Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Manuel Neuer ndio wachezaji watatu waliotajwa na Shirikisho la soka Ulimwenguni FIFA kuwa ndio wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa Dunia kwa mwaka 2014.
Mreno Cristiano Ronaldo ameiongoza vyema klabu yake ya Real Madrid kutwaa taji la ligi ya mabingwa barani Ulaya binafsi akitupia takribani magoli 17 wavuni wakati Manuel Neuer ndiye aliyeisaidia kwa kiasi kikubwa timu ya Taifa ya Ujerumani kutwaa taji la kombe la Dunia kwenye fainali za mwaka huu zilizofanyika huko nchini Brazil lakini pia ndiye aliyekua nguzo imara katika kuhakikisha kuwa anaisaidia klabu yake ya Bayern Munich kutwaa taji la Bundesliga msimu uliopita.
Messi anaonekana kutokuwa na msimu mzuri sana katika ngazi ya klabu lakini alikua muhimili imara katika kuhakikisha kuwa anaisaidia timu yake ya taifa ya Argentina inafika katika hatua ya fainali ya michuano ya kombe la dunia kule nchini Brazil lakini anajivunia kuweka rekodi mpya ya kuwa mfungaji mwenye magoli mengi zaidi kwenye michuano ya Champions League na La Liga akiwa na umri mdogo kabisa wa miaka 27.
Kwa upande wa soka la akina mama kutakua na kimbembe baina ya Mjerumani Nadine Kessler, Marta wa Brazil na Mmarekani Abby Wambachhere kwenye tuzo ya mchezaji bora wa kike kwenye tuzo zinazotarajiwa kutangazwa mnamo mwezi wa Januari 12 mwakani.
Kwa upande wa Mameneja shughuli itakua baina ya kocha aliyeiwezesha timu ya taifa ya Ujerumani kutwaa taji la Dunia Joachim Low, ambaye atapambana na kocha aliyetwaa kikombe cha UEFA Champions League Carlo Ancelotti na kocha aliyeiwezesha timu ya Atletico Madrid kutwaa ubingwa wa La Liga na kufikia fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya Diego Simeone watakaokuwa wanawania tuzo ya mwalimu bora wa mwaka kwa upande wa akina baba.
Kwa upande wa kumbukumbu ya goli bora la michuano ya kombe la Dunia na mashindano mbalimbali yaliyochini ya FIFA (Puskas) mwanamama raia wa Ireland Stephanie Roche atavaana uso kwa uso na mababa wawili James Rodriguez na Robin van Persie watakua wanawania tuzo ya goli bora la mwaka.
Halikadhalika Ralf Kellerman, Maren Meinert na Norio Sasaki ndio majina matatu ya wanawake wanaowania tuzo ya kocha bora wa mwaka kwa upande wa wanawake. FIFA pia itatumia nafasi hiyo kukitangaza kikosi cha mwaka cha FIFA kitakachotokana na orodha ya wachezaji 55 waliokuwa kwenye orodha ya awali.
Post a Comment