Na Oswald Ngonyani
Moja ya vitu vikubwa ambavyo vilinifanya nihamanike
kuvishuhudia katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu VPL 2015/2016 ni uwepo wa
timu kadhaa ambazo kwazo zilikuwa kila kitu katika soka ya enzi zilizopita.
Binafsi nilikuwa nimejipa matumaini ya moja kwa moja kuwa
sasa Mpira wa
Tanzania ulikuwa unazidi kurudi katika hadhi yake,hadhi ile ambayo akina Peter
Tino wa Majimaji walikuwa na majina makubwa zaidi kuliko nyota wa Simba na
Yanga.
Enzi zile
ambazo mtoto mdogo wa darasa la tano alikuwa ana uwezo wa kukutajia majina ya
wachezaji wote wa kikosi cha kwanza cha Majimaji ama timu ya Pamba FC ya Mwanza.
Nyakati ambazo
soka ilikuwa inachezwa mguuni badala ya mdomoni. Nyakati tamu zaidi ambazo Wana
Ruvuma ‘wamezimisi’ na kuitaka timu yao ifanye vile ambavyo ilikuwa inafanya.
Angalau Mwadui
FC wameonekana kuimarika, Lakini kwa namna fulani naiona hali mbaya zaidi kwa timu
yangu ya nyumbani Majimaji FC, ambapo tamati yake ya duru la kwanza la Ligi
(VPL 2015/2016) imehitimishwa kwa kipigo cha mbwa mwizi.
Inawezekana
wachezaji wa Majimaji walikwenda Taifa pasipo kujua kama walikuwa wanakwenda
kukutana na mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Tanzania bara.
Inawezekana
Majimaji FC walikuwa hawajui kama wanakwenda kukutana na bingwa mtetezi wa VPL,
kilichotokea baada ya mchezo husika ilikuwa ni dhahama iliyozidi kuleta hasira
kwa wanasongea wengi.
Labda kiwango
cha Yanga kilikuwa cha juu mno kwa Majimaji, lakini mpaka sasa bado sijaijua
azma sahihi ya mlinzi Sadick Gawaza katika dakika ile ya 84.
Tofauti na
enzi za zilipendwa, siku hizi mchezo wa mpira unachezwa hadharani. Usipoenda
uwanjani unapata wasaa wa kuangalia kwenye luninga. Bila shaka Gawaza aliingia Taifa
na taswira ya Ligi za ndondo za kule Peramiho, Songea.
Pengine
alijitoa ufahamu wa nani alikuwa anakabana naye, labda alifikiri anakabana na Dulla
wa Peramiho Stars au Moses Pajero wa Red Stars katika mashindano ya Njunde Cup
au Ansgar Cup.
Bila shaka
alipata jawabu baada ya nyavu kutikisika. Ni vigumu sana kufanya masihara kama
yale na kusalimika mbele ya miguu yenye uchu wa magoli ya Mrundi Amiss Tambwe.
Kuna kila
dalili nyakati hizi zikawa ngumu zaidi kwake kwa sasa, pengine idadi hii kubwa
ya magoli waliyofungwa inaweza kuwa kizugio kwake, lakini hata hivyo sidhani
kama Wanaruvuma wanaweza kumwelewa kirahisi.
Niliufuatilia
kinaganaga mchezo ule, mwisho wa siku timu ya Majimaji imeonekana kuwa timu
kibonde zaidi inapocheza katika uwanja wa Taifa. Katika mechi mbili ilizocheza
na Simba na Yanga imekubali kufungwa magoli 11, aibu iliyoje.
Mengi yanaweza
kuzungumzwa kwa sasa kuhusiana na kinachoendelea kwa kikosi husika huku
mashinikizo ya mashabiki yakiendelea kupewa nafasi kubwa zaidi na hata kuzidi
kuwachanganya wachezaji.
Wakati goli la
nne likifungwa, nilimtazama Gody Mvula, Meneja wa timu lakini pia Hassan Banyai
Mwalimu msaidizi wa timu na kujikuta nikisononeka moyoni.
Uso wa kila
mmoja wao ulionekana kuwa na vitu vingi zaidi vilivyojificha. Wawili hawa kila mmoja
wao amekuwa akipigiwa kelele sana na mashabiki na Viongozi fulani wa Chama cha
Mpira cha Mkoa wa Ruvuma (FARU).
Ninaweza
nikamtetea Banyai kwa matokeo haya yanayotukia kila leo, kwa sababu nyuma yake
kuna makocha wakuu ambao ndio haswa wanaohusika na jukumu zima la upangaji wa
kikosi, hapa ninamzungumzia Mika Lonnstrom aliyerudi kwao Finland na Kalimangonga
Ongalla Kocha wa sasa.
Kuhusu Mvula,
sitaki nimzungumzie kwa sasa lakini bado suala la Kiuongozi ndani ya timu
halijawa katika usahihi wake, ndio maana leo hii ni kitu kilichozoeleka mno
kumuona mchezaji wa Majimaji akilia njaa.
