Meneja wa klabu ya Manchester United Mholanzi Louis van Gaal amethibitisha maumivu ya mlinzi wake wa kati raia wa Argentina Marcos Rojo ambaye amejitonesha maumivu bega lake kwenye mchezo ambao timu yake ilipoteza kwa goli 1-0 dhidi ya Manchester City kwenye dimba la Etihad Stadium.

Rojo alitolewa mapema kipindi cha pili na kuwekewa mtungi wa gesi ya oksijeni mara baada ya kupatwa na maumivu hayo ya bega kwenye mchezo huo.

Muajentina huyo sasa ataungana na majeruhi wengine ndani ya klabu hiyo wakiwemo Rafael na Phil Jones huku Chris Smalling akiwa anatakiwa kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata kwenye mchezo huo dhidi ya  manchester City ikishuhudiwa United ikiangukia pua dhidi ya mahasimu wake hao wa mji mmoja.

"Ameumia bega, limetoka kwenye sehemu yake, hivyo huwezi kujua ni kwa muda gani atakua nje ya uwanja," Van Gaal alikiambia kituo cha televisheni cha Sky Sports cha nchini Uingereza. "Tuanatakiwa kusubiri mpaka kesho lakini kutokana na hali ya mambo ilivyo hataweza kucheza dhidi ya Crystal Palace."