Na Oswald Ngonyani.
Bado imeendelea kuwa na
mvuto mkubwa zaidi kuliko Ligi nyingine yoyote duniani. Naizungumzia Ligi Kuu
ya England (EPL) inayoonekana kupendwa katika pembe zote za dunia. Kwa sasa imefikisha
miaka 22 tangu ilipoanza.
Ligi hii yenye idadi kubwa
ya mashabiki ilianzishwa na Chama cha Soka cha England Februari 20, mwaka 1992
kutokana na uamuzi wa klabu kuachana na Ligi ya Soka iliyoasisiwa mwaka 1888.
Kwa kuachana na ligi hiyo
ya zamani na kuanzisha Premier League, klabu hizo ziliingia kwenye mikataba
minono na haki za kuoneshwa kwenye vituo mbalimbali vya televisheni.
Hadi
kufikia miaka ya 2008 na 2009, thamani ya Ligi hiyo ilikuwa Pauni bilioni
mbili. Hii ndiyo ligi ya soka inayotazamwa na watu wengi zaidi duniani kote,huku
ikirushwa kwenye zaidi ya nchi 212 na inakadiriwa
kuwa na zaidi ya watazamaji milioni 643.
Tangu kuanzishwa kwa Ligi hiyo tayari vilabu kadhaa
vya nchini England vimekwishawahi kuchukua ubingwa huo vikiwemo vilabu vya
Manchester United, Arsenal, Chelsea, na Manchester City.
Uwepo wa upinzani mkubwa katika ligi hiyo imewafanya
wapenzi wengi wa soka ulimwenguni kote kuifuatilia sana soka ya nchini humo
huku vilabu husika vikionekana kuwagawa mashabiki katika mawanda ya
ushangiliaji.
Tazama, kila mwaka kumekuwa na hali ya upinzani
mkubwa kwa vilabu fulani vya nchini humo hususan katika mbio za kuwania
ubingwa, mbio ambazo katika msimu uliopita 2013/2014 pamoja na klabu ya Arsenal
kuongoza kwa kipindi kirefu katika hatua za mwanzo, Klabu tajiri ya Manchester
City ilifanikiwa kuutwaa ubingwa huo mbele ya Liverpool waliokuwa wanaongoza
Ligi katika dakika za lala salama.
Tofauti na msimu uliopita ambapo vilabu vya Arsenal
na Liverpool vilionekana kuanza vema Ligi. Msimu huu 2014/2015 vijana wa Jose
Mourinho wameonekana kuwa na adhma ya kutwaa ‘ndoo’ hiyo kutokana na kasi
waliyoanza nayo msimu huu.
Wazee hawa wa darajani mpaka sasa wamekwisha cheza mechi 7 na
kushinda mechi 6 huku wakitoa sare mchezo mmoja ambapo tangu kuanza kwa Ligi
hiyo Wanaume hawa wala hawajawahi kupoteza mchezo.
Mpaka sasa ndio timu kinara wa EPL ikiwa na pointi
19, pointi tano zaidi ya zile za Manchester City, wanaoshika nafasi ya pili
katika msimamo huo. Tayari, rekodi nzuri na yenye kutia matumaini ya Mourinho
kwa timu hiyo imewafanya wanazi na mashabiki wa klabu hiyo kuanza kuuota
ubingwa.
Huenda wakawa wanakosea kuuzungumzia ubingwa wakati huu kwani
kuna zaidi ya michezo 30 mbele yao wanayotakiwa kuicheza yaani michezo 12 ya mzunguko
wa kwanza lakini pia michezo 19 ya mzunguko wa pili, ni wazi kuwa wanapaswa
kuvuta subira.
Pengine uwepo wa wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu kikosini
hapo yaani akina Diego Costa, Cesc Fabregas, Eden Hazard, na wengineo wengi
huenda ikawa sababu ya kupata matokeo chanya katika michezo yake mingi ya EPL
tofauti na msimu uliopita ambapo akina Samwel Etoo’ na Ferdinando Torres
walionekana kuigharimu timu.
Naweza nikawa ninawaudhi mashabiki husika lakini acha tu
niseme, si wakati wake kwa sasa kuanza kujipa uhakika wa kuchukua ubingwa, ligi
bado mbichi sana na ni lazima wachezaji wapambane vya kutosha ili kuweza
kukidhi haja ya uhitaji kwa mashabiki wao.
Kuna timu kama Manchester United ambayo safari hii imeonekana
kuja vizuri tofauti na msimu uliopita, lakini pia vilabu vya Manchester City,
Liverpool, Totenham, na hata Arsenal wala havipo nyuma, chochote kinaweza
kikatokea.
Binafsi naiheshimu sana Chelsea, lakini pia namheshimu sana Mourinho
kwani ni aina ya makocha wachache wanaoweza kuisoma saikolojia ya mpinzani au
wapinzani anaopambana nao. Ni aina ya kocha anayeweza kuibuka mshindi hata
katika mchezo ambao atazidiwa kila kitu, mimi na wewe tu mashahidi.
Rekodi
ya Chelsea katika EPL ipoje? Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1905 tayari
imekwishafanya mambo makubwa katika soka ya ndani na nje ya England. Kwa mara
ya kwanza ilipata mafanikio makubwa mwaka 1955, ambapo ilichukua ubingwa wa ligi, na kushinda mataji
kadhaa katika miaka ya 1960, 1970, 1990 na 2000.
Imefurahia
zaidi mafanikio katika miongo miwili iliyopita,
kwa kushinda mataji makubwa 15 tangu mwaka 1997. Nchini England, Chelsea
imeshinda ubingwa wa ligi mara nne, kombe
la FA mara saba, kombe
la ligi mara nne, pamoja na ngao
za jamii mara nne pia.
Kimataifa
Chelsea imekwishashinda UEFA
Cup Winners' Cups mara mbili, UEFA
Super Cup mara moja, UEFA
Europa League mara moja na UEFA
Champions League mara moja pia.
Ndio
klabu pekee kutoka London kushinda UEFA Champions League, na ni moja kati ya
klabu nne kutoka Uingereza, kuchukua makombe yote makubwa matatu ya Ulaya.
Tangu Julai 2003, Chelsea imekuwa ikimilikiwa na Bilionea wa Kirusi, Roman
Abramovich.
Si
nia yangu kuiombea njaa Chelsea, lakini shauku ya mashabiki wake imekuja mapema
mno kwani ndio kwanza Ligi ipo katika mzunguko wa 7 huku zikiwa zimebaki zaidi
ya mechi 30 ambazo maandalizI yenye tija zaidi yanahitajika ili kuweza
kuendeleza rekodi ya ushindi kwa wapinzani.
Ni mapema mno kuipa ubingwa Chelsea,
tuvute subira kidogo. Hapana shaka wakati utatupa majibu stahiki.
(Maoni/Ushauri tuma kwenda namba 0767 57
32 87, au ngonyanioswald@gmail.com)
Post a Comment