Na Osward Ngonyani.
Mara kwa mara nimekuwa nikiandika sana makala za kimataifa
kuhusu wachezaji fulani ambao kwa kiasi kikubwa huwa wamefanya makubwa katika
mawanda ya soka la kimataifa na hata kuwa gumzo kwa kila aliye mdau wa michezo.
Kwa wiki kadhaa zilizopita nimekuwa nikiwaandika sana akina
Messi na Ronaldo, nadhani kwa mtu anayefuatilia mchezo wa soka kwa sasa ni
lazima ataniunga mkono kutokana na ukweli kuwa wachezaji hao kwa sasa ‘ndiyo
habari ya Mujini’.
Wakati nyakati na enzi zikizidi kwenda kasi, nimejikuta
nikikikumbuka kitu fulani cha muhimu sana ambacho kwayo kilinifanya nijilaumu
kwa kutokukiandika gazetini kwa muda wote wa uandishi wangu.
Ni kweli tangu nianze kazi ya Uandishi nimewahi kuandika
makala nyingi sana kuhusu wachezaji nguli waliowahi kuzikonga nyoyo za mahusuda
wengi wa soka la dunia lakini kamwe sikuwahi kuandika makala kuhusu shujaa
fulani wa Afrika na dunian kwa ujumla, George Weah.
Weah ambaye ni msomi wa Chuo Kikuu cha Devry cha nchini
Amerika kwa siku za karibuni amejikita zaidi katika siasa, alizaliwa miaka 48
iliyopita (Oktoba 1 mwaka 1966) huko Monrovia nchini Liberia.
Mwanandinga huyu ndiye mchezaji wa kwanza kutoka nchi ya
Kiafrika kutunukiwa tuzo ya Mwanasoka Bora wa dunia, yaani tuzo ambayo mpaka
leo hii hakuna mchezaji yeyote wa kiafrika aliyewahi kuipata.
Pamoja na akina Samuel Etoo’, Didier Drogba, Yaya Toure na
hata akina Michael Essien kuvuma sana kwa siku za karibuni lakini wote kwa ujumla
wao wameshindwa kabisa kuifikia rekodi iliyowekwa na mpambanaji huyu.
Nakumbuka ilikuwa mwezi Desemba, mwaka 1995, ambapo FIFA iliitangazia
dunia ya soka kuwa kuwa George Weah amechaguliwa kwa kupigiwa kura kuwa
mwanasoka bora wa dunia.
Ni katika mwaka huo, George Weah akawa Mwanasoka Bora wa
Ulaya, na haikuishia hapo, akatangazwa pia kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika! Ndani
ya mwaka mmoja, akajikusanyia mataji matatu.
Hapana shaka haya ni mafanikio yasiyo na mifano katika
historia ya soka barani Afrika. Weah ni alama ya soka ya Liberia, aliwahi kutoa
misaada kwa timu ya taifa ya Liberia iliyokuwa na hali duni ili iweze kucheza
michuano ya kombe la dunia na kombe la mataifa ya Afrika, hii ilichangia
kumfanya aheshimiwe zaidi na wananchi wa nchini humo.
Nakumbuka mara baada ya kutunukiwa tuzo hiyo George
Weah aliwahi kuibeba timu yake ya Taifa akiwa ndiyo nahodha wa kikosi hicho kwa
gharama zake yeye mwenyewe ambapo aliambatana na kikosi hicho kwa ajili ya
mchezo wa kimataifa dhidi ya Timu ya Taifa ya Tanzania.
Watanzania wengi walikuwa wagumu sana kuamini kuwa yeye
ndiye haswa alikuwa George Weah. Kila alichokuwa akikifanya pale Sheraton hotel
kilionekana kushuhudiwa na watanzania wengi waliokuwa wakimshangaa.
Hata siku ya mechi uwanjani bado macho ya watanzania
wengi yalionekana kumshangaa yeye zaidi kuliko kuufuatilia mchezo ule.
Walionekana kumpapatikia vya kutosha kutokana na heshima yake wakati huo,
heshima ambayo ameendelea kudumu nayo mpaka leo hii kwani hakuna aliyeweza
kumfikia.
Takwimu za maendeleo yake katika makuzi ya soka zinaeleza
wazi kuwa alianza kusakata kabumbu nchini kwake Liberia kabla ya kuhamia katika
klabu ya Monaco ya Ufaransa, na baadae Paris Saint Germain ya nchini Ujerumani.
Baadaye mwaka 1995
akaenda kwenye klabu ya AC Milan na ndipo akafikia kilele cha mafanikio yake
katika mawanda ya soka. Kwenye uwanja wa nyumbani wa San Siro wa timu ya AC Milan,
George Weah alikuwa mfalme aliyependwa sana na wapenzi wa Milan.
Alipewa kila kitu pale Milan, alihusudiwa na kamwe hakubezwa
kutoka na rangi yake. Uwezo wake wa hali ya juu katika mchezo wa soka
uliwafanya hata wabaguzi wa rangi wa kipindi kile kujikuta wakiwa wapole na
hata kuonesha mahaba ya wazi kwa shujaa huyu msomi.
Baadaye, George Weah akaenda kuchezea Chelsea na kisha Manchester City. Pamoja na mafanikio
makubwa katika soka, George Weah hakuwahi kushiriki kucheza fainali za Kombe la
Dunia, nadhani hiki ni kitu ambacho kitaendelea kumuumiza nafsi yake milele.
Baada ya umri wake kumtupa kidogo, aliamua kustaafu soka na
hata kujikita zaidi katika masuala ya kisiasa ya nchini kwake pasipo kusukumwa
na mtu au kikundi chochote cha watu.
Bila shaka alikuwa na shauku kubwa ya kuiona nchi yake
ikiongozwa na mtu makini atakayeweza kuifanya itulie na kuondokana na vita vya
wenyewe kwa wenyewe na hata kucheza kombe la dunia.
Mwaka 2005, kwa dhati ya moyo wake akaamua 'kucheza
kandanda ya majukwaa ya siasa'. Alishiriki uchaguzi mkuu wa Liberia akigombea
nafasi ya Urais wa nchini humo, haikuwa kazi rahisi kama wengi walivyodhani
kwani kunako mchezo huo wa siasa alikutana na mabingwa waliobobea katika kuucheza
mchezo huo.
Si kwa kuonewa, si kwa kufanyiwa hila, mwanamama Ellen
Johnson-Sirleaf alimgaragaza vilivyo mpambanaji huyu maarufu katika mchezo wa
soka na hata kumfanya mwanamama huyo kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika nchi
za bara la Afrika.
Hapana shaka ataendelea kukumbukwa tena na tena kutokana na
kile ambacho alikifanya ndani ya dimba. Ataendelea kuwa Shujaa wa miaka yote wa
bara la Afrika.
Tamati
rasilimali……………………….
(Maoni/Ushauri tuma kwenda
namba 0767 57 32 87. Kitabu changu ‘MAGWIJI WA SOKA WALIOWAHI KUITIKISA DUNIA…..’
kipo jikoni kikiendelea kupikwa, Mola akipenda Mwezi Desemba kitakuwa sokoni,
NITAWAHABARISHA)
Post a Comment