0
Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager leo imeibuka na ushindi wa bao 1- 0 dhidi ya wenyeji Chad katika mchezo uliopigwa jana katika uwanja wa Omnisport Idriss Mahamat Ouya uliopo jijini N’Djamena.

Kikosi cha Stars kilicheza vizuri kwa maelewano kwa lengo la kusaka bao la mapema, safu ya ushambuliaji ilikuwa mwiba kwa walinzi wa Chad katika dakika 30 za kipindi cha kwanza na kukosa nafasi zaidi ya nne za wazi kupitia kwa Ulimwengu, Farid, Samatta na Kazimoto.
Nahodha Mbwana Samatta ambaye alikua akikiongoza kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa katika nafasi hiyo, aliipatia Tanzania bao la kwanza dakika ya 30 akimalizia pasi ya Farid Mussa aliyewataoka walinzi wa Chad kabla ya kumpasia mfungaji.

Mara baada ya bao hilo wenyeji walikuja juu kusaka bao la kusawazisha, lakini ukuta wa Stars uliokuwa chini ya Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Haji Mwinyi na mlinda mlango Aishi Manula walikua imara kuokoa michomo hiyo.

Kipindi cha pili Stars ilianza kwa kufanya mabadiliko, Mwinyi Kazimoto aliyeumia alimpisha John Bocco na kuongeza nguvu katika sehemu ya ushambuliaji, na kuwapa wakati mgumu walinzi wa Chad.

Dakika ya 73, David Mwantika aliingia kuchukua nafasi ya Farid Mussa, huku Ibrahim Ajibu akiingia dakika ya 80 kuchukua nafasi ya Thomas Ulimwengu, mabadiliko ambayo yaliongeza nguvu kwa stars na kujilinda mpaka mwisho wa mchezo.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Chad 0 –1 Tanzania.

Post a Comment

 
Top