0
Match Preview: Yanga – Mgambo, Wenyeji wanakibarua kizito kurudisha heshima

Klabu ya Yanga kesho Jumamosi itaikaribisha timu ya Mgambo JKT ikiwa ni muendelezo wa Ligi Kuu ya Tanzania bara raundi ya saba mechi hiyo ikifanyika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga chini ya kocha Marcio Maximo inaingia katika mchezo wa kesho ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kipigo cha bao 1-0, ilichokipata wiki iliyopita kutoka kwa wenyeji Kagera Sugar katika uwanja wa Kaitaba.

Kwa upande wa wapinzani wa Yanga Mgambo JKT, itaingia katika mchezo huo ikiwa na imani ya kupata pointi tatu na kuwapita wapinzani wao katika nafasi ya nne waliyopo kwa sasa hasa wakichagizwa na ushindi wa mabao 2-1 walioupata Jumatatu dhidi ya timu ngumu ya Mbeya City.

Yanga inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi hiyo huku Mgambo JKT ikiwa katika nafasi ya sita ikiwa na pointi tisa pointi moja nyuma ya mabingwa hao wa zamani hicho ndicho kitakacho leta ugumu katika pambano hilo ambalo makocha wote Bakari Shime wa Mgambo na Marcio Maximo wanaumiza vichwa kuhakikisha kila mmoja anapata ushindi.

Kikosi cha Yanga tayari kilisha wasili Dar es Salaam tangu Jumatatu kikitokea Bukoba na kuanza maandalizi ya kujiandaa na mchezo wa kesho na Maximo amesema haijui Mgambo lakini atahakikisha wancheza kwa nguvu ili kuhakikisha wanapota pointi tatu zitakazo waweka kwenye nafasi nzuri ya kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa inaongoza ligi.

Maximo amesema pamoja na kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar lakini kikosi chake kipo katika hali nzuri na anatarajia kumtumia winga wake Simon Msuva ambaye hakucheza mechi mbili za Kanda ya Ziwa dhidi ya Stand United na Kagera Sugar kutokana na kuwa majeruhi.

“Tunacheza na Mgambo JKT ni moja ya timu nzuri katika ligi najua mchezo utakuwa mgumu lakini tumejianda kucheza kwa nguvu ili kupata ushindi kwa sababu wachezaji wangu wote wapo fiti isipokuwa Husseni Javu mwenye matatizo ya goti lengo letu ni kumaliza mzunguko wa kwanza tukiwa tunaongoza ligi ,”amesema Maximo.

Bakari Shime kocha wa Mgambo JKT anasema amekuja Dar es Salaam akiwa na matumaini kesho atapata ushindi mbele ya kikosi cha kocha Maximo.
Shime amesema ushindi walioupata katika mechi mbili dhidi ya Ndanda FC na Mbeya City umewapa ari ya kujiamini na kufufa matumaini ya kufanya mambo makubwa msimu huu baada ya kuanza vibaya kwa kufungwa mechi tatu mfululizo.

“Yanga ni timu kubwa hilo hatulipingi lakini tumekuja hapa tukiwa tumejianda kwa chochote kitakachotokea ndani ya dakika 90 na hamasa kubwa tuliyonayo ni kuifunga Yanga katika mechi ya mzunguko wa pili msimu uliopita kwenye uwanja watu wa Mkwakwani Tanga,”amesema Shime.

Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na Mgambo katika mchezo wa raundi ya pili uliofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga na kuondoa matumaini yao ya kutwaa ubingwa.

Post a Comment

 
Top