Na Oswald Ngonyani
“Maisha yana vitu vingi sana, na kamwe hauwezi kuvipata vyote, kama binadamu uliyekamilika itakupasa kuchagua kimoja ukifanye kwa utaratibu”.
Ndani ya kichwa changu ningali nikizungukwa na sauti inayopaza maneno tajwa hapo juu, sauti inayoyapaza maneno hayo kwa miali ya mwangwi.
Bila shaka ushindi wa Chile dhidi ya Argentina katika fainali ya Copa America (2016) ndiyo sababu ya ujumbe huu mzito kuweka makazi ubongoni mwangu leo hii.
Inawezekana Messi amechagua kuwa mfalme pale Catalunya,yale machozi ya wengi pale Amerika yana maana kubwa sana kwa Messi katika usiku ule, usiku wa Juni 27.
Siku zote machozi ya mwanaume hutokea mara chache sana kwa sababu maalumu ambayo pengine hushindwa kabisa kuepukika.
Katika usiku wa Jumatatu (tar. 27 Juni, 2016) Muargentina huyu mpole alilowanisha jezi yake kwa machozi.
Haiba ya upole wake iliwafanya mashabiki wengi wa Argentina wajiunge naye katika kitendo cha kumwaga machozi.
Historia ya maisha yake tangu akiwa andunje na utukufu wake katika soka viliwafanya mashabiki wake wajiinamie kwa uchungu huku wakipokezana kuinuka kujifuta machozi.
Inawezekana sijajua aliumia kiasi gani, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa Messi aliumia moyoni, tena aliumia sana.
Inawezekana hii ndiyo dhana halisi ya msemo wa Kiswahili unaosema ‘Dunia haina usawa’ Na katika hili ni kweli dunia haijalingana kwani kwa mara nyingine tena akina Alexis Sanchez walifanikiwa kuiadhibu Argentina ya Messi, Argentina ya Angel Di Maria, Argentina ya Kun Aguero.
Inawezekana maisha ya Messi yanajidhihirisha katika dhana dhahanifu ya msemo huu,"Mungu hakupi unachotaka bali anakupa unachostahili" Japo ni vigumu kidogo kuuamini msemo huu linapokuja suala la Messi na Argentina na takwimu kuhusu mafanikio ya kila moja.
Lakini Je, ni kweli Argentina hawakustahili kutwaa ndoo ya Copa America mwaka huu 2016?
Katika macho na fikra za wengi tayari Argentina ilikwisha twaa ubingwa huo wa Amerika kwa mwaka huu.
Katika fikra za wengi tayari Lionel Messi alikuwa amekwishaweka historia nyingine katika ukurasa wake pendevu wa maisha ya soka.
Inawezekana akili ya wengi ilijipa majibu pasipo kuangalia upande wa pili wa shilingi. Labda Chile haikuzungumzwa sana kwa sababu ilitwaa ubingwa huo mwaka jana (2015) mbele ya Argentina hivyo dhana ya kulipa kisasi ilikuwa inaibeba Argentina.
Kumbe mpira haupo hivyo, ndio maana siku zote mchezo huu unatajwa kuwa miongoni mwa michezo michache yenye kuleta maajabu makubwa katika uso wa dunia.
Chile hii ya akina Alexis Sanchez na Eduardo Vargas haikupaswa kudharaulika kama ilivyokuwa.
Inawezeakana Kocha wa Argentina (Gerardo Martino)alilijua hilo ndiyo maana wakati fulani alikiri wazi kuwa fainali hiyo ingekuwa ngumu.
Inawezekana ulikuwa ni ubingwa wa nje ya uwanja kwa Argentina, inawezekana zilikuwa ni tuzo maridhawa za kabla ya mchezo kwani baada ya mchezo Argentina pamoja na kuwa na kikosi kipana, bado walipoteza.
