Timu ya mpira wa miguu ya maveterani wa Songea (Songea Veterans Fc) ya mjini songea leo itajitupa kwenye dimba la Tamasha lililopo kwenye mji mdogo wa Peramiho kwaajili ya kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya vijana wa Red Star ya Peramiho.
Akizungumza na mwandishi wa mtandao huu mwenyekiti wa maveterani hao bwana Lenzian Mpangwa amesema pamoja na kuwa wao kwa sasa umri wao umekwenda inawalazimu kucheza michezo mingi ya kirafiki na timu za vijana kwakuwa mkoa wa Ruvuma na Manispaa ya Songea umekua na uhaba wa timu za maveterani hivyo kuwalazimu kucheza na timu za vijana ili kuusaka utimamu wa mwili na akili.
Nae nahodha wa timu hiyo ya Songea Veterani Victor Swela (Shimba) amesema pamoja na timu yao kucheza michezo mingi na timu za vijana wamekua wakitoa upinzani wa nguvu kwa vijana hao na imekua ni nadra sana kwao kupoteza mchezo kwani wao wamekua ni watu ambao wanacheza kwa kufuata kanuni zaidi tofauti na vijana wa sasa ambao wamekua na papara sana wawapo uwanjani.
Akitoa tathimini ya kikosi kitakochokwenda kucheza pale Peramiho hii leo mhasibu wa maveterani hao bwana Jaribuni Mangoma amedai kuwa kikosi hicho kitakwenda kikiwa kamili licha ya kuendelea kuwakosa washambuliaji wake hatari Godfrey Mvula na Hossam Ulaya wanaosumbuliwa na majeruhi.
"Kikosi chetu kikokamili kabisa licha ya kuwakosa washambuliaji wetu wawili Goddy Mvula anayeuguza majeraha yake ya kuchaniaka nyama za paja maumivu aliyoyapata kwenye mchezo ambao timu yetu ilipoteza kwa jumla ya magoli 6:2 dhidi ya Lizaboni Jubior na Hossam Ulaya aliyeumia kifundo cha mguu wa kulia siku ya Iddi Pili tulipokua pale wilayani Namtumbo tulipokua tukicheza dhidi ya vijana wa Bodaboda Fc ya wilayani Namtumbo ambapo tulipata ushindi wa magoli 4:2" Alifafanua Mangoma.
Timu ya Songea Veterani imekua kwenye mazoezi ya nguvu ikijiandaa kwa safari ya mkoani Lindi inakotarajia kwenda kushiriki bonanza la kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere hapo baadae mwezi wa kumi mwaka huu.
Post a Comment