0
TP Mazembe ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imevishwa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya tano baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya USM Alger ya Algeria katika mechi ya marudiano ya fainali iliyochezwa Jumapili ya jana jijini Lubumbashi.

Magoli yalitoka kwa Mtanzania Mbwana Samatta na Mu-Ivory Coast Roger Assale mbele ya mashabiki wao nyumbani mjini Lubumbashi.

Ushindi huo uliwapa Mazembe jumla ya magoli 4-1, baada ya klabu hiyo ya Kongo kushinda 2-1 mechi ya awali mjini Algiers juma lililopita

Samatta alifumania nyavu dakika ya 75 na kuifanya Mazembe kuongoza. Lilikuwa goli la saba la Samatta katika kampeni hizi, jambo linalomfanaya kufungana na Bakry ‘Al Medina’ Babiker wa Al Merreikh ya Sudani.

Assale alihakikisha ushindi unakuwa mnono baada ya kufunga goli safi dakika za majeruhi.

Mazembe inayonolewa na Mfaransa Patrice Carteron ametwaa taji hili kwa mara ya kwanza tangu 2010 walipoigaragaza Esperance ya Tunisia kwa jumla ya magoli 6-1.

Wameshinda pia michuano ya klabu za Afrika mwaka uliopita, na ni klabu pekee ya kusini mwa Jangwa la Sahara kufanikiwa kushinda taji hilo tangu 2004.

Timu za Kaskazini mwa Afrika zimetawala Ligi ya Mabingwa Afrika kwa miaka ya hivi karibuni, timu nane kati ya 10 za mwisho kutwaa ubingwa zikiwa zinatokea Misri au Tunisia.

Lakini kipigo cha mechi ya awali na ushindi wa nyumbani wa Mazembe, ulimaanisha kuwa USM Alger tayari walikuwa na mlima mrefu wa kupanda.

Mafanikio hayo, Mazembe wataiwakilisha Afrika kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Klabu la Fifa baadaye mwaka huu kule Japani.

Chanzo Goal.com

Post a Comment

 
Top