Na Oswald
Ngonyani.
Wahenga walisema ‘Mtoto wa Nyoka ni Nyoka’ Unamkumbuka
mlinda mlango mahiri wa Klabu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania enzi zile? Bila
shaka jina la mvaa Kapelo huyu ‘Peter Manyika’ haliwezi kuwa geni kwa shabiki
yeyote wa soka la bongo.
Unamfahamu golikipa kinda wa Simba aliyedaka ile
mechi ya watani Jumamosi iliyopita? Subiri nitakueleza kitu.
Ilikuwa ni mechi ya wachezaji vijana dhidi ya Wachezaji Maveteran! Binafsi nilijikuta
nikimwona kwa mbali Mwameja au Kaseja wakizaliwa upya. Ashukuriwe aliyefanya
usajili huu unaoonekana kuwa na tija zaidi kwa Wana Msimbazi.
Pamoja na yote acha niwapongeze wazazi wake,
Peter Manyika na Teresa John. Hapana shaka walifanya kitu kwa ajili ya kipaji cha mtoto wao. Wakati
mwingine yatupasa kuweka ushabiki kando na hata kuweza kuzungumza ukweli ulio
wazi. Ukizingatia umri wake, na wakati aliopangwa inatosha kusema kuwa ameweza.
Unaweza ukawa ni ukweli unaouma zaidi kwa watu
fulani, lakini acha tu niuseme. Naamini kwa aliyeufuatilia mchezo ule tangu
mwanzo mpaka mwisho, ni wazi kuwa ataungana na mimi katika hili kuwa Peter
Manyika Junior, alikuwa ‘Man of the Match’
huo ndio ukweli.
Alikuwa katikati ya milingoti mitatu pamoja na
Vijana wengine wenye umri wa kuanzia miaka 20 kushuka chini waliopena majukumu
tofauti tofauti uwanjani. William Lucian, Tshabalala
Mohamed, Hassan
Isihaka, Said Ndemla, Jonas Mkude,
Ramadhani Singano, na Haroun Chanongo walionekana kuuhimili vilivyo mchezo ule
dhidi ya wachezaji wakongwe wa klabu ya Yanga akina Cannavaro na wengine.
Kwa soka la bongo, hiyo ni rekodi
mpya kwa kipa mwenye umri kama wake, hasa ukizingatia nafasi ya kipa mara
nyingi inakuwa kwa ajili ya wachezaji wazoefu zaidi tofauti na ilivyokuwa kwake.
Pengine dhana ya kufa kufaana
ilichukua nafasi zaidi kutokana na ukweli ulio wazi kuwa alipata nafasi ile baada
ya makipa wote wawili wa Simba kuwa majeruhi. Nawazungumzia akina Ivo Mapunda
na Hussein Shariff ‘Casillas’ ambao waliumia kwa nyakati tofauti mjini Zanzibar
na jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Simba ilipokuwa imeweka kambi.
Kwa kilichotokea,Viongozi wa Simba,
hasa benchi la ufundi chini ya Kocha Mzambia Patrick Phiri wanastahili pongezi kwa
kujivika ujasiri wa kutotishika na ukubwa wa pambano lenyewe huku kijana wa
miaka 18 akikabidhiwa lango kulilinda.
Tazama, hata baada ya mechi
kumalizika, Magolikipa wakongwe Ivo Mapunda (Simba) na Juma Kaseja (Yanga)
hawakuweza kuficha hisia zao kwa bwana mdogo huyu. Walijivika mkaja na kuinuka
katika mabenchi ya timu zao na kwenda kumpa mkono wa Pongezi Peter Manyika
Junior.
Alifanya kazi kubwa langoni,
anastahili kupongezwa. Ndiyo maana hata Deogratius Munishi wa Yanga hakusita
kumwagia sifa huku akimnadi kuwa ‘Man of the Match’ wa mtanange ule ulioisha
kwa sare tasa.
Ndiyo maana hata baada ya filimbi ya mwisho ya
mwamuzi Israel Mjuni Nkongo kupulizwa, mashabiki wa Simba walijikuta wakimjaza
mapesa dogo huyu kwa kufanya kitu ambacho pengine hakikutegemewa kabla. Kuzuia
michomo ya akina Coutinho, Jaja na wenngineo.
“Ilikuwa
ni bahati” anasema mlinda mlango huyo wa timu ya Taifa ya vijana ya
Tanzania. “Nilikuwa tayari kucheza mchezo wowote si ule wa Yanga tu lakini
nashukuru Mungu mambo yamepita salama licha ya kutopata ushindi.”
anasema kijana huyo ambaye alionyesha kujiamini na kucheza bila papara kila
Yanga walipofanya shambulizi.
“Baba yangu ndiye silaha yangu kubwa, ni
kila kitu kwangu, amekuwa mshauri na kunieleza mambo muhimu ya kufanya katika
soka. Sasa najua nini cha kufanya” anasema , Manyika JR, ambaye
amesajiliwa msimu huu.
Ikumbukwe kuwa Simba ilikumbwa na hofu kubwa hasa
baada ya kuumia kwa golikipa namba mbili Hussein Shariff wakiwa katika michezo
ya kirafiki huko Afrika Kusini, kipa chaguo la kwanza Ivo Mapunda aliharakishwa
kupona ili kucheza mchezo huo wa mahasimu lakini badala yake kiwango kizuri cha
timu nzima kililindwa na Manyika ambaye hakuwa tayari kuona Yanga wakifunga
katika lango lake, hii ni sifa ambayo itaendelea kuzungumziwa tena na tena kwa
kinda huyu.
“Nimekuwa nikicheza na wachezaji wenzangu
uwanjani, wote tunahitaji kupewa sifa sawa, nawashukuru wachezaji wenzangu
ambao walinitia moyo kabla ya mchezo na waliniambia ‘umefanya vizuri’ baada ya
mchezo kumalizika.
Nawashukuru benchi la ufundi kwa kunipatia
nafasi katika mchezo huo wenye presha kubwa, lakini sikuwa tayari kuogopa
chochote.”Alizidi kuweka bayana Manyika Jr.
Kuna mengi sana ya
kuandika katika mchezo ule lakini acha tu nitamatishe pongezi zangu kwa bwana
mdogo huyu ambaye kwa kila hali huenda akawa hazina nyingine ya Taifa katika
siku zijazo.
Amejipambanua vya
kutosha, anastahili kuwa namba moja pale Msimbazi. Pengine akina Ivo Mapunda na
Hussein Shariffu watahitaji kufanya kazi ya ziada zaidi ili kuweza kulinda
heshima, vinginevyo benchi linawasubiri.
(Maoni/Ushauri
tuma kwenda namba 0767 57 32 87)
Post a Comment