MABAO
mawili ya Ernest Sugira yameipa ushindi wa pili mfululizo Rwanda katika
mchezo wa Kundi A Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN),
inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee kufuatia
ushindi wa 2-1 dhidi ya Gabon leo.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Amahoro, Kigali – Sugira alifunga mabao hayo dakika za 42 akimalizia pasi ya Jacques Tuyisenge na dakika ya 47 akiunganisha pasi ya Dominique Nshuti.
Mchezo mwingine wa kundi hilo leo, bao pekee la penalti la Krahire Yannick Zakri dakika ya 10 limeipa Ivory Coast ushindi wa 1-0 dhidi ya Morocco.
Sasa Rwanda inajihakikishia kwenda Nusu Fainali kuelekea mechi yake ya mwisho ya kundi hilo dhidi ya Morocco, baada ya kufikisha pointi sita kutokana na mechi mbili, ikiongoza Kundi A ikifuatiwa na Ivory Coast yenye pointi tatu.
Ivory Coast inaweza kufikisha pointi sita ikishinda mechi ya mwisho dhidi ya Gabon, wakati Morocco na Gabon hata zikishinda zitamaliza na pointi nne – hivyo haziwezi kuwazuia Rwanda kwenda Nusu Fainali.
Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi za Kundi B, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC ikimenyana na Angola na Cameroon na Ethiopia Uwanja wa Huye.
Post a Comment