Klabu ya maveterani wa mji wa Songea (Songea Veteran) imeandaa bonanza kubwa la kufunga mwaka linalotarajiwa kufanyika kwenye dimba la Majimaji kuanzia Ijumaa hii.
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa klabu hiyo Godifrey Ambrose Mvula almaarufu Papaa amethibitisha juu ya uwepo wa bonanza hilo litakalo zishirikisha timu zote za maveterani za manispaa ya Songea.
"Ni kweli kuwa tutakuwa na bonanza kubwa la maveterani litakalozihusisha timu tatu za maveterani wa Songea na moja kutoka jijini Dar es salaam ya Mwambao veterani wanaotarajiwa kuwasili mjini hapa siku ya leo alhamisi jioni".
"Lengo la bonanza hilo ni maandalizi kwa timu zote tatu za maveterani za Songea zinazojiandaa kuelekea jijini Mbeya kwenye bonanza kubwa la kufungia mwaka litakalozihushisha timu zote za maveterani za kanda ya nyanda za juu kusini linalodhaminiwa na TBL".
Aidha Mvura alizitaja timu za maveterani za mjini Songea zitakazoshiriki bonanza hilo ni pamoja na wenyeji Songea veterani, Kambarage veterani na Mandera veterani ambapo linatarajiwa kupigwa kwenye dimba la Majimaji.
Huu utakua wasaa mzuri kwa wapenda soka wa mji wa songea na vitongoji vyake kwenda kujionea kwa mara nyingine hazina ya vipaji vya miaka ya nyuma ambavyo hawakupata kuviona au hata kuwa wamevikosa kwa muda mrefu kutokana na wachezaji hao kuamua kuachana kabisa na masuala ya kabumbu kutokana na umri na majukumu mengine ya kibinaadamu.
Post a Comment