0

 PeléPelé

Na Oswald Ngonyani.

Bado unaendelea kupendwa na watu wengi zaidi kuliko michezo mingine yote inayochezwa ulimwenguni kote. Unapendwa na wazee, Vijana, na hata watoto wadogo. Unapendwa na watu wa rika na jinsia zote. Nauzungumzia mchezo wa soka maarufu kwa jina la kandanda.

Wakati dunia ikionekana kuuhusudu zaidi mchezo huu, leo hii katika makala yangu haya nimeamua kuja na kitu kipya kabisa kuhusu wachezaji nguli wa ubora wa hali ya juu waliowahi kuwa gumzo katika mawanda ya soka duniani kote na hata kuitengeneza kumbukizi isiyofutika katika viriba vya ubongo vya mashabiki wengi wa soka ulimwenguni kote.

Nawazungumzia akina Edson Arantes Do Nascimento wa Brazili na Diego Armando Maradona wa Argentina ambapo ukulu wao katika usakataji wa ‘Gozi la Ng’ombe’ ungali unakumbukwa mpaka sasa.

EDSON ARANTES DO NASCIMENTO (PELE)

Kwa wengi anajulikana zaidi kwa jina la Pele. Mwanaume huyu alizaliwa tarehe 21 Mwezi Oktoba mwaka 1940 (miaka 73 iliyopita) huko Três Corações nchini Brazili.

Ni mwanasoka mstaafu anayesemakana kuwa mwanasoka wa uwezo wa hali ya juu zaidi kuliko wanasoka wengine wote duniani. Kwa wengi anatambulika kama ‘mchawi wa soka’ ambaye inasadikika kuwa uwezo wake haujafikiwa bado na mwanasoka mwingine yeyote katika historia ya soka la dunia.

Ana kimo cha mita 1.73. Mnamo mwaka 1999 alichaguliwa kuwa mwanasoka bora wa karne (World player of the Century) na shirikisho la kimataifa linalojishughulisha na historia na takwimu za mchezo wa soka (International Federation of Football History & Statistics (IFFHS))

Mwaka huo huo (1999) Pele alichaguliwa na Shirikisho la Kimataifa la Michezo ya Olympiki (OIC) kama mchezaji bora wa karne (Athlete of the Century). Kwa mujibu wa IFFHS linamtaja Pele kama mfungaji bora zaidi wa miaka yote katika michezo mbali mbali ya Ligi.

Mpaka anatundika daruga mwaka 1977, alikuwa amefunga magoli 1281 katika mechi 1363 alizocheza yaani katika michezo yote ya Ligi na hata mechi za kirafiki.

Ni miongoni mwa wanasoka wachache walioandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha rekodi ya mashujaa wa dunia yaani wanasoka wote waliowahi kuitikisa dunia katika ufumaniaji wa nyavu wakiwa na idadi kubwa ya magoli.

Nchini Brazili, Pele anajulikana kama shujaa wa miaka yote wa Taifa hilo katika Historia ya soka nchini humo. Mwaka 1961 aliyekuwa Rais wa Brazili Jânio Quadros alijikuta akimtangaza Pele kama hazina ya Taifa kutokana na mambo makubwa aliyokuwa ameyafanya katika soka.

Ana majina mengi ya utani yanayoonyesha heshima yake katika uga wa soka kitaifa na kimataifa. Nchini kwao Brazili wengi hupenda kumuita “Mfalme wa soka” lakini pia wengine humuita “Mfalme Pele” Kama hiyo haitoshi, baadhi yao humuita “Mfalme”

Alianza kujihusisha na mchezo wa soka tangu enzi, lakini jina lake lilianza kujulikana wakati akiwa na umri wa miaka 15 akiwa na klabu ya Santos ya nchini Brazili ambapo mwaka mmoja baadaye alianza rasmi kuitumikia timu yake ya Taifa.

Akiwa mchezaji wa timu ya Taifa ameiwezesha Brazili kushinda mataji matatu ya dunia kati ya mataji matano yaliwahi kuchukuliwa na Taifa hilo. Alifanya hivyo katika miaka ya 1958, 1962 na 1970 ni mchezaji pekee kufanya hivyo katika historia ya fainali za Kombe la dunia tangu zilipoanzishwa mwaka 1930 nchini Uruguay.

