Chelsea walifanikiwa kudumisha nafasi yao kileleni mwa Ligi ya Premia
kutokana tu na hali kwamba jina lao limo mbele kwenye alfabeti
tukiingia mwaka mpya lakini watahitaji kufanya kazi ya ziada nyumbani
dhidi ya Newcastle United Jumamosi kuzuia Manchester City wasiwapite.
Vijana wa Jose Mourinho walibeba alama nne pekee kutoka kwa tisa
walizopigania kipindi cha mechi nyingi za sikukuu, kichapo cha
kunyenyekeza cha 5-3 wakiwa Tottenham Hotspur Januari 1 kikiwafanya
mabingwa City kuwa sawa nao kwa alama baada ya wakati mmoja kuwa nyuma
kwa alama nane.
Ushindi rahisi Kombe la FA dhidi ya klabu ya daraja la pili Watford
kuliwapa Chelsea kitulizo, lakini watakuwa wenyeji wa Newcastle
wasiokuwa na meneja kwa sasa, wakijua kwamba hakuna nafasi ya makosa
kati ya sasa na Mei.
City, walio sawa na Chelsea kwa alama (46), tofauti ya mabao (25) na
mabao waliyofunga (44), watakuwa ugenini dhidi ya Everton siku hiyo,
wakilenga kuendeleza mkimbio safi ambao umewazalishia alama 26 kutoka
kwa 30 walizopigania.
Baada ya klabu ya Mourinho kutishia kuponyoka mapema msimuni, mbio za
ligi sasa ziko wazi mkondo wa lala salama wa mechi 18 ukianza.
Chelsea walianza kujikwaa ugenini walipolazwa na Newcastle na Tottenham kisha wakatoka sare Southampton.
Wamekuwa shwari nyumbani hata hivyo, wakishinda mechi tisa kati ya
tisa za ligi, na straika wao Loic Remy anaamini kujikwaa kwao majuzi sio
mwanzo wa kuteleza kwao.
“Hali ni nzuri kikosini na tunaangazia malengo yetu,” alisema Remy aliyefunga dhidi ya Watford.
“Msimuni, kila timu itakuwa hatarini wakati fulani, kwa hivyo kwetu
tunatumai tushapitia kipindi chetu mechi mbili zilizopita za ligi.”
John Carver anazidi kushikilia kazi Newcastle kwa muda baada ya Alan
Pardew kuhamia Crystal Palace na atakuwa macho kuzuia kichapo cha
Chelsea anapozidi kusaka kazi hiyo kwa muda mrefu.
City watatiwa nguvu na kurudi kwa mfungaji mabao bora wao Ligi ya
Premia Sergio Aguero wanaposafiri kukutana na Everton ambao wameshindwa
mechi nne zilizopita ligini.
"Nilitaka kuwajulisha kwamba nimeanza kazi uwanjani. Aste aste
lakini nitarudi wakati ufaao zaidi. Asanteni sana kwa heri zenu!” raia
huyo wa Argentina, aliyeumia goti walipolaza Everton 1-0 nyumbani,
alisema kwenye Twitter.
Edin Dzeko na nahodha Vincent Kompany pia wanatarajiwa kurudi upande wa Manuel Pellegrini.
Nambari tatu na nne watakutana Old Trafford Jumapili Manchester
United wakiwa wenyeji wa Southampton huku Tottenham walioamka, sasa
wakiwa nambari tano, wakiwa mtihani wa kwanza wa Pardew ligini akiwa
meneja wa Palace Jumamosi. Tottenham wanaweza kufika nambari nne
wakishinda mechi hiyo.
Tottenham wanakabiliwa na mechi sita katika siku 21, ikiwa ni pamoja
na mechi mbili za nusufainali League Cup na mechi ya marudiano Kombe la
FA dhidi ya Burnley.
Arsenal walio nambari sita watakuwa wenyeji wa Stoke City Jumapili.
Chanzo:- Supersport.com
Post a Comment