Mabingwa watetezi Real Madrid wana kibarua cha ziada kuwachapa
majirani wao Atletico Madrid katika jaribio la nane msimu
huu ili kufuzu kwa nusu fainali yao ya tano ya ligi ya
mabingwa Ulaya.
Tangu walipoilaza Atletico 4-1 katika fainali ya kipute hicho msimu
wa mwaka jana, Real wamejaribu bila ufanisi kupata ushindi dhidi ya mahasimu wao mara saba ikiwemo
sare tasa wiki iliyopita katika mkondo wa kwanza wa robo fainali kwenye dimba la
Vincente Calderon.
Real wamekumbwa na majeraha kwa wachezaji muhimu wakiwemo kiungo Luka
Modric na mshambuliaji Gareth Bale kufuatia maumivu ya goti na paja huku
Marcelo akiwa anatumikia adhabu ya kadi na mshambuliaji Karim Benzema akirejea kutoka kwenye tatizo la goti lililokuwa likimsibu.
Kurejea uwanjani kwa nyota wa Kombe la Dunia wa Colombia, James
Rodriguez, kumewapa Real msisimko mkubwa wa kumudu pigo hilo huku
akifunga mabao mawili katika mechi nne kufuatia miezi miwili ya kuwa nje kwa
majeraha.
“Kabla ya kuondoka, nilikuwa nafunga mabao, kucheza katika kiwango
kizuri na sasa, naonelea niko katika hali hiyo. Nataka kuendelea hivi,
kutumia uwezo wangu kusaidia timu hii kufanikisha malengo muhimu.
“Sote tuna ndoto ya pamoja kuendelea kutoka awamu hii na
nikifanikiwa kufunga pia, itakuwa jambo kubwa. La muhimu zaidi ni kushinda
na kufuzu kutoka mechi hii ngumu zaidi lakini tuko uwanjani mwetu mbele
ya mashabiki wetu. Itakuwa mechi kubwa,” Rodriguez aliambia tovuti rasmi
la Real Madrid.
Atletico wamefungwa goli moja pekee katika mechi zao nane za mwisho
za ligi ya mabingwa na wamezuia maadui wao kupenya goli lao mara saba
msimu huu.
Post a Comment