Na Oswald Ngonyani.
Wakati
fulani Mwezi Mei mwaka huu 2014 Baba mzazi wa Sergio Aguero aliweka wazi kuwa
mshambuliaji huyo wa Manchester City anapenda sana kujiunga na klabu ya Barcelona
ya nchini Hispania.
Kupitia
kauli hiyo vyombo mbalimbali vya habari nchini Hispania viliripoti sana suala
hilo kuwa wababe hao wa Katalunya walikuwa wanajiandaa kuweka mezani ofa ya
paundi milioni 31 ili kumpata mtalamu huyo wa soka ambaye alikuwa ameonesha
mahaba ya wazi kwa klabu hiyo.
Hazikuwa
habari za uzushi kama wengi wanavyoweza kudhani, kwa kiasi kikubwa habari hizo
zilikuwa na ukweli ndani yake japo baadaye mambo hayakwenda kama ilivyotegemewa
ambapo Man City wameendelea kupata huduma ya ‘fundi’ huyu wa soka mpaka sasa.
Barcelona walikuwa
tayari kufikia paundi milioni 47 ili kuinasa saini ya Aguero lakini pia
walikuwa wametenga kiasi hicho kama Man
City wangekataa ofa yao ya kwanza, lakini hawakufanikiwa.
Nakumbuka
ilikuwa ni katika siku za awali za Kocha Luis Enrique, Mwalimu wa Barcelona aliyeonekana
kuchizika sana na uwezo wa Muargentina huyu na hata kujikuta akishindwa
kujizuia kuisaka saini yake.
Kwa hali
na mali, kwa nguvu zote lakini pia kwa akili yake yote Enrique alijitahidi
kumnasa mwanaume huyu lakini Mabosi wa Man City walionekana kutokuwa tayari
kumuachia kirahisi.
Unadhani
kwanini walimbakiza pale Etihad? Kiwango chake katika usakataji wa ‘Gozi la
ngo’ombe’ uwanjani ndiyo sababu ya msingi iliyowafanya Mabosi wa Man City
wazidi kumng’ang’ania.
Aguero
mwenye umri wa miaka 25, ana uhusiano mzuri na nyota wa Barcelona, Lionel Messi
kitu kinachomfanya Enrique aamini kuwa
kuwaweka pamoja wachezaji hawa kunaweza kukaisaidia klabu na Argentina kwa
ujumla.
Kwa mujibu
wa nyaraka za Klabu ya Manchester City, Mkataba wa Aguero utamalizika mwaka
2017, lakini klabu yake inaweza kumuuza kwa zaidi ya paundi milioni 36
walizotumia kumsajili mwaka 2011, hicho ndicho kitu cha pekee ambacho klabu ya
Barcelona ingali inakisubirishia.
Pamoja na
kuwa katika kikosi chenye mafundi wengi cha Man City, kwa kipindi kirefu sasa
Aguero amekuwa na msimu mzuri zaidi pale Etihad licha ya kuandamwa na majeruhi
ya mara kwa mara.
Siku zote amekuwa mwiba katika vilabu shiriki vya
Ligi Kuu ya England (EPL) lakini pia katika mashindano mengine makubwa ya
kimataifa.
Unaukumbuka mchezo wa wikiendi iliyopita wa EPL?
Ilikuwa ni mechi iliyompambanua zaidi na
kuudhihirishia ulimwengu kuwa anajua. Pamoja na kucheza na timu ngumu ya Tottenham,
haikuwa shida kwake kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi mnono wa goli 4-1.
Ilikuwa ni zaidi ya hat trick, Mwanamume huyu
alifunga magoli yote manne na kuiwezesha timu yake kufikisha pointi 17, pointi
tano nyuma ya vinara wa Ligi hiyo kwa sasa, Klabu ya Chelsea yenye pointi 22.
Pamoja na Man City kuwa na kikosi chenye mafundi
wengi kama akina Bacary Sagna, Vincent Kompany, Pablo Zabaleta, Frank Lampard,
James Milber, Edin Dzeko, David Silva, Jesus Navas, na wengineo wengi lakini
bado Aguero ameonekana kujipambanua zaidi na hata kukonga nyoyo za wengi.
Ni wazi kuwa magoli ya wikiendi iliyopita katika
dakika za 13, 32, 68, na 75 dhidi ya Tottenham yamezidi kumpa jina mpambanaji huyu na hata
kuzidi kunyatiwa na Mabosi wa timu nyingi barani Ulaya japo hawajajionyesha wazi,
lakini huo ndio ukweli.
Pengine unaweza ukamwona wa kazi gani, lakini
utendaji wake wa kazi awapo uwanjani ni kitu kimojawapo kinachoweza kumvutia
kila mdau wa soka asiyekuwa na majungu. Ndio maana Mwalimu Luis Enrique wa Barcelona bado angali
akiisaka saini yake mpaka sasa.
Je, atafanikiwa kumnasa Aguero? Tayari Aguero
mwenyewe amekwishaonyesha mahaba ya wazi kwa ‘Vijana hao wa Katalunya’,
kilichobaki ni makubaliano ya Mabosi wa timu zote mbili, Ma City na Barcelona
ili kuweza kufikia muafaka.
Si kitu rahisi hivi lakini itabidi busara zaidi
itumike ili kuweza kufanya maamuzi ambayo hayataiathiri Man City. Kwa haraka
haraka siuoni urahisi wa Aguero kwenda Barcelona japo Luis Enrique angali
akimhitaji sana.
Naomba
kuwasilisha….
Post a Comment