TIMU ya soka ya Azam Fc
imebanwa mbavu na Ndanda Fc kwa kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo
wa kiporo wa ligi kuu ya Vodacom uliopigwa kwenye dimba la Azam Complex
Chamazi.
Azam walikuwa wa kwanza
kupata bao kupitia kwa Ramadhan Singano 'Messi' katika dakika ya 10
akimalizia krosi ya Michael Balou kabla Didier Kavumbagu hajaipatia bao
la pili dakika ya 42 hivyo kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao hayo
mawili.
Kipindi cha pili Ndanda
walionekana kubadilika na kuanza kutengeneza nafasi za mabao ambapo
katika dakika ya 50 jitihada zao zilizaa matunda baada ya Atupele Green
kuipatia bao kwa mkwaju wa penati uliotokana na Paul Ngalema kufanyiwa
madhambi na kipa wa Azam Aishi Manula ndani ya eneo la hatari.
Baada ya bao hilo Ndanda
walicharuka zaidi na kama si kukosa umakini kwa wachezaji wake Omar
Mponda na Salum Minely basi wangeweza kupata mabao mengine katika dakika
za 55 na 68.
Katika dakika ya 86,
Ndanda walijihakikishia kuondoka na pointi moja baada ya beki wa Azam
Aggrey Moris kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa
na Ahmad Msumi aliyeingia kuchukua nafasi ya Minely.
Mabadiliko mengine kwa
upande wa Ndanda ni Burhan Rashid aliyeingia badala ya Masoud Ally huku
Azam wao wakiwatoa Racine Diof, Waziri Salum na Kavumbagu na nafasi zao
zikichukuliwa na Mudathir Yahaya, David Mwantika na John Bocco.
Diof na Pascal Wawa ndio
wachezaji pekee waliozawadiwa kadi za njano katika mchezo huo ambao
matokeo yake ya sare yameifanya Azam ifikishe pointi 52 baada ya kushuka
dimbani mara 23 wakibakia katika nafasi yao ya tatu nyuma ya Simba (57)
na Yanga (53).
Katika mchezo mwingine
wa Ligi kuu ya Vodacom, Majimaji ya mjini Songea imetandika Coastal
Union mabao 2-0 yaliyofungwa na Danny Mrwanda pamoja na Lucas Kikoti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment