0
Kocha mpya wa timu ya taifa ya Brazil Dunga amemjumuisha msahambuliaji wa timu ya Santos Robinho kwaajili ya maandalizi ya michezo ya kirafiki dhidi ya Colombia na Ecuador.

Mchezaji huyo anakwenda kuchukua nafasi ya Hulk kwenye kikosi cha wachezaji 22 kutokana na mshambuliaji huyo wa Zenit St Petersburg ya huko nchini Urusi kuumia kwenye mchezo ambao timu hiyo ilipata ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Lokomotiv Moscow siku ya jumaamosi.

Robinho,aliyeichezea Brazil takribani michezo 92, hajaitumikia timu yake ya taifa tangu novemba mwaka jana dhidi ya timu ya taifa ya Chile na aliachwa kwenye kikosi cha mwalimu Luiz Felipe Scolari kilichoshiriki michuano ya kombe la Dunia kwenye ardhi ya nchini kwake Brazil mwaka huu. 

Robinho amerejea nyumbani kwa mkopo akitokea klabu ya AC Milan ya huko nchini Italy mara baada ya kocha wa timu hiyo Filippo Inzaghi kumtamkia waziwazi kuwa yeye ni mmoja kati ya wachezaji ambao hawapo katika mipango yake ndani ya klabu hiyo.

Naye mlinzi wa kushoto wa mabingwa wa Ulaya, Real Madrid Mbrazil  Marcelo amejumuishwa kwenye kikosi hicho cha Dunga  mara baada ya awali kutemwa kutokana na kuwa majeruhi.

Brazil inatarajiwa kukipida dhidi ya Colombia wiki ijayo katika mji wa Miami nchini Marekani ikiwa na takribani wachezaji kumi tu ambao walishiriki kwenye michuano ya kombe la Dunia kikosi ambacho kiliandika historia mpya kwa kupokea vichapo vikubwa vya mfululizo.

Post a Comment

 
Top