0
Match Preview: Stand United- Azam FC, Wageni kuendeleza mbio za kufukuzia Ubingwa
Azam FC wanapewa nafasi kubwa ya kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo lakini lolote linaweza kutokea kutokana na uimara wa kikosi cha Stand United.

HUU ni mtihani mwingine kwa kocha mpya wa wenyeji Stand United Mathia Lule, ambaye baada ya wiki iliyopita kufungwa mabao 2-1 na JKT Ruvu kwenye uwanja wa Azam Complex kesho itakuwa ni siku la kulipa kisasi watakapo wakaribisha mabingwa watetezi klabu tajiri ya Azam uwanja wa Kambarage Shinyanga.

Japo wageni Azam FC wanapewa nafasi kubwa ya kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo lakini lolote linaweza kutokea kutokana na uimara wa kikosi cha Stand United ambacho kimefanyiwa mabadiliko makubwa kwenye usajili mdogo na kuweza kupata sare mbili za ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar na Polisi Moro wiki mbili zilizopita kabla ya kufungwa na JKT Ruvu.

Kocha Mathia Lule raia wa Uganda ameonekana kukibadilisha sana kikosi hicho ambacho kabla kilikuwa chini ya kocha mzawa Emmanuel Masawe, na sasa kimekuwa kikitoa upinzani kwa timu nyingi kubwa licha ya kushika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 11.

Katika dirisha dogo Stand United ilisajili wachezaji saba wapya ambao ni Hamis Thabit (Yanga), Chanongo (Simba), Nduwimana (Burundi), Shaban Kondo, Chinedu, Hamis Shengo na Misheto (Ujerumani).

Kutua kwa nyota hao kumekifanya kikosi hicho kuwa moto wa kuotea mbali na mashabiki wengi wanatazamiwa kufurika kwa wingi kwenye uwanja wa Kambarage, wakitaka kukiona kikosi chao kikicheza kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa mapumziko ya muda mrefu.

Kwaupande wa Azam FC japo itamkosa mshambuliaji wake tegemeo John Bocco lakini uwepo wa Mrudi Didier Kavumbagu na Brian Majwega, kunafufua matumaini ya kikosi cha kocha Josph Omog kupata ushindi wa ugenini na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.

Azam FC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutolewa kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi na Mtibwa Sugar licha ya kuwa ni moja ya timu ambayo ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kunyakua taji hilo mwaka huu.

Mchezaji kama Serge Wawa Frank Domayo na chipukizi Mudathir Yahya wameonekana kufanya vizuri kwenye mechi za karibuni na kumshawishi Omog aweze kuwatumia wakiwa ni ingizo jipya kwenye kikosi hicho ambacho kinashika nafasi ya tatu kwa sasa kikiwa na pointi 14 sawa na Yanga.

Niwazi kocha wa Omog lengo lake kubwa litakuwa ni kuondoka Kanda ya Ziwa na pointi zote tatu ili kunyemelea kiti cha uongozi ambacho hawaja kikalia tangu Oktoba nne ilipopata ushindi mdogo wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons na Mtibwa kuifunga Ndanda FC 3-1, na kukalia kiti cha uongozi.

“Tunarudi kwenye ligi tukiwa na matarajia ya kufanya vizuri kutokana na kiwango tulichokuwa nacho hivi sasa tumefanya maandalizi ya kutosha ikiwemo kushiriki michuano ya Mapinduzi lakini tuliweka kambi Uganda lengo ni kufanya vizuri na hilo halina mjadala,”amesea Omog.

Omog amesema katika mchezo huo atamkosa nahodha wake Bocco lakini anaamini wachezaji waliopo Kipre Tchetche na Didier Kavumbagu watafanya vizuri kazi yao na kuipeperusha vyema bendera ya Azam FC.

“Naiheshimu Stand United pamoja na ugeni wake lakini imekuwa ikitoa changamoto kwa timu kubwa kwahiyo tumejiandaa kuhakikisha tunaweza kukabiliana nayo ikiwa nyumbani kwao na ninaamini tunaweza kupata ushindi,”amesema Omog.

Chanzo: Goal.com

Post a Comment

 
Top