Mlinda mlango wa klabu ya Manchester United David De Gea huenda akawa golikipa anayelipwa mshahara mkubwa zaidi katika historia ya soka la nchini Uingereza endapo kama atakubaliana na ofa babukubwa aliyowekewa mezani na klabu yake ya Manchester United.
Mlinda mlango huyo ambaye amekuwa muhimili imara wa lango la klabu ya Manchester United msimu huu amekuwa akitajwa kutaka kujiunga na Magalaktiko wa klabu ya Real Madrid ambao wako kwenye mchakato kabambe wa kumsaka mrithi wa nyanda wa sasa wa klabu hiyo Muhispania Iker Casillas.
Taarifa zinadai kuwa meneja wa klabu ya Manchester United, Mholanzi Louis van Gaal ameonekana kuwashauri mabosi wake kuwa wapambane kwa udi na uvumba kuhakikisha kuwa mlinda mlango huyo haondoki ndani ya klabu hiyo na katika kutekeleza maagizo hayo tayari mabosi wa klabu hiyo wamekwisha tangaza kuwa wanataka kumpa mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya paundi milioni 36.
Kwenye mkataba huo mpya anaotarajiwa kupewa De Gea itashuhudiwa akijinyakulia kitita cha jumla ya paundi za Uingereza 140,000/= kwa wiki kama mshahara wake kiasi kinachotajwa kuwa ni zaidi ya mara mbili ya mshahara wake wa sasa.
Mshahara huo utamfanya mlinda mlango huyo kuwa na mshahara mnono kuwazidi mlindamilango wa klabu ya Manchester City, Joe Hart, ambaye anatajwa kuwa nae yuko mbioni kusaini mkataba mpya na matajiri hao wa jiji la Manchester.
Post a Comment