0
Uganda imelazmishwa sare ya mabao 2-2 na Mali katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi D Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN 2016), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee Uwanja wa Rubavu mjini Kigali, Rwanda hapo jana.

Joseph Ochaya alianza kuwafungia Korongo wa Kampala dakika ya 12 akimalizia pasi ya Nahodha, Farouk Miya, kabla ya Sekou Koita kuisawazishia Mali dakika ya 23 akimalizia pasi ya Lassana Samake.

Nahodha Farouk Miya akaifungia The Cranes bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 41 kwa penalti, lakini Hamidou Sinayoko akawakomboa Mali kulala kwa kusawazisha dakika ya 60 baada ya kazi nzuri ya Mamadou Coulibaly.

Katika mchezo uliotangulia wa kundi hilo, kiungo mkongwe Isaac Chansa ameifungia bao pekee Zambia dakika ya 53 ikiwalaza jirani zao Zimbabwe 1-0.

Chipolopolo sasa ndiyo wanaongoza kundi hilo kwa pointi zao tatu, wakifuatiwa na Mali na Uganda, wakati Zimbabwe inashika mkia.

Michuano hiyo itaendelea leo kwa mechi za Kundi A, wenyeji Rwanda wakimenyana na Gabon kabla ya Morocco kupepetana na Ivory Coast Uwanja wa Amahoro, Kigali.

Ikumbukwe katika mechi za kwanza, Rwanda waliifunga Ivory Coast 1-0, wakati Gabon ilitoka sare ya 0-0 na Morocco.

Post a Comment

 
Top