0
Jamal-Malinzi-1Kamati ya utendaji ya Chama cha soka mkoa wa Ruvuma (FARU) kupitia kwa Mwenyekiti wake bwana Golden Sanga maarufu kama Sanga One  hapo jana kupitia kituo pekee bora cha redio cha mkoani Ruvuma kinachosikika kupitia masafa ya 93.0 Jogoo Fm kwenye kipindi chake cha Michezo Leo kimetoa tamko rasimi kuhusiana na fukuto linaloendelea hivi sasa kwenye mpira wa miguu baina ya shirikisho la soka la Tanzania TFF, Bodi ya Ligi na vilabu vinavyoshiriki ligi kuu.

Katika tamko hilo lililotolewa na FARU limeonesha wazi wazi kuunga mkono kwa chama hicho cha soka kwa maamuzi ya TFF kukata asilimia tano ya mapato ya milangoni ili kutunisha mfuko wa maendeleo ya soka la vijana na kuvisaidia vilabu vya ligi daraja la kwanza.

Kupitia redio Jogoo FARU imetoa maagizo kadhaa kwa bodi ya ligi kuu na kumkana hadharani mwanasheria mahiri Damas Daniel Ndumbaro kuwa anayoyafanya yasihusishwe na wao FARU licha ya kuwa bwana Ndumbaro ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma.

Siku za hivi karibuni kumeibuka mvutano baina ya TFF, Bodi ya ligi na vilabu vya ligi kuu kuhusiana na maamuzi ya kamati ya utendaji ya TFF kamua kuvikata vilabu vya ligi kuu asilimia tano ya mapato ya milangoni suala ambalo lilipelekea vilabu hivyo kwenda kutafuta msaada wa kisheria ili kujinusuru na makato hayo yasiyo na msingi.

Katika tamko lake FARU wameonesha ni jinsi gani wamekurupuka kutoa tamko pasi na kujiuliza maswali kadhaa kabla ya kufanya hivyo kwani kimsingi ukiangalia kwenye tamko lao hutuma ndio zimejaa kuliko mambo ya msingi maana imediriki kumtaja na kuziingilia kazi za kampuni ya mwanasheria Damas Ndumbaro kwa kusema wao kama FARU hawahusiki naye lich ya kuwa ni mzawa wa mkoa wa Ruvuma.

Labda kuna jambo ambalo FARU mmelisahau kuhusiana na Damas, nalo ni kuwa aliye mwana Ruvuma ni Damas Ndumbaro na si taaluma yake ya shaeria wala kampuni yake. Hivyo kitendo cha yeye kuvitetea vilabu kisihusishwe na uanasheria wake wala kampuni yake ya sheria kwani hivyo ni Lila na Fila ambavyo kamwe havitangamani.

Mpira wa tanzania mara kadhaa umekua ukirudishwa nyuma na viongozi kuendeleza makundi ya uchaguzi hata mara baada ya uchaguzi kupita. hili limejitokeza miaka kadhaa iliyopita na wanaruvuma tunaweza kujiuliza swali moja tu lamsingi kuwa je katika kipindi chote ambacho Leodger Tenga alikua madarakani ni mara ngapi amewahi kuja ,koani Ruvuma? hapo unaweza kupata jibu kwanini FARU imetoa tamko haraka haraka.

Lakini wadadisi wa mambo wanadai kuwa tofauti za kiuchaguzi baina yake na aliyekuwa mwenyekiti wa FARU wa wakati huo ndugu Joseph Mapunda ni moja katiya sababu za kigogo huyo kumaliza mihula yake pasi na kukanyaga mkoani hapa hata mara moja na inasemekana kuwa Mapunda alikua mfuasi wa Ndolanga kwenye uchaguzi wa awali uliomwingiza Tenga madarakani.

FARU walikua na kila sababu ya kutoa tamko kuhusiana na suala hili lakini kabla ya kufanya hivyo walikua na masuala kadhaa ya kujiuliza kabla ya kutoa tako hilo.

1. Mamilioni ya pesa yanayokatwa na TFF kutokana na mapato ya asilimia 3.4 ya mapato ya milangoni yanayokwenda kwenye mfuko wa maendeleo ya mpira wa miguuu (FDF) yako wapi na yamekwisha fanya nini mpaka sasa katika hayo wanayoyaita maendeleo ya mpira wa miguu na nadhani mwenyekiti wa FARU anaweza akawa na majibu sahihi kwani yeye ni mmoja kati ya wajumbe wa kamati ya udhibiti na ukaguzi wa fedha ya TFF.

2. Kama TFF inakata pesa kutoka kwa vilabu kutoka kwenye mapato ya mlangoni kwa lengo la kuyaweka kwenye mfuko wa maendeleo ya mpira wa miguu (FDF) je maendeleo ya mpira wa miguu hayahusishi soka la vijana na kama yanahusisha sasa hizi asilimia tano ni za nini sasa ikiwa zipo pesa zinazokatwa kwa madhumuni sawa na hayo?

3. Kampuni ya vinywaji baridi ya Cocacola imeamua kuwekeza katika soka la vijana kwa kuanzisha michuano ya Copa Cocacola je wao kama TFF wamechukua hatua gani madhubuti ya kuifanya michuano kuwa na tija (Productive)? wakati katika uhalisia ni kuwa michuano haina mfumo maalumu kwani kila mwaka uendeeshaji unabadilika pasi na sababu za msingi kutolewa.