Ni wazi kuwa nyakati hizi zitakuwa za maumivu zaidi kwa mashabiki wa Argentina, nyakati hizi zitapeleka simanzi pia kwa Wafuasi wa Lionel Messi, mwanasoka bora mara nyingi zaidi wa Dunia.
Kikubwa ambacho kinaniumiza nafsi ni kwamba kila Argentina inapopata matokeo hasi ni lazima Lionel Messi alaumiwe, lakini kila inapofanya vema wengi huona kawaida tu.
Wanaomlaumu Messi wamejifanya kujisahaulisha kuhusu uwepo wa wachezaji wengine wa ubora ya juu katika soka ya dunia kikosini hapo. Wamejifanya kutowafikiria akina Aguero, Di Maria, na wengineo wengi.
Kumlaumu Messi katika kila ambacho Argentina inakikosa uwanjani ni kumuonea bure. Kwa sasa Argentina ina mafundi wengi sana wa mpira waliojifanya kujificha kwenye kivuli cha Messi.
Kama ilivyo kuwa mwaka 2007 katika fainali ya Copa Amerika dhidi ya Brazili, kama ilivyokuwa mwaka juzi katika fainali za kombe la dunia kule Ujerumani, kama ilivyokuwa mwaka jana katika fainali za Copa Amerika nchini Chile, ndivyo ilivyokuwa mwaka huu nchini Marekani.
Jibu bado halijabadilika, wanandinga hao mahiri wameendelea kujificha nyuma ya Messi hadi sasa.
Kwanini Argentina, kwanini Lionel Messi? Hili ndilo swali ambalo limeonekana kukosa majibu katika vichwa vya wadadisi wengi wa mchezo wa kandanda kote duniani.
Kwanini Argentina, kwanini Lionel Messi? Hili ndilo swali ambalo limeonekana kukosa majibu katika vichwa vya wadadisi wengi wa mchezo wa kandanda kote duniani.
Ikumbukwe kuwa Argentina imepoteza mchezo wa fainali kwa mara ya nne mfululizo. Kombe lao la mwisho kwenye michuano mikubwa lilikuwa ni Copa America mwaka 1993, kipindi ambacho Messi ndio kwanza alikuwa anafikisha miaka 6.
Bahati mbaya kwa mashabiki wa Argetnina ni kwamba baada ya kupoteza mchezo huo wa fainali ya Copa America 2016, Messi ameamua kuachana na timu yake ya taifa. Amestaafu kukitumikia kikosi cha Albiceleste.
“Kwa sasa timu ya taifa basi tena. Baada ya kupoteza fainali nne sitaendelea tena kuitumikia timu ya taifa. Ninaamini katika maamuzi niliyoyachukua. Nimechukua uamuzi huu kwa ajili yangu pamoja na watu wangu waliotaka iwe hivi. Nimepambana sana, lakini ninaondoka nikiwa sijafanikiwa”.
Yalikuwa ni maneno yake wakatia kizungumzia kuhusu uamuzi wake wa kujiweka kando katika michezo ya Kimataifa akiwa na timu ya Taifa. Bila shaka maamuzi haya yatakuwa pigo jingine kwa Argentina.
Ndiyo, maamuzi hayo yamekuwa pigo kubwa kwa Argentina kiasi ambacho hata Rais wa Argentina ameshindwa kukaa kimya, amejikuta akizungumza kitu kumtaka nyota huyo kuendelea kukitumikia kikosi hicho.
Tangu atangaze kustaafu, thamani ya Messi pale Argentina imekuwa juu kwa sasa tofauti na ilivyokuwa kabla. Wapo waliojikuta wakishika mabango barabarani kumtaka Messi abadili uamuzi wake.
Inawezekana Waargentina wamekumbuka shuka wakati kumekwisha kucha. Inawezekana wangempa heshima hii kabla wala asingechukua maamuzi haya aliyoamua kuyachukua.
Kwanini Argentina, Kwanini Lionel Messi? Je atabadili msimamo wake? Hapana shaka nyakati zitatupatia majibu stahiki.
(0767 57 32 87)
Post a Comment