MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta anaondoka asubuhi ya leo
kwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
kujiunga na klabu yake, TP Mazembe wakati sakata la uhamisho wake
likiendelea.
Samatta anaondoka na Maofisa wa Wizara ya Michezo walioteuliwa kwenda kuzungumza na Rais wa TP Mazembe, Moise Katumbi kumshawishi amruhusu mchezaji huyo kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji.
Lakini iwapo Katumbi ataendelea kusistiza msimamo wake wa kutaka Samatta aende Nantes ya Ufaransa, basi mchezaji huyo ataamua kubaki Mazembe amalizie miezi yake mitatu ya Mkataba wake ili aondoke kama mchezaji hurumnamo mwezi April.
Taarifa zinasema kuwa klabu ya Genk wako tayari kutoa Euro 800,000
kumnunua Samatta kutoka Mazembe, lakini Moise amesema anataka Euro
Milioni 1.
Aidha, Katumbi anataka asilimia 25 ya mgawo iwapo klabu itakayomnunua Samatta itamuuza kwa klabu nyingine.
Moise anasema Nantes wamekubali kutoa Euro Milioni 1 na mgawo wa asilimia 25, wakati Genk wamekomea kwenye Euro 800,000 na ofa ya mgawo ya asilimia 20 mchezaji huyo akiuzwa klabu nyingine.
Genk inaona miezi mitatu aliyobakiza Samatta Mazembe ni michache kutoa zaidi ya Euro 800,000 kumnunua na mgawo wa zaidi ya asilimia 20 iwapo itamuuza sehemu nyingine na hapo ndipo wanapotofautiana na Katumbi.
Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo anaamini kwa msimamo wa Samatta kutaka amalizie Mkataba wake Mazembe ili aondoke kama mchezaji huru Aprili, Katumbi anaweza kulainika na kumruhusu nyota huyo aliyeibukia Mbagala, Dar es Salaam ili asikose kabisa.
Na Genk ambao tayari wamekwishasaini Mkataba wa awali na Samatta wapo tayari kumsubiri hadi Aprili atakapomaliza Mkataba wake ili aanze kucheza Agosti.
Wakati huo huo, Rais wa klabu ya Nantes ya Ufaransa, Waldemar Kita amesikitishwa mno na kitendo cha Nahodha huyo mpya wa timu ya taifa ya Tanzania kukataa ofa ya kujiunga na klabu yake.
Kita
alitegemea sana Mazembe aliofikia nao makubaliano kumsaidia kumpata
Mwanasoka huyo Bora Anayecheza Afrika, lakini sasa wazi amekwama.
Ikumbukwe tayari Samatta amepatiwa viza na Ubalozi wa Ubelgiji kwenda kuanza maisha mapya KRC Genk.
Ikumbukwe tayari Samatta amepatiwa viza na Ubalozi wa Ubelgiji kwenda kuanza maisha mapya KRC Genk.
Samatta aliyejiunga na TP Mazembe mwaka 2011 akitokea Simba SC aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon, hadi sasa ameichezea klabu hiyo mechi 103 na kuifungia mabao 60.
Ndani ya mechi hizo, kijana huyo wa umri wa miaka 24, ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mazembe, huku naye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.
Post a Comment