Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa
kuendelea Jumatano na Alhamisi, mvuto zaidi ukiwa mechi za miamba watatu
wanaofukuzana kileleni, Azam FC, Simba na Yanga SC.
- Yanga kujaribu uwezo wa Kally Ongala ambaye ametangazwa kuwa kocha mpya wa Majimaji FC, Je! atahimili vishindo?
- Kibadeni ataiongoza JKT Ruvu kucheza dhidi ya klabu aliyo na mapenzi nayo ya Simba na
- Azam kuikabili Mgambo JKT baada ya kuvurunda mechi ya wana kimanumanu African Sport.
Yanga SC inaongoza Ligi Kuu kwa wastani wa mabao, ikiwa inalingana
kwa pointi (36) na Azam FC iliyo nafasi ya pili, wakati Simba SC
inafuatia ikiwa na pointi 30.
Azam FC baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na vibonde African Sports
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam wanasafiri hadi Tanga
kuwafuata Mgambo JKT ambayo inaonekana kurejea kwa kasi kwenye ligi kuu mara baada ya kuivurumisha JKT RUVU jumla ya magoli 5-1 kwenye mchezo uliofanyika wikiendi iliyopita.
Mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua utapigwa Jumatano
katika uwanja wa Mkwakwani na Azam FC watahitaji ushindi ili kuendelea
‘kula sahani moja’ na Yanga SC katika mbio za ubingwa.
Hali kadhalika Simba SC nao watakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Jumatano kumenyana na JKT Ruvu katika mchezo ambao utawakutanisha
makocha wa zamani wa Kagera Sugar, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Mganda Jackson Mayanja.
Kibaden, kocha na mchezaji wa zamani wa Simba SC kwa sasa anaiongoza
JKT Ruvu iliyofungwa 5-1 na Mgambo JKT, wakati Mayanja atakuwa kwenye
mchezo wa pili tangu arithi mikoba ya Muingereza, Dylan Kerr Simba SC.
Simba SC inaweza kumkosa mshambuliaji wake tegemeo, Ibrahim Ajib
aliyeumia Jumamosi timu hiyo ikishinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi nyingine za Ligi Kuu Jumatano ni kati ya Stand United na Toto
Africans Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Ndanda FC na Mbeya City
Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Prisons dhidi ya Coastal
Union Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Mabingwa watetezi, Yanga SC wao watashuka dimbani Alhamisi kumenyana
na Majimaji ya Songea, iliyo chini ya kocha mpya, Muingereza mwenye
asili ya Tanzania, Kalimangonga Sam Daniel Ongala.
Kali Ongala, mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC na kocha Msaidizi wa
zamani wa Azam FC, huo utakuwa mchezo wake wa pili tangu apewe timu
hiyo, baada ya mwishoni mwa wiki kupata sare ya ugenini ya 1-1 na
Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Yanga SC ambayo haikucheza soka la kuvutia ikishinda 1-0 dhidi ya
Ndanda mwishoni mwa juma, itakutana na majaribu ya wachezaji wake wa
zamani kesho, beki Lulanga Mapunda na mshambuliaji Danny Mrwanda ambao
wapo Majimaji kwa sasa.
Mechi nyingine za Ligi Kuu kesho ni kati ya Mwadui FC na Kagera Sugar
Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na African Sports wataikaribisha
Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Post a Comment