Chelsea, Manchester United, Manchester City na watetezi Arsenal
walifuza raundi ya nne ya kombe la FA Jumapili huku washiriki wenzao wa
ligi ya Premier wanaotatizika QPR wakiondolewa na klabu cha daraja la
tatu, Sheffield United.
Arsenal walijikatia tikiti kwa kuwanyamazisha timu waliolaza fainali
ya musimu jana Hull City 2-0 kwenye uga wao wa Emirates. Beki Per
Mertesacker aliwapeleka kifua mbele kwa kichwa kutokana na kona yake
nyota Alexis Sanchez dakika ya 20.
Sogora huyo wa Chile alihakikisha ushindi na bao maridadi alipogeuka
na kufyatua kombora la kujipinda kisandukuni ikisalia dakika nane muda
wa kawaida kutimia.
Vingozi wa pamoja wa ligi ya Premier, Manchester City, walitolewa
jasho jembamba na timu ya ngazi ya pili, Championship, Sheffield
Wednesday kwenye kasri yao ya Etihad kabla ya kufuzu 2-1 na bao la
ushindi la dakika ya 91 kutoka James Milner.
Wednesday ambao walilipuliwa 7-0 kwenye kombe la League Cup uwanjani
huo huo September walitwaa uongozi wa mshtuko dakika ya 14 kupitia
Atdhe Nuhiu, lakini Milner, aliyesherehekea mwaka wake wa 29 tangu
kuzaliwa, alisawazisha dakika ya 66 kabla ya kuibuka shujaa.
Majirani wao Manchester United walihemeshwa na Yeovil Town wa daraja
la tatu kabla ya kunyakua ushindi wa 2-0 kupitia mabao ya Ander Herrera
dakika ya 64 na staa Angel Di Maria aliyetoka benchi na kutia kizimbani
dakika ya mwisho ya kipindi cha kawaida.
Chelsea walibarizi na kujizawadia ushindi wa 3-0 bila tatizo dhidi
ya Watford nyumbani mwao Stamford Bridge kupitia magoli ya kipindi cha
pili kutoka Willian, Loic Remy na Kurt Zouma.
Huenda ikawa ishara njema kwa vijana wa Jose Mourinho ambao walilaza Watford njiani ya kutwaa kombe hilo 1970, 2009 na 2010.
Sheffield United ambao walifika nusu fainali ya musimu jana
waliwakunguta wenyeji QPR 3-0 na kuwaongezea fedheha kupitia bao la
ufunguzi la Marc McNulty na mawili katika kipindi cha lala salama kutoka
Jamal Campbell-Ryce.
Southampton wa Premier watarudia mechi yao dhidi ya Ipswich wa
Championship baada ya wawili hao kutoshana nguzu 1-1 ugani St. Mary’s na
kwingineko, bao la nguvu muda ukiyoyoma kutoka Christian Benteke
liliwapatia Aston Villa wa ligi kuu ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya
vijana wa daraja la pili Blackpool.
Wrexham ambao hawajaorodheshwa kwenye ligi za kulipwa Uingereza
nusura waandikishe historia ikisalia dakika kumi ya mechi yao dhidi ya
Stoke City wa Premier kuisha lakini walisalimu amri 3-1 kufikia kipenga
cha mwisho.
Mark Carrington aliwapatia uongozi dakika ya 73 ugani Britannia
kabla ya Marko Arnautivic kusawazisha saba baadaye. Stephen Ireland
alifunga mawili ya kuchelea kuokolea vijana wa Mark Hughes fedheha.
Alan Pardew, aliyeteuliwa Jumamosi, alianza maisha mapya kama kinara
wa Crystal Palace wakati viungo vyake walipowacharaza Dover Athletic
ambao hawachezi kwenye ligi kupitia magoli mawili kutoka beki Scott Dann
katika kipindi cha kwanza kabla ya Dwight Gayle na Kevin Doyle
kukamilisha kazi baada ya mapumziko.
Sunderland walirudia ushindi wao wa fainali ya kombe hilo dhidi ya
Leeds United ya mwaka wa 1973 kwa kuwalaza wapinzani hao hao nyumbani
1-0 pale beki wa Uholanzi, Patrick van Aanholt aliibuka shujaa kwa
kubusu wavu dakika ya 33.
Tottenham wanasafiri Burnley Jumatatu kwa marudio ya fainali ya 1962
walioshinda huku Liverpool wakitembelea AFC Wimbledon kwa mechi ambayo
inaleta kumbukumbu kwa mchuano baina yao kwenye mechi ya uamuzi ya 1988.
Chanzo:- Supersport.com
Post a Comment