AZAM FC inarudi katika uwanja wake wa nyumbani kesho Jumamosi ikiwa
katika wakati mgumu baada ya vipigo viwili mfulululizo dhidi ya JKT Ruvu
na Ndanda FC ambavyo vilichangia kuondoka kwa kocha wake msaidizi Kali
Ongala.
Matokeo hayo bado yanaonekana kuithiri Azam na hasa inapokwenda
kucheza na Wagosi wa Kaya Coastal Union ambayo msimu huu imeonekana
kuimarika zaidi na hata kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi na
kuzipita klabu kongwe na kubwa za Simba,Yanga na Azam.
Kocha Joseph Omog huenda mambo ya kazi kumuwia magumu kesho kutokana
na ugumu wa mchezo huu kwani vipigo hivyo vimeonyesha Azam inamapungufu
makubwa katika safu yake ya ulinzi ambayo imeruhusu nyavu zake kutikiswa
mara nne katika mechi sita za ligi ilizocheza timu hiyo.
Na endapo Azam ikipoteza mchezo huo wa kesho inamaana hata malengo ya
kutetea ubingwa kwa kocha Omog yatakuwa yanazidi kupotea kwasababu hata
Coatal Union inaweza kunyakua ubingwa kutokana na namna ilivyojipanga.
Kocha Omog kesho ataendelea kukitumia kikosi chake kipana akiwemo
mshambuliaji raia wa Haiti Lionel Saint Preux,ambaye alicheza kwenye
mechi ya Ndanda FC, akiingia kipindi cha pili lakini hakuweza kuisaidia
timu hiyo.
Mbali ya safu ya ulinzi ya Azam kuonyesha mapungufu mengi lakini hata
ile ya ushambuliaji imeonekana kupoteza makali ambayo ilianza nayo
msimu huu kwa kufunga mabao matano katika mechi mbili za awali.
Mshambuliaji mpya wa timu hiyo Mrundi Didier Kavumbagu,alifunga mabao
manne katika mechi mbili dhidi ya Polisi Moro na Ruvu Shooting lakini
kwa sasa ameonekana kupotea kabisa kwani hata ushindi wa mwisho
iliyoupata kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya lilifungwa na beki Agrrey
Moris.
Omog ambaye katika mchezo wa kesho atakuwa akipata msaada kutoka kwa
Mkenya Ibrahim Shikanda aliyeteuliwa kuziba nafasi ya Kali Ongala
amesema bado anaimani na kikosi chake na atahakikisha watafanya vizuri
katika mchezo wa kesho na kupata ushindi.
“Vipigo vimevuruga malengo yetu ya kutopoteza mchezo kama ilivyokuwa
msimu uliopita lakini ni hali ya kawaida ambayo inatokea kwa timu yoyote
lakini tumejipanga kuhakikisha kesho tunapata ushindi najua wapinzani
ni timu nzuri lakini nakumbuka msimu uliopita tuliwafunga mabao 4-0
kwenye uwanja huu,”amesema Omog.
Omog amesema ataendelea kukitumia kikosi chake kilekile ambacho
alikitumia kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara kwa sababu anaamini
nido bora kwake pamoja na kwamba walipoteza mchezo.
Katika mchezo wa kesho Azam huenda ikamtumia mshambuliaji wake Kipre
Tchetche ambaye hajaonekana katika mechi mbili zilizopita kutokana na
kurudi kwao Ivory Coast kwa matatizo ya familia .
Kocha wa Coatal Union Mkenya Yusuph Chipo ameapa kuhakikisha wanapata
ushindi kwenye uwanja wa Azam Complex kesho kutokana na uimara wa
kikosi chake msimu huu.
Chipo amesema anafahamu kuwa Azam ni timu kubwa na ndiyo mabingwa
watetezi lakini hilo lipo nje ya uwanja na siyo ndani ya dakika 90.
“Tumekuja kuhakikisha tunalipiza kisasi cha kufungwa mabao 4-0, msimu
uliopita wakati ule tulikuwa na matatizo mengi ambayo yalitokana na
wachezaji lakini Coastal hii ni tofauti na malengo yetu ni kumaliza
mzunguko wa kwanza tukiwa vinara,”amesema Chipo.
Chipo amesema anajivunia kiwango bora cha kipa wake Shabani Kado na
viungo Rama Salim na Lutimba Yayo ambao wamekuwa wakifanya kazi tangu
kuanza kwa msimu huu na kuipa mafanikio timu yake.
Timu hizo zinakutana wakati wageni Coastal Union wakishika nafasi ya
pili nyuma ya Mtibwa Sugar ikiwa nafasi ya pili na pointi 11 na Azam ipo
kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 10 na zote zimecheza mechi sita.
Post a Comment