Mechi za michuano ya kombe la FA, hatua ya 32 bora kuelekea 16 bora
zimepangwa kuchezwa wikiendi hii Jumamosi na Jumapili katika viwanja
tofauti nchini.
Kesho Jumamosi Jumla ya timu sita zitashuka dimbani kusaka ushindi
ambao utawapeleka katika hatua inayofuata ya 16 bora huku changamoto
kubwa ikiwemo kwa klabu za Ligi ya Vodacom ndani yake.
Mchezo unaozungumzia sana kesho ni ule utakaopigwa uwanja wa Jamhuri
Morogoro kati ya wenyeji Burkinafaso inayoshiriki daraja la kwanza
itakapo ikabili Simba.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kwasababu Burkinafaso
ndiyo mabingwa wa mkoa wa Morogoro na siyo timu ya kubeza ingawa haina
matokeo mazuri sana kwenye mechi za kufuzu kucheza Ligi ya Vodacom msimu
ujao.
Simba chini ya kocha Jackson Mayanja itaingia kwa nguvu katika mchezo
huo ikitaka kuendeleza wimbi lake la ushindi wa mechi mbili mfululizo
chini ya kocha huyo msaidizi aliyechukua timu siku chache baada ya
kufukuzwa kwa Dylan Kerr.
Mayanja atataka kushinda mchezo huo ili kuendelea kuimarisha
saikolojia za wachezaji wao kufanya vizuri kwenye Ligi ya Vodacom,
itakayoendelea Januari 30, kwa mzunguko wa pili.
Kule Jijini Mwanza katika michuano hiyo ya FA, timu zenye upinzani wa
jadi Toto Afrika inayoshiriki Ligi ya Vodacom itapambana na Pamba FC,
ya Mwanza mchezo utakaopigwa uwanja wa CCM Kirumba.
Pamba kwa muda mrefu imekuwa ikipambana kurudi Ligi ya Vodacom lakini
imekuwa na wakati mgumu na haina matokeo mazuri na kuwaacha Toto
wakitawala ingawa na yenyewe imekuwa ikipanda na kushuka.
Katika pambano la kesho litakuwa na ushindani wa aina yake na siyo
rahisi kutabiri ni timu gani inaweza kushinda kwasababu hata Toto
wamekuwa na matokeo mabaya kwenye mechi mbili za ligi walizocheza hivi
karibuni.
Nayo Ndanda FC, kesho watakuwa nyumbani uwanja wa Nangwanda Sijaona
kucheza na Mshikamno FC timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza.
Ndanda itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya
ushindi wa mabao 4-1, dhidi ya Mbeya City kwaiyo matokeo hayo wanaweza
kuwachangamoto ya kuweza kupata ushindi kwenye mchezo huo.
Mshikamano FC, ni timu yenye uwezo wa kati katika michuano ya Ligi daraja la pili sawa na Ndanda FC, ambayo ukiacha kuwa na wachezaji wenye majina na
uzoefu havitofautiani na uwezo wa kipesa na Mshikamano kwaiyo chochote
kinaweza kutoke kwenye mchezo huo.
Baada ya michezo huyo Jumapili vinara wa Ligi ya Vodacom Tanzania
Yanga watashuka uwanja wa taifa kuwakabili Friends Rangers.
Friend Rangers moja ya timu ngumu kwenye ligi daraja la kwanza
haipewi nafasi ya kushinda mchezo huo lakini Yanga wanalazimika kufanya
kazi ya ziada ili kushinda mchezo huo.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo wa Jumapili ikiwa na kumbukumbu
nzuri ya kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni lakini pia ikishinda
kwa idadi kubwa ya ushindi wa mabao 5-0, huku Amissi Tambwe akifunga
Hat- trick.
Njombe Mji watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa
Amani Makambako, huku Stand United wakicheza dhidi ya Mwadui FC katika
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Pia michuano hiyo itaendelea Jumatatu, Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa
Rhino Rangers katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Panone FC
dhidi ya Madini FC katika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi na African Lyon
wakiwa wenyeji wa Azam katika Uwanja wa Karume, Dar es salaam.
Jumanne Mtibwa Sugar wataikaribisha Abajalo FC Uwanja wa Jamhuri
mjini Morogoro, Lipuli dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Wambi Mafinga,
African Sports dhidi ya Coastal Union Mkwakwani jijini Tanga, na Geita
Gold watakuwa wenyeji wa Mgambo Shooting katika Uwanja wa Nyankumbu
mjini Geita.
Singida United watacheza dhidi ya Mvuvumwa Jumatano katika Uwanja wa
Namfua mjini Singida, na mchezo wa mwisho utachezwa Februari Mosi katika
ya Wenda FC dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mpaka sasa timu ya JKT Mlale pekee ndio imeshafuzu kwa mzunguko wa
nne baada ya kuiondosha Majimaji kwa mabao 2-1, katia mchezo uliochezwa
wiki iliyopita kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Bingwa wa michuano ya Kombe la FA ataiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF CC) mwaka 2017
Post a Comment