Yanga kesho Jumamosi itatupa karata yake ya tatu kwenye hatua ya
makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, CAF, kwa kuikabili
Madeama ya Ghana.
Mpambano huo wa Kundi A, utapigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam
kuanzia saa 10:30, na unatarajiwa kushuhudiwa na idadi kubwa ya
mashabiki kutokana na timu zote mbili kuwa na hesabu za kutaka kutinga
hatua ya nusu fainali.
Yanga inayoshika nafasi ya mwisho kwenye kundi hilo ikiwa haina pointi
yoyote huo utakuwa mchezo wake wa pili kucheza nyumbani na wa mwisho
kwenye mzunguko wa kwanza inalazimika kushindi ili angalau iweze kupanda
hadi nafasi ya tatu na kuwashusha Madeama waliopo nafasi hiyo wakiwa na
pointi moja.
Katika michezo yake miwili ya mwanzo Yanga ilipoteza baada ya
kufungwa 1-0 na MO Bejaia ya Algeria ikiwa ugenini na baadaye ilicheza
na Mabingwa wa Afrika TP Mazembe nyumbani Dar es Salaam na kukubali
kipigo kama hicho ambacho kiliishusha timu hiyo hadi nafasi ya mwisho.
Mchezo wa kesho unatarajiwa kuwa na presha kubwa kwa wenyeji Yanga,
ambao watakuwa wanahitaji ushindi tena mbele ya kundi kubwa la mashabiki
wao ambao bado wanamatumaini na timu yao kuiona ikicheza nusu fainali
ya michuano yao mwaka huu.
Katika mchezo wa kesho Yanga itamkosa mchezaji mmoja Kelvin Yondani
anayecheza beki wa kati kutokana na kuwa na kadi mbili za njano, lakini
uwepo na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye pia ni nahodha wa timu hiyo
kuna punguza presha katika upande wa ulinzi.
Furaha kubwa kwa kocha Hans van der Pluijm wa Yanga kesho ni kurejea
dimbani kwa mshambuliaji wake Amissi Tambwe, ambaye aliukosa mchezo
uliopita kutokana na kuwa na kadi mbili za njano ingawa mchezaji huyo
alikuwa akisumbuliwa na malaria lakini taarifa zinasema kwasasa yupo
fiti na huenda akacheza mchezo huo.
Kocha Pluijm, amesema ameupa uzito mkuba mchezo huo lengo lake ni
kuhakikisha wanapata pointi tatu ili kufufua matumaini ya kucheza nusu
fainali kama ambavyo walijipangia mwanzoni na mchezo huo ndiyo wenye
tiketi yao ya kufika huko wanapopataka.
“Tutacheza kwa kushambulia muda wote wa mchezo ninachotaka kipindi
cha kwanza tupate mabao mawili ya haraka ili tuwe na kazi nyepesi
tutakaoingia kipindi cha pili kwasababu ingawa Madeama ni timu ambayo
naijua lakini wanaweza kubadilika kwasababu siyo timu mbaya,”amesema
Pluijm.
Mdachi huyo amesema baada ya Tambwe kupona anatarajia kutumia mfumo
wa 4-4-2 kwa kumwanzisha kwenye ushambuliaji Tambwe na Donald Ngoma,
huku viungo wa pembeni akiwatumia Juma Mahadhi na Simon Msuva. Ambao nao
wanauwezo mkubwa wa kufunga licha ya kutokea pembeni.
Pluijm amesema maandalizi waliyoyafanya kwa wiki mbili baada ya
mchezo na TP Mazembe yanampa uhakika wa kushinda mchezo huo na kuwataka
mashabiki wa Yanga kufika kwa wingi uwanjani akiahidi kuwapa raha ile
ambayo wameizoea kuiona kwenye Ligi ya Vodacom Tanzania.
Madeama tayari wamewasili Tanzania tangu jana mchana wakiwa na
msafara wa watu 32 wakiwemo wachezaji 19, na kocha wake Prince Yaw
Owusu, amejitapa amekuja Tanzania kuchua pointi tatu kwa kua anawajua
vizuri Yanga baada ya kuiona kwenye michuano ya Kombe la Kagame
iliyofanyika Tanzania Julai 2015 yeye akiwa kocha msaidizi kwenye klabu
ya Al Khartoum ya Sudan.
“Naijua Yanga ni timu nzuri inawachezaji wazuri lakini hatulihofii
hilo tumekuja kwa lengo moja la kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu
nimezungumza na wachezaji wangu na kuwambia ubora na udhaifu wa Yanga
kwaiyo naamini mipango yetu itatimia ingawa wao wanafika kwa mara ya
kwanza Tanzania,”amesema Owusu.
Kocha huyo raia wa Ghana amesema kikosi chake kinaingia kwenye mchezo
huo akijivunia pointi moja waliyokuwa nayo baada ya kutoka sare ya bila
kufungana na MO Bejaia hivyo anauhakika wa kupata pointi tatu ili
kufikisha alama nne ambazo zitawapa nafasi ya kucheza nusu fainali ya
michuano hiyo mwaka huu.
Kocha Owusu ataingia kwenye mchezo huo akifurahia kurejea kwa viungo
wake wawili Kwesi Donsu na Eric Kwakwa, ambao walikuwa majeruhi baada ya
kuumia kwenye mechi za ligi ya Ghana.
Chanzo: Goal.com
Post a Comment