Waswahili wana
msemo wao mmoja unaosema ‘Moto ukiwaka ndani kwako usimtafute mchomaji,
utapoteza mali zako bure, uuzime kwanza’. Hapa kuna kitu nataka kukisisitiza.
Wakati timu
shiriki katika VPL zikijipanga vema katika mwanzo wa raundi ya pili ya Ligi
husika, ni wakati muafaka sasa kwa Wanasongea wote kuungana na kuwa kitu kimoja
badala ya kuendekeza hulka za kumtafuta mchawi.
Tukumbuke haya
yanatokea katika kipindi ambacho tayari timu ipo chini ya Mwalimu mpya,
Kalimangonga Ongala na ilikuwa ni mojawapo ya mechi yake ya awali kabisa kuwa
katika benchi.
Inawezekana
kuna kitu hakiendi sawa ndani ya timu lakini je kwa hali ilivyo sasa ni sahihi
kuanza kutafutana wenyewe kwa wenyewe wakati Ligi ndiyo kwanza inapamba moto?
Katika hili,
ni jambo jema zaidi iwapo tutajivika mkaja kwa lengo la kuutanguliza mbele
uzalendo wa Uanaruvuma wetu na hata kuweza kuwashawishi wadau na viongozi wote
wa ligi kuhakikisha kuwa wachezaji wote wanapewa stahiki zao zote wanazodai
kila kunapokucha.
Kama
Mwanaruvuma mwenye uzalendo na timu yangu ya nyumani ninaumia moyo kwa matokeo
haya mabaya tunayo kumbana nayo kila kukicha. Sipendezwi na baadhi ya watu
wanaotukejeli kwa kuiita timu yetu kuwa ni timu ya Kampeni.
Nasutwa na
nafsi yangu kwa kushindwa kutoa ushauri stahiki pale ilipotakiwa kuutoa japo
mengi yalikwishawahi kuzungumzwa kabla na wazalendo wengine wengi.
Sitaki kuwa
mtuhumiwa pale timu itakapokumbwa na dhahama ya kushuka daraja, sitaki kadhia
hiyo itokee na hapa ninawataka wanaruvuma wote kuhakikisha kuwa hali hiyo
haitokei asilani.
Jicho langu la
tatu linaiona Majimaji ikihangaika kupambana kwa lengo la kujihakikishia kusalia
katika nafasi salama ya kutoshuka daraja.
Hii hali ni ya
aibu kubwa sana kwa klabu yetu hii ambayo ni miongoni mwa vilabu vichache
vyenye heshima iliyotukuka nchini Tanzania.
Inashika
nafasi ya 13 ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza michezo yote 15 ya mzunguko wa
kwanza.Bila shaka michezo ya mzunguko wa pili itakuwa migumu zaidi kwa sababu
kila timu itakuwa inapambana kujinusuru.
Ni wakati
muafaka sasa akili za Kalimangonga Ongala na msaidizi wake kutakiwa kufanya
kazi ya ziada zaidi ili kutengeneza kikosi kilichoshikamana na chenye uwezo wa
kucheza kitimu zaidi kwa sababu katika mechi nyingi za mzunguko wa kwanza timu
ilionekana ikicheza kwa minajili ya ‘bora liende’
Kihistoria, Majimaji
ilianzishwa mwaka 1977 na kupanda Ligi Kuu mwaka 1978. Kuanzia hapo ilicheza
Ligi kwa miaka 32 mpaka iliposhuka mwaka 2000.
Kuanzia hapo
ilianza kucheza mchezo wa ‘panda shuka’ wakati ilipopanda mwaka 2002 na kushuka
mwaka 2005. Ikapanda tena mwaka 2008 na kushuka mwaka 2010. Hatimaye imepanda
tena mwaka jana 2015.
Wababe hawa wa
Kanda ya Kusini wanahitaji kurudi katika uimara thabiti kama ule waliocheza
Ligi kuanzia mwaka 1978 hadi 2000 bila ya kushuka.
Hii itategemea
watakuja vipi katika duru hili la pili, lakini katika duru la kwanza, hakuna
cha maana walichokifanya zaidi ya ule ushindi mfululizo wa mechi tatu za kwanza
waliokuwa wameupata wakiwa nyumbani.
Hatua
iliyobakia ni hatua ngumu sana. Hatua ya
lala salama ambayo tutashuhudia ukatili wa washambuliaji wengi mbele ya lango
lakini pia umaridadi wa mabeki wengi wasio na masihara ndani ya 18.
Tuendelee
kusubiri na kujiuliza, Je! Ni kweli watarudi kivingine na kutamba kama zama za
akina Peter Tino, Mhando Mdeve, Peter Mhina, Octavian Mrope na wengineo?
Wakati
utatupatia majibu stahiki.
(0767 57 32 87)
Post a Comment