Na Oswald Ngonyani.
Inaweza ikazidi kuwapa hasira zaidi mashabiki wa
‘The Gunners’ lakini wakati mwingine ni jambo jema sana kuukubali ukweli,
hususani ukweli unaouma kama huu ambao nitauzungumzia kwa siku ya leo.
Msomaji wangu usije ukajiuliza swali kuhusu ukweli
upi ninaouzungumzia. Kuwa mpole, mintarafu ya jawabu la swali hili ni rahisi
sana kulipatia utatuzi.
Nauzungumzia ukweli wa ndani ya uwanja kuhusu ubabe wa
Jose Mourinho kwa Arsene Wenger.
Sijui ni kwanini, lakini pengine Jose Antonio
Mourinho ana kitu cha ziada zaidi kinachoonekana kumnyima raha mara kwa mara
Arsene Wenger na hata katika mechi za timu hizo wengi hujikuta wakiwa na
matokeo tayari tena hata kabla ya mchezo wenyewe.
Unadhani kwanini watu huwa na matokeo ya nje ya
uwanja ya mchezo baina ya Arsenal na Chelsea? Hakuna haja ya kuzunguka, uwepo
wa Mourinho pale darajani ndio haswa sababu ya Arsenal kufungwa hata nje ya
uwanja.
Tazama mchezo wa Jumapili iliyopita ulivyoonekana
kuwa na upinzani mkubwa lakini mwisho wa siku Chelsea wakiwa nyumbani
waliendeleza wimbi la ushindi kwa washika bunduki hao na kuzidi kujenga
historia ya ubora wa Mourinho kwa Wenger.
Nakumbuka kabla ya mchezo wa Jumapili tayari
rekodi za makocha hao zilikuwa zinaonekana kumpa ushindi Mourinho ingawa kikosi
cha Arsenal cha msimu huu kinaonekana kuwa bora zaidi ukilinganisha na kile
kilichofungwa magoli 6 katika msimu uliopita.
Unadhani kwanini Arsenal pamoja na kuwa na kikosi
bora walilala pale darajani? Uwepo wa Mourinho pale Chelsea ilikuwa ndio haswa
sababu ya watoto hao wa Wenger kuendelea kuwa ‘mdebwedo’.
Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa rekodi zinazohusisha
timu hizo zinaweka bayana kuwa kabla ya mchezo wa Jumapili Arsene Wenger alikuwa
amekutana na Mourinho mara 11 katika mechi za Barclays Premier League (EPL).
Tazama, katika mechi hizo zote Mourinho alikuwa
ameiongoza timu yake kushinda michezo 6 na kutosa sare 5, huku Wenger akiwa
hajawahi kuambulia ushindi dhidi ya mpinzani wake, ni kweli ukweli huu unauma
tena unauma sana.
Ni kama kusema mchezo wa Jumapili ulikuwa ni
mchezo wa 12 kuzikutanisha timu hizo na hivyo kuzidi kumpa nafasi Mourinho ya
kuthibitisha ubora wake mbele ya Wenger kwani ushindi huo unakuwa ni ushindi wa
7 katika michezo yote ya EPL waliyowahi kukutana.
Kitakwimu, mpaka sasa Wenger ameiongoza Arsenal
kufunga jumla ya magoli sita tu dhidi ya Chelsea katika michezo 12 waliyokutana wakati
Mourinho ameiongoza Chelsea kufunga jumla ya magoli 21 dhidi ya Washika bunduki
hao wa London.
Ni
wazi kuwa mashabiki wa Arsenal walitegemea makubwa sana kutoka kwenye kikosi
kilichokuwa kimesheheni asilimia kubwa ya nyota wake wakiwemo akina Szczesny,
Chambers, Mertesacker, Koscielny, Gibbs, Wilshere, Flamini, Cazorla, Ozil,
Alexis, na Welbeck lakini tamati ya mchezo huo ilizidi kuwapa machungu
yasiyomithilika mashabiki hao.
Wanaume hao
walishindwa kufanya chochote mbele ya akina Courtois, Ivanovic, Cahill, Terry,
Azpilicueta; Matic, Fabregas; Schurrle, Oscar, Hazard; na Costa ambao
wameendelea kujiimarisha kileleni mwa EPL huku wakiwa juu kwa pointi tano
zaidi.
Haikuwa
mechi ya lelemama, ilikuwa ni patashika nguo kuchanika ndio maana hata akina Mourinho
na Wenger walionekana kutaka kuzichapa kavukavu uwanjani huku mwamuzi wa mchezo
huyo akionekana kutishia kuwapeleka jukwaani.
Mechi
hiyo ilijaa vituko kibao ikiwa ni pamoja na kuchelewa kuanza kwa dakika 15, ambapo
ndani ya uwanja ushindani ulikuwa juu huku Eden Hazard na Diego Costa wakiwa
mashujaa wa Chelsea kwa kufunga mabao hayo mawili.
Pengine
kikosi cha Chelsea kilikuwa bora zaidi kuliko kile cha Wenger lakini pengine
historia ilionekana kumhukumu Wenger na hata kujikuta akiwa hana madhara mbele
ya Jeshi la Mourinho.
Ubabe
wa Mourinho kwa Arsene Wenger utatamatika lini? Hapana shaka wakati utatupatia
majibu stahiki.
(Mwandishi wa makala
haya ni Mwandishi/Mchambuzi wa Makala za Michezo ya Kimataifa katika Gazeti la Michezo la
Dimba, anapatikana kwa simu namba 0767 57 32 87 au kwa barua pepe
ngonyanioswald@gmail.com)
Post a Comment