0
Na Oswald Ngonyani

Kwanini pombe? Inawezekana swali hili likawa linaulizwa na wengi juu ya uso wa dunia, lakini kwa kiasi kikubwa majibu ya swali hili yakakosekana.

Maisha ya mwanadamu yametawaliwa na vitu vingi sana vizuri, lakini kwa bahati mbaya sana asilimia kubwa ya vitu hivyo vina madhara kama mtumiaji atavitumia vitu hivyo pasi kuwa na kikomo.

Leo hii nchini Tanzania tunatumia muda mwingi kumhurumia Malkia wa kuchezesha nyonga, Mwandada Ray C kwa sababu ya kuathirika na madawa ya kulevya.

Yupo wapi Chid Benz, aliyekuwa anahusudiwa hata na watoto wadogo majumbani? Pamoja na kuanza kurudi katika hali yake ya kawaida kwa sasa lakini kwa kiasi kikubwa Ulevi wa madawa ya kulevya umeyayumbisha sana maisha yake.

Ni ukweli unaouma lakini acha tu niuweke wazi ili jamii ya watanzania na duniani kwa ujumla iweze kuadilika.

Tuachane na habari za akina Ray C na Chid Benz, Tumzungumzie Paul Gascoigne maarufu kama Gazza.

Shujaa huyu wa soka alikuwa kila kitu nchini England hususani katika miaka ya 80 na 90. Kwa kiasi kikubwa ulevi umepoteza heshima yake pale England na duniani kwa ujumla.

Ameiruhusu pombe imtawale na kumuendesha kama gari bovu. Kuna wakati huwa anakunywa kupitiliza mpaka anapoteza fahamu. Ndivyo yalivyo maisha yake kwa sasa, anatia sana huruma.

Amefikia hapa Gazza, Mwanasoka aliyependwa na kuhusudiwa na wengi katika ardhi ya wapenzi wengi wa kandanda ulimwenguni. Mmoja kati ya viungo bora wa muda wote.

Kwa sasa pombe imesambaa katika mwili wake, pombe imeshinda vita dhidi yake na kujikuta ikifanikiwa kumuongoza. Inatia sana simanzi lakini ndiyo maisha aliyoamua kujichagulia, Gazza ameichagua pombe kuwa msindikizaji wa maisha yake hapa duniani.

Ni ukweli ulio wazi kuwa ndani ya uwanja Mungu alimtunuku kipaji cha kipekee Gazza. Aliijenga vema heshima yake kwa matofali ya machozi jasho na damu ndani ya uwanja. Miguu yake ikampatia heshima na utajiri mkubwa.

Inawezekana alishindwa kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu upekee wa historia yake katika mchezo wa soka ndani na nje ya England.

Inawezekana nafsi yake ilishindwa kubaini kama alikuwa pambo la wengi waliomhusudu na hata kutamani kuja kufanana naye ‘Role model’. Kwa sasa yale maisha mazuri aliyokuwa nayo kabla yamebaki kuwa historia.

Tatizo kubwa alilolifanya ni kufunga pingu za maisha na maji yaitwayo pombe, Mkataba huo wa kudumu ndio unao mtesa mpaka leo, asilimia 99 ya akili yake inawaza pombe, huko  ndipo alipoizika heshima yake katika uso wa dunia.

Leo hii ukimuona Gazza ni kama ‘Ngongoti’ wa Kwenye maonesho ya saba saba. Kwa Gazza mastaa wetu Chid Benz na Ray C wana unafuu mkubwa. Ule utajiri wake mkubwa wa mali na fedha kwa sasa imebaki historia tena akiwa na umri wa kawaida tu wa miaka  49.


Si msaada tena wa familia kama ilivyokuwa kabla, badala yake amekuwa mzigo wa familia. Ameyavuruga maisha yake yeye mwenyewe kwa kuipa nafasi pombe imtawale.

Ukiangalia kwenye ‘highlights’ za euro 2016 zilizomalizika wikiendi iliyopita,  yule mtu anayepiga kanzu kwa mguu wa kushoto halafu anaunga kwa mguu wa kulia na kufunga ndio Paul Gascoigne Gazza ninayemzungumzia hapa.

Nakumbuka ilikuwa katika Mashindano ya Euro 1996 (Mashindano ya kwanza kutumia jina la Euro). Ilikuwa ni katika mchezo mkali kati ya England dhidi ya Scotland.

Wakati fulani Wayne Rooney alipachikwa jina la Gazza na Waingereza kama dua ya Waingereza kumuombea ili aweze kuchukua nafasi ya Gazza huyu ninayemzungumzia hapa.

Pamoja na kumtunuku Rooney jina hilo lakini bado Uingereza haijawahi kuwa ile ya akina Gazza, Uingereza ya moto inayoendelea kukumbukwa mpaka sasa katika historia ya soka la kimataifa.

Huyu ndiye Gazza aliyeikonga dunia kwa ustadi wake wa kuuchezea mpira uwanjani.

Huyu ndiye Gazza aliyekuwa kila kitu pale England, Gazza anayekata tawi la mti akiwa amelikalia. Bila shaka mwisho wake utakuwa wa kusikitisha sana huku akihukumiwa na historia yake pendevu katika mawanda ya soka ya dunia.

(0767 573287)

Post a Comment

 
Top