TIMU ya Yanga kesho inashuka uwanja wa taifa Dar es Salaam kuikabili
Ruvu Shooting ya Pwani huo ukiwa ni mchezo wa raundi ya tisa kwa timu
hiyo inayoshika nafasi nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 14.
Yanga inaingia katika mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbu ya kutoka
sare ya 2-2 na Mabingwa watetezi Azam FC, katika pambano lililopigwa
Desemba 28 mwaka 2014 kwenye uwanja huo.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa gumu kutokana na kila upande kuhitaji
pointi tatu ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa
ligi hiyo ambao kwa sasa unaelekea ukingoni mwa mzunguko wa kwanza.
Yanga ambayo inazidiwa michezo miwili na Ruvu Shooting, kutokana na
timu hiyo kwenda kushiriki michuano ya Mapinduzi itataka kushinda mchezo
huo ili kujiweka katika nafasi ya kuongoza ligi hiyo endapo wapinzani
wao Azam na Mtibwa Sugar watapoteza mechi zao za kesho wanazocheza
ugenini.
Kocha wa Yanga Mholanzi Hans van der Pluijm, amesema kikosi chake
kipo katika hali nzuri kuelekea kwenye pambano hilo la kesho na kwa wiki
nzima ambayo wameweka Kambi Bagamoyo, amekuwa akiyafanyia kazi
mapungufu ambayo ameyaona kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Pluijm ameiambia Gaol anafurahi kuona kikosi chake hakina mchezaji
aliyekuwa majeruhi hivyo ananafasi kubwa ya kutumia kikosi imara ambacho
kitawasambaratisha Ruvu Shooting na kufikisha pointi 17 kabla ya
kuelekea Tanga wiki ijayo kucheza na Coastal Union kwenye uwanja wa
Mkwakwani.
Pluijm ambaye hiyo itakuwa mechi yake ya pili tangu aliporejea kwa
mara ya pili kuifundisha timu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Mbrazili
Marcio Maximo, amesema anajivunio uimara na kiwango bora kilichoonyeshwa
na wachezaji wake kwenye michuano ya Mapinduzi japo safu ya
ushambuliaji ilimuangusha kwa kupoteza nafasi nyingi za mabao
walizozipata.
“Tangu tumeanza maandalizi kujianda na mechi za Ligi Kuu nimekuwa
nikidili zaidi na safu ya ushambuliaji nataka kuata ushindi wa mabao
mengi na hilo linawezekana kutokana na uwezo waliokuwa nao washambuliaji
wangu kama Mrisho Ngasa Kpah Sherman, Amisi Tambwe na Andrew
Coutinho,”.
Pluijm amesema pamoja na ugumu uliopo lakini atahakikisha anawafunga
Ruvu Shooting ili wachezaji wake waweze kuwa na ari ya kujiamini wakati
watakapo kwenda kucheza mechi mbili za uganini za Tanga na Mbeya dhidi
ya Mbeya City ambayo imeanza kuibuka baada ya kuanza vibaya msimu huu.
Lakini wakati kocha wa Yanga akipania kikosi chake kuibuka na ushindi
katika mchezo huo kocha wa Ruvu Shooting, Tom Olaba anakiingiza kikosi
chake kesho akiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 7-0, kwenye mchezo wa
raundi ya pili msimu uliopita chini ya Mholanzi huyo Pluijm.
Olaba anaingia kwenye mchezo wa kesho huku pia akiwaza kipigo cha bao
1-0 walichokipata kwenye uwanja wa Mkwakwani Jumamosi iliyopita dhidi
ya Mgambo JKT , lakini kibaya zaidi kocha huyo nikama yupo katika wakati
mgumu kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye ligi.
Ruvu Shooting katika msimamo wa Ligi inashika nafasi ya 9 ikiwa na
pointi 11 huku ikiwa mbele kwa michezo miwili dhidi ya Yanga ambayo
imecheza michezo nane na ipo katika nafasi ya nne endapo itashinda
mchezo huo itazidi kupaa kileleni na kuongeza presha kwa timu za Mtibwa
Sugar , JKT Ruvu, na Azam zilizopo juu yake.
Kocha Tom Olaba amesema baada ya mchezo wa Tanga tayari kikosi chake
kimewasili Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa kesho na anajivunia
uwepo wa mshambuliaji Betram Mwombeki na wengine ambao anaamini wanaweza
kuwashangaza watu kwa kuonyesha kiwango cha juu na kuifunga Yanga.
Chanzo: Goal.com
Post a Comment