Na
Oswald Ngonyani.
Unataka mshahara mkubwa
kuliko? Fedha nyingi kwenye uhamisho? Au unahitaji nini zaidi katika maisha
yako ya usakataji wa kabumbu? Mwanamume fulani aliyezaliwa tarehe 7 Mwezi
Januari mwaka 1966 jijini Lisbon-Ureno ndiyo suluhisho la hayo yote.
Namzungumzia Jorge
Paulo Agostinho Mendes maarufu kwa jina la Jorge Mendes wakala wa kimataifa wa
mchezo wa soka anayeonekana kuimudu barabara kazi hiyo.
Jorge Mendes ndiye
wakala wa mmoja wa makocha bora wa soka Jose Mourinho, lakini pia wakala wa
mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani Cristiano Ronaldo na wachezaji wengi wa
hadhi ya juu barani ulaya.
Katika miaka minne
iliyopita Mreno huyu amepokea tuzo mara mbili ikiwepo tuzo ya wakala bora
inayotolewa na Globe Soccer Awards. Kampuni yake ya Gestifute International
inaingiza $200 milioni kwa mwaka. Mendes pia ni mahiri katika kufanikisha
madili makubwa ya usajili hasa kwa wachezaji wa kibrazil na kireno.
Kwa siku za karibuni, Soka
imekuja kuwa biashara nzuri mno tena nzuri kuliko.Jukumu la mawakala limezidi
kuwa na umuhimu mkubwa huku muda mwingine likiwasumbua sana makocha na vilabu
kadhalika.
Vitendo vya kuvitishia
vilabu ili kuongezewa mishahara au kutishia kuondoka vimeshaanza kuwa vya
kawaida sana kutoka kwa mawakala ambao nia yao ni kuendelea kutengeneza fedha
nyingi kupitia wateja wao. Imetokea kwa takribani miaka 10 iliyopita ikiwa
mchezaji anataka kuondoka kwenye klabu, Mendes ndio mtu anayepigiwa simu
kushughulikia dili hilo.
Oktoba 9 mwaka huu 2014
Mashirika mbalimbali ya Kimataifa yanayojishughulisha na Habari hususan habari
za Michezo yalionekana kumzungumzia sana mchezaji nguli wa Klabu ya Real Madird,
Cristian Ronaldo.
Mwanandinga huyu
alizungumziwa kutokana na ukweli kuwa wakala wake alikuwa ameweka bayana kuwa
nyota huyo hana mpango wowote wa kurejea Manchester United na anatarajia
kutundika daruga zake akiwa na Real Madrid.
Pengine habari hii ilileta
ukakasi mkubwa kwa Mashabiki wengi wa Man U, lakini siku zote lisemwalo lipo na
kama halipo ujue linakuja, wakala huyo sidhani kama alikuwa na lengo la
kujifurahisha, ni wazi kuwa alikuwa amemaanisha.
Ronaldo mwenye umri wa
miaka 29 tayari amefunga mabao 15 msimu huu ikiwemo hat-trick yake ya 22 katika
La Liga. Kwa siku za karibuni, kumekuwa na tetesi zinazomhusisha Ronaldo
na kurejea katika klabu yake ya zamani ya United aliyokuwa ameifanyia mambo makubwa.
Taarifa hizo kwa kiasi
kikubwa zilionekana kuwapa faraja sana Mashabiki wa Man U ambao kwao mchezaji
huyu ni kama ‘Lulu’ na wanatamani sana arejee pale Old Trafford yalipo makao
makuu ya klabu yao hiyo.
Wakati wengi wakiwa na
imani ya kurejea kwa nyota huyo, kwa bahati mbaya taarifa hizo zimekanushwa na
wakala huyo mwenye ushawishi mkubwa kwa Ronaldo.
Mendez amesema kuwa Ronaldo
ana furaha zaidi kuwepo Madrid na ataendelea kuvunja rekodi zote na kustaafu
akiwa hapo na si kwingineko. Bila shaka matamshi haya yaliwaumiza sana
mashabiki wa United.
Kauli hiyo au maneno hayo
ni kama yamewafumbua macho wakereketwa wengi ambao kwa kila hali walionekana
kuzipa nafasi zaidi habari hizo za Uzushi ambazo wengi wao walijikuta wakiziamini.
Hazikuwa habari za
uhakika kutokana na ukweli kuwa wote wawili Ronaldo lakini pia wakala wake, hawakuwahi
kuzungumza chochote mpaka Mendez alipoamua kuweka bayana.
Kama hiyo haitoshi,
Wakala huyo aliendelea kumnadi mteja wake kwa kudai kuwa haitawezekana kutokea
mchezaji wa aina yake kwa kipindi kirefu sana, kwani kila siku anazidi
kuimarika na ataendelea hivyo mpaka atakapofikia miaka 40. Ikumbukwe kuwa Ronaldo
aliondoka United kwenda Madrid mwaka 2009 kwa kitita cha paundi milioni 80.
Wakala huyo ambaye
anaonekana kumkubali sana Ronaldo ameiweka Man U njia panda hasa kwa mashabiki
wake ambao bado wangali wakiililia huduma ya Ronaldo klabuni hapo japo timu yao
si mbaya sana kwa sasa.
Kwao, uwepo wa akina
Robin Van Persie, Radamel Falcao, Angel Di Maria, Wayne Rooney na wengineo
wengi bado wanaona haitoshi mpaka Ronaldo atakaporudi kundini kitu ambacho
mpaka sasa kimeonekana kuota mbawa.
Pengine zinaweza zikawa
habari za kutia simanzi kwa mashabiki wa Man U, lakini ukweli kuhusu Ronaldo
kwenda klabuni hapo upo mikononi mwa wakala tajiri na mwenye ushawishi mkubwa
kwa mchezaji huyo, Jorge Mendes.
Binafsi, sijaona ubaya
wa kikosi cha sasa cha Manchester United japo uwezo wa Ronaldo ungeweza kuwa
msaada mkubwa zaidi kwa vijana hao wa Van Gaal na hata kujihakikishia uhakika
wa kuchukua ubingwa wa EPL.
Hapana shaka matumaini
ya kumnasa Ronaldo yametamatika, kilichobaki ni kumuona Van Gaal akiwatumia
vema wachezaji aliokuwa nao ili kuweza kujenga imani kwa mashabiki waliokosa
imani na kikosi cha sasa kinachoongozwa na kapteni ‘mtata’ Wayne Rooney.
(Maoni
& Ushauri tuma kwenda 0767 57 32 87/ 0755231571)
Post a Comment