Pamoja na kuwa mchezaji bora wa miaka yote katika Historia ya soka la dunia, pia ni mfungaji bora wa miaka yote katika mawanda ya soka la Brazili akiwa amefunga magoli 77 katika michezo 92 aliyoicheza akiwa na timu ya Taifa.

Pele amekuwa balozi wa muda mrefu wa soka katika historia ya soka la dunia huku jina lake likitumiwa mara nyingi zaidi katika matangazo mengi ya kimataifa ambapo mwaka 2010 alichaguliwa kuwa Rais wa heshima wa klabu ya New York Cosmos, klabu ya nchini Marekani aliyowahi kuichezea kwa mafanikio makubwa.

Mwaka 1995 alitunukiwa medali ya dhahabu kwa kuwa  mdau mkubwa wa soka nchini Brazili ambapo baadaye aliyekuwa Rais wa Taifa hilo Fernando Henrique Cardoso alimteua kuwa waziri wa ziada katika wizara ya Michezo ya nchini humo.

Amekuwa mgeni wa heshima katika matamasha mengi ya michezo katika nchi tofauti tofauti ulimwenguni huku akiwa miongoni mwa wadau wakubwa zaidi katika kila nchi zinapofanyika fainali za kombe la dunia.

Mbali na kuipa Brazili makombe matatu ya dunia, Pele amekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Taifa hilo katika soka akichagiza ushindi wa pili wa Taifa hilo katika Kopa Amerika mwaka 1959 lakini pia alikuwa chachu ya ushindi wa Taifa hilo katika makombe tofauti tofauti ya barani Amerika yakiwemo Cruz Cup: 1958, 1962, na 1968, Bernardo O' Higgins Cup: 1959, Atlantic Cup: 1960, na Oswaldo Cruz Cup: 1958, 1962, na 1968.

Ameitendea haki nafasi yake ndani ya dimba na hata kujikuta akiwa na tuzo lukuki zisizohesabika kutoka kwa watu na mashirikisho mbalimbali yakiwemo FIFA, UNICEF, BBC, Gazeti la Times, na mengineyo mengi.

Ingawa kuna mengi yanazungumzwa kuhusu ubora wa soka ya zamani na ya sasa huku wachambuzi wengi wa kandanda wakiamini kwamba Mwanaume huyu alivuma sana kutokana na ukweli kuwa soka ya zamani haikuwa na upinzani sana, nadharia hiyo wala haina mashiko lakini pia haina ukweli wowote.

Yanaweza yakazungumzwa na kuandikwa mengi sana kuhusu upekee wa Pele na wanasoka wengine wa kizazi cha sasa lakini mwisho wa siku heshima yake itaendelea kutukuka daima dumu kutokana na umahiri wake uwanjani. Hapana shaka dunia itaendelea kumkumbuka sasa na hata siku zijazo.

Je ni kweli ataendelea kukumbukwa milele? Ndiyo ataendelea kukumbukwa kesho na hata keshokutwa kwa sababu aliwahi kuikonga dunia na hata kuandika kumbukizi isiyofutika katika viriba vya ubongo vya wapenda soka wengi ulimwenguni, mimi nikiwa mmoja wao.

Hapana shaka anastahili sifa, lakini pia anastahili kuheshimiwa! Kuhusu Pele naomba tuishie hapa, tukutane tena kesho katika ukurasa huu huu kwa ajili ya kumtazama nguli mwingine wa soka namzungumzia Diego Armando Maradona.

Maradona ni nani? Muargentina huyu ni Mtalaamu wa soka ambaye Waingereza wamegoma kabisa kumsamehe. Unadhani kwanini Waingereza wamegoma kumsamehe? Usikose kumakinika nami wakati ujao panapo Majaaliwa.

Wakatabahu wakaa……

 (Mwandishi ni Mchambuzi wa Makala za Kimataifa katika gazeti la Michezo la Dimba, kwa wenye Maoni au Ushauri wanaweza wakatuma kwenda namba 0767 57 32 87)


Post a Comment

 
Top