Wapenda Michezo wengi wa Mkoa wa Ruvuma
hususan mchezo wa soka wapo babaikoni kwa sasa, babaiko ambalo limesababishwa na
tamko la Bw. Golden Sanga maarufu kama ‘Sanga One’ Mwenyekiti wa Chama cha soka
cha Mkoa wa Ruvuma (FARU).
Ni tamko la wazi
kufuatia Vilabu vya Ligi kuu ya Vodacom (VPL) kugomea makato ya asilimia 5 ya
fedha za klabu zinazotokana na wadhamini, makato ambayo TFF ilitaka iyakate‘kibabe’ili
kutunisha mfuko wa maendeleo ya soka la vijana na kuvisaidia vilabu vya ligi
daraja la kwanza pasipo vilabu husika kukubali.
Katika tamko hilo Mwenyekiti
huyoameonekana kuonesha msimamo wa wazi wa kuuunga mkono uamuzi huo ‘usio na
huruma’ kwa vilabu huku tamko lake hilo likionekana kuwawakilisha wakazi wote
wa Mkoa wa Ruvuma, kitu ambacho si cha kweli.
FARU imetoa maagizo
kadhaa kwa bodi ya ligi kuu na kumkana hadharani mwanasheria mahiri Damas
Daniel Ndumbaro kuwa anayoyafanya yasihusishwe na wao FARU licha ya kuwa bwana
Ndumbaro ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma.
Ni kama kusema Bwana
‘Sanga One’ alikurupuka kutoa tamko hilo kwani haikuwa na haja ya kuharakisha
kufanya hivyo ndio maana mpaka sasa hakuna mwenyekiti yeyote wa chama cha soka cha
mkoa wowote nchini aliyezungumza chochote kuhusu sakata hilo zaidi yake.
Hajatutendea haki
wakazi wa Ruvuma kwa kutoa tamko linaloonekana kuwa tamko la WanaRuvuma wote, sijui
jamii ya wakazi wa mikoa mingine imetuchukuliaje sisi wakazi wa Ruvuma kwa
kuunga mkono kitu ambacho hakihitaji ‘degree’ kukielewa, kitu ambacho kina
dalili zote za ukandamizaji.
Mara
kwa mara tumekuwa tukiandika mengi kuhusu ‘madudu’ yanayofanywa na baadhi ya
Viongozi wa soka tuliowaweka madarakani, Viongozi ambao wengi wao si watu wa
mpira ila wameingia madarakani kwa mlengo fulani.
Tabia
zao, mienendo yao lakini pia hulka zao katika maisha yao ya kila siku ni
ushahidi ulio wazi unaotanabaisha ukweli kuhusu Viongozi wengi wa namna hii
ambao kimsingi hawaitakii mema soka yetu watanzania.
Mpaka
sasa bado sijajua sababu iliyomfanya Sanga One auvae ujasiri wa kutoa tamko
hilo kubwa, tamko ambalo kwa akili ya kawaida kabisa linapingana na wengi kwani
hali ya uchumi kwa vilabu vyetu vingi ipo wazi, vilabu vyetu vingi vinaandamwa
na ukata.
Sijajua
kama lengo lake lilikuwa kujipendekeza kwa Malinzi au vipi lakini alichokitamka
Mwenyekiti huyu kamwe hakikuwawakilisha wakazi wa Mkoa wa Ruvuma. Narudia tena
tamko la Bw. Sanga One lilikuwa ni tamko lake yeye binafsi na wafuasi wake
ambao wanamuunga mkono (kama wapo) lakini si wana Ruvuma wote kama wengi
wanavyofikiri.
Ifikie
wakati kabla ya kutoa matamko haya ni jambo la msingi kama tutarudi nyuma na
kuzitathmini nyadhifa zetu kwa jamii lakini pia madhara ya kile tunachokizungumza
tena mbele ya halaiki ya watu.
Huenda
kuna suala lililojificha nyuma ya tamko hili lakini Je, kama lipo kuna haja ya
kulificha? Wakati wenzetu katika mikoa mingine wanawaza namna ya kuzipandisha timu
zao katika Ligi kuu ya Vodacom (VPL) sisi ambao kwa zaidi ya miaka miwili sasa
hatuna timu katika VPL tunaitisha mikutano na waandishi wa Habari na kuzungumza
vitu visivyo na ‘kichwa wala miguu’ eti kwa sababu fulani kasema, Je tutafika?
Ndio
maana hata Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Al
Haji Juma Nkamia hakuhitaji kuumiza kichwa kutoa uamuzi kuhusu maamuzi haya ya
TFF badala yake mapema jana alikutana na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) na ule wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na kuagiza kusitishwa kwa zoezi la
ukatwaji wa asilimia 5, huyo ndiyo Kiongozi bora.
Kama
hiyo haitoshi, kwa niaba ya Serikali, Nkamia aliitaka TFF kukutana kwa pamoja
na wadau hao, halafu wafikie mwafaka kabla ya kurejea serikalini.
“Wanatakiwa
wakutane, wazungumze na kukubaliana na siku nzuri ya kufanya hivyo nimeona ni
Jumamosi.Baada ya hapo watakachofikia mwafaka, basi watarudi serikalini na sisi
tuangalie, lakini suala la kukata fedha hizo kweli nimesitisha na sasa
liangaliwe hilo la kukutana kwanza,” alisema Nkamia ambaye kitaaluma ni
mwanahabari mzoefu lakini pia ni Mdau mkubwa wa Michezo tofauti na hao wengineo.
Mkutano
huo unasubiriwa kwa hamu kwa kuwa pande zote tatu zimekuwa na msimamo wa aina
mbili.
Bodi ya
ligi pamoja na klabu hizo za ligi kuu, zimesisitiza haziwezi kukubaliana na
hilo la kukatwa fedha zao za udhamini kwa kuwa mikataba ya Vodacom na Azam Tv
iko wazi na haielezi hilo la asilimia tano ndio maana Dk. Ndumbaro ameamua
kulivalia njuga suala hilo kwa leng la kupigania haki ya wateja wake
wanaoonekana kutaka kudhulumiwa.
Lakini
tayari TFF kupitia Rais wake Jamal Malinzi ilishatangaza suala hilo halitakuwa
na mjadala na lazima wakatwe.Pia kwa hesabu za kawaida, inaonyesha TFF
inachukua fedha nyingi zaidi kuliko hata klabu moja moja kupitia udhamini wa
Vodacom na Azam TV.
Haihitajiki
uwe na ‘degree’ au ‘masters’ kupambanua mdahaka huu zaidi ya akili ya kawaida
sana ambayo hata mtoto mdogo anaweza akawa na majibu stahiki.
SANGA ONE AMEPOTOKA,
HAKUWASEMEA WANARUVUMA, ALIJISEMEA YEYE MWENYEWE NA WAFUASI WAKE.
Naomba kuwasilisha.
Ni mimi mwakilishi wa WanaRuvuma wengi wanaoipinga kauli ya
Sanga One na ile ya Rais wa TFF, Bw. Jamal Malinzi napatikana kwa simu namba
0767 57 32 87)
Post a Comment