0
Ikicheza kama vile iko nyuma kwa mabao kadhaa, Yanga leo imeisambaratisha bila huruma Majimaji ya Songea mabao 5-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliochezwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Thaban Kamusoko aliwashtua Majimaji kwa bao la mapema la dakika ya nne akitumia pasi nzuri ya Deus Kaseke. Baada ya bao hilo Majimaji inayonolewa na Kalimangonga Ongala ilionyesha utulivu hasa kwenye eneo la kiungo hali iliyopelekea timu hizo kwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao hilo moja pekee.

Kipindi cha pili Yanga iliingia kwa nguvu mpya na katika dakika ya 47 tu Kamusoko alimtengenezea bao safi Donald Ngoma aliyeiandikia Yanga bao la pili.


Baada ya bao la pili Majimaji walianza kupoteana ndipo mshambuliaji hatari Amissi Tambwe alipoanza kutoa adhabu kali kwa Majimaji akifunga bao la tatu katika dakika ya 57 kwa pasi ya Ngoma kabla Kaseke hamjamtengenezea bao jingine kwenye dakika 72.

Ikionekana kama vile pambano hilo lingeisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 4-0, beki wa Majimaji Sadick Gawaza alimzawadia Tambwe bao la tatu kwake na la tano kwa Yanga katika dakika ya 84 baada kufanya uzembe wa kujiangusha na Tambwe akaunasa mpira huo na kumchambua kipa David Burhan.

Kwa ushindi huo Yanga imerudi tena kileleni kwa kufikisha pointi 39 sawa na Azam lakini ikiizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika michezo mingine ya ligi kuu leo, Mwadui FC iliyokuwa nyumbani imeifunga Kagera Sugar mabao 2-1 wakati huko Tanga African Sports imetoka sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar.

Post a Comment

 
Top