0

Uongozi wa klabu ya Majimaji ya mjini Songea umesema bado haujakata tamaa kwenye suala la kuongeza mkataba na mwalimu wa timu hiyo Kally Ongala ambaye kwa siku za hivi karibuni ametajwa kutaka kuachana na timu hiyo aliyoitumikia kwa nusu msimu wa ligi kuu iliyokwisha.

Mkataba wa Ongala na Wanalizombe umemalizika mwisho ni mwa msimu uliopita huku viongozi wa klabu hiyo wakiwa kimya kuzungumza kuhusiana na kandarasi mpya ya mchezaji huyo wazamani wa Azam FC kutokana na sintofahamu iliyojitokeza ya kumalizika kwa mkataba wa udhamini baina ya timu hiyo na kampuni ya ufuaji umeme ya Symbion Power.

"Ni kweli tunasikia kweli kuna timu kadhaa zimeonesha nia ya kumuhitaji lakini tutapambana kwa nguvu zetu zote kuhakikisha kuwa tunasainiana nae kandarasi mpya mwalimu wetu," alisema afisa habari wa timu hiyo Mtega Narthan.

Kwa upande wa Kally mwenyewe amanukuliwa kudai kuwa mbioni kuachana na timu hiyo kutokana na viongozi wa timu hiyo kukaa kimya kwa muda mrefu baada ya kukamilika kwa msimu wa ligi uliopita.

Aidha Ongala alisema hawezi kurudi kufundisha Majimaji kutokana na kushindwa kufanya maandalizi ya msimu ujao mapema kitu ambacho kitampa wakati mgumu mwanzoni mwa msimu.

Kocha huyo alisema pia alikuwa akihitaji wachezaji watano ndani ya kikosi hicho lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika huku msimu  mpya ukitarajiwa kuanza mwezi ujao.

"Nilikuwa nahitaji wachezaji watano kwa ajili ya kuongeza nguvu ndani ya timu lakini uongozi upo kimya ligi ipo njiani kuanza sasa  mazingira kama hayo sitoweza kurudi tena," alimaliza Ongala ambaye ni mtoto wa mwanamuziki wa zamani marehemu Dr. Remmy Ongala.

Post a Comment

 
Top