4. Ligi gani duniani ambayo vilabu vyake vinatumika kama wafadhili kwa kuchangishwa mapesa kwa kukatwa mapato ya langoni ili kuendeleza soka la vijana na kuvisaidia vilabu vilivyo katika madaraja ya chini?

5. TFF imekwisha watafuta wadhamini wangapi na kuwauzia mpango mkakati wa angalau kutaka kuanzisha ligi imara ya vijana na wadhamini wamewajibu nini kutokana na mpango wao huo amabo huenda ungekua na tija kama ungesimamiwa ipasavyo?

6. TFF imeshawatafuta wadhamini wangapi na kuwauzia mpango wa kuwaomba udhamini wa ligi daraja la kwanza wakawakatalia mpaka ifikirie na kuamua kuwa vilabu vya ligi kuu vinatakiwa kukatwa kiasi fulani cha pesa ili kuvisaidia vilabu vya ligi daraja la kwanza?

7. Endapo vilabu vikubwa viwili vya mkoani Ruvuma ambavyo FARU inavilea vya Mlale Jkt na Majimaji vingekua viko kwenye Ligi kuu na vingekua vimeamua kujiunga kwenye mgomo huo je wao kama FARU wangethubutu kutoa tamko la kuunga mkono maamuzi ya TFF ilihali watoto wao wanaowalea wangekua moja ya waathilika wa kadhia hayo?

8. TFF wametumia nguvu kiasi gani kuishawishi kampuni ya simu ya Airtel kuifanya michuano yao ya Airtel Rising Star kuwa ya nchi nzima ili iweze kuleta tija kwenye soka la vijana badala ya kuwa ikishirikisha mikoa kadhaa kama ilivyo sasa?

9. Ikiwa TFF ilifanikiwa kumshawishi mdhamini mkuu wa Taifa Stars kuanzisha michuano maalumu isiyo na manufaa yenye malengo ya kusaka vipaji nchi nzima inashindwa nini kwa makampuni mengine au mdhamini huyo huyo kuidhamini ligi daraja la kwanza au kuanzisha michuano ya vijana?

10. Kama kuna makubaliano ya kikanuni na kikatiba baina ya pande zote kuhusiana na makato hayo  iweje malalamiko yaibuke wakati ligi imekishaanza na si mwanzoni wa ligi?

FARU inawezekana wakawa wako sahihi mno katika kutoa tamko lao lakini swali la msingi linalobakia vichwani mwa watu ni Je kulikua na ulazima wowote kwa wao kulitoa tamko hilo hadharani badala ya kusubiri kuukwamisha mchakato uliotangazwa na bwana Ndumbaro wa kukusanya theluthi mbili ya saini ili kuitisha mkutano wa dharura ambao utakwenda kupiga kura ya kutokuwa na imani na Raisi?

Leo hii nchi kadhaa Duniani zimejikuta zikiingia katika matatizo mbalimbali na kufikia hata kufungiwa kujihusisha na masuala ya soka sababu moja wapo ni uongozi wa kibabe na kiimla unaowaona tabaka la watawaliwa kuwa ni majuha wasiofahamu kitu chochote kile kuhusiana na uongozi wa mpira jambo ambalo ukitazama kwa undani ndilo linalotaka kuibuka sasa ndani ya TFF kutokana na kauli za kibabe na dharau zinazotolewa na viongozi tena wa juu wa chombo hicho.

Ndumabaro, vilabu na Bodi ya ligi ni watu wenye akili timamu amabao hawawezi kupayuka payuka kama watu wa mataifa pasi na kuwa na sababu za kimsingi. Hivyo kabla ya FARU kutoa tamko walitakiwa kukaa, kujiuliza na kutahimini kwa kina kabla ya kutoa tamko ambalo ndani yake lina shutuma dhidi ya watu binafsi, vilabu au bodi ya ligi.

Labda kuna jambo wamelisahau FARU kabla ya kutoa tamko lao nalo ni kuwa aliye mwana Ruvuma nia Damas Daniel Ndumbaro na si kampuni ya uwakili ya Ndumbaro and Maleta Advocate Company (NMAC) hivyo kumkana Ndumbaro kuwa anayoyafanya yeye kama mwana Ruvuma hayahusiani na FARU ni sawa na kumkataza mwanasheria huyu asitafute mkate wake wa kila siku kupitia chombo chake halali alichokianzisha ili kujipatia mkate wake wa kila siku.

Leo hii FARU wanaona kitendo cha vilabu kutafuta msaada wa kisheria kwa Damas Ndumbaro ni kosa kubwa sana kama la uhaini ilihali wamesahau wao walishawahi kukipeleka chama cha soka Manispaa ya Songea (SUFA) kwa mwanasheria na kutaka kulipwa fidia ya milioni 50 kwa sababu tu ya chama hicho cha manispaa kusimama kidete kutetea wizi wa uuzaji wa tiketi kwenye michezo ya ligi daraja la kwanza; Amakweli ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni.

Makala hii imeandikwa na 
                           Hossam Hassan Ulaya.
                            hossamulaya@gmail.com
                                   0755231571/0713281932

Post a Comment

 
Top