Kocha wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema Angel Di Maria alikuwa ni mmoja kati ya wachezaji waliokuwa wanaighalimu sana timu hiyo haswa inapokuwa uwanjani kutokana na tabia yake ya kupoteza mipira mara kwa mara na ndio maana haikuwa tabu sana kwake hata mabosi wa klabu yake kuamua kumruhusu aondoke klabuni hapo.
Di Maria aliuzwa kiajabuajabu kwa klabu ya Manchester United kwa ada ya uhamisho wa rekodi ya paundi milioni 59.7 mnamo mwezi August, wakati mashabiki wengi wa Les Blancos na wachambuzi wengi wa masuala ya soka wakiwa hawaliungi mkono suala hilo la kuuzwa kwani alikua ni mmoja kati ya wachezaji muhimu sana kwenye mbio zao za kupambana kuvisaka vikombe mbalimbali kwa msimu uliopita ikiwemo ile ya Champions League na Copa del Rey.
Lakini pia kocha huyo aliongeza kuwa ujio wa James Rodriguez, aliyesajiliwa kwa ada ya Euro milioni 80 kutokea pale klabu ya Monaco mara baada ya kumalizika kwa michuano ya kombe la Dunia kumefanya kutokuwa na mahitaji tena ya kuwa na Di Maria kwani anaonekana kufiti sana katika nafasi aliyokuwa akiitumikia Muajentina huyo.
Ancelotti amesema tabia ya Di Maria kupoteza mpira na aina yake ya uchezaji haswa linapokuja suala la michezo migumu ilikuwa ikiighalimu sana timu hiyo kwani wakati mwingine alikua akipoteza pasi nyakati muhimu.
Post a Comment