, aliyafunga Ronaldo De Lima, baada ya mkongwe Khan kutema mipira iliyokuwa imepigwa na Rivaldo Ferreira.

Kitendo hicho cha kutema mipira miwili iliyosababisha kufungwa kwa Ujerumani, kilimudhi sana mkongwe huyu na kuanza kulia uwanjani hapo baada ya mchezo huo kumalizika.  Ana umri wa miaka 45 kwa sasa na amekwishastaafu soka kitambo.

Makuzi yake ya soka yalianzia kunako klabu ya Karlsruher S.C ya nchini Ujerumani. Mwaka 1994 alijiunga na Klabu ya Bayern Munich na kustaafu soka lake akiwa na klabu hiyo ambayo alikuwa ameitumikia kwa mafanikio na mahaba makubwa.

MATAJI ALIYOSHINDA
Kahn ameweza kushinda mataji mengi kwa timu kiujumla na tuzo nyingine nyingi binafsi. Mwaka 2001, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi, kwenye mchezo wa fainali ya UEFA, dhidi ya Valencia na timu yake, Bayern Munich. 

Haikuishia hapo, msimu wa 2000-2001, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi ya Ujerumani.
Kwenye mwaka 1999, 2001 na mwaka 2002 Khan, alichaguliwa kuwa mlinda mlango bora kwenye ligi zote barani Ulaya.

Katika miaka ya 1994, 1997, 1998, 1999, 2000, 2001 na mwaka 2002, Kahn aliweza kuchaguliwa mlinda mlango bora kwenye ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’.Kwenye kikosi bora cha michuano ya Kombe la Dunia, mwaka 2002, Khan alichaguliwa kuwa mlinda mlango bora na kupewa tuzo iliyozidi kuchagiza ubora wake.

HITIMISHO
 Hapana shaka orodha hiyo ya tuzo na mataji kwa nyanda huyu ni ushahidi tosha kuwa dunia itaendelea kumkumbuka zaidi kutokana na vile alivyokuwa amekitendea haki kipaji chake awapo ndani ya milingoti mitatu.

Kwa sasa mlinda mlango huyo amekuwa hajishughulishi tena na masuala ya soka, japokuwa kwa uchache, bali amekuwa mshauri mzuri wa kocha wa sasa wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Leow.

Pamoja na kujiweka kando na soka bado wachambuzi wengi wa masuala ya soka wangali wakiamini kuwa, ipo siku atarudi kwenye mchezo huu wa soka kama mwalimu kwenye timu yoyote ile ya Taifa ama klabu.

Hapana shaka wakati utatupa majibu stahiki.

(Maoni/Ushauri tuma kwenda namba 0767 57 32 87. Kitabu changu ‘MAGWIJI WA SOKA WALIOWAHI KUITIKISA DUNIA…..’ kipo jikoni kikiendelea kupikwa, Mola akipenda Mwezi Desemba kitakuwa sokoni, NITAWAHABARISHA)

Post a Comment

 